Upembuzi Bomba la Mafuta Uganda – Tanzania umekamilika

Jamii Africa

UPEMBUZI yakinifu katika mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania, umekamilika.

Kazi hiyo ya kupembua, ilifanywa na Serikali ya India, kupitia Jeshi lake la majini, baada ya nchi hizo mbili kukubaliana kutekeleza kazi hiyo.

Kukamilika kwa upembuzi huo ni hatua muhimu, ikiashiria kuanza hivi karibuni kwa kazi ya kutandaza mabomba na kuweka vifaa muhimu ili kukamilisha mradi huo wa mabilioni ya shilingi.

Zaidi ya Sh. trilioni 10 (dola za Marekani bilioni 4), zimewekezwa katika mradi huo mkubwa wa kusafirisha mafuta ghafi.

Mkataba baina ya Tanzania na Uganda unaonesha kuwa kazi ya mradi huo unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni, 2020.

Kazi hiyo ya upembuzi yakinifu katika Bandari ya Tanga, ilihusisha utafiti uliofanywa kwa muda wa mwezi mmoja kwa kutumia meli ya INS Darshak, helikopta pamoja na vifaa vingine vya kisasa.

Katika kukamilisha kazi hiyo, pia wanajeshi wa Tanzania walihusika na walipata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu upembuzi huu, kutoka kwa wataalamu wa kazi hiyo kutoka Jeshi la India.

Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi, lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

Kampuni ya Mafuta ya Total, yenye makao yake makuu Ufaransa, ilishinda zabuni ya ujenzi wa bomba hilo na kuridhiwa na serikali ya Uganda.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *