Serikali kununua ndege mpya 4, moja itabeba abiria 262

Jamii Africa

Rais Magufuli amesema kuwa Serikali itanunua ndege zaidi katika juhudi za kufufua Shirika la Ndege nchini(ATCL). Amesema Serikali itanunua ndege 4 zikiwemo ndege kubwa 3 ambazo zitasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini wanaotoka hasa nchi za Ulaya na Marekani.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar baada ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Masoko ya Afrika kutoka Kampuni ya utengenezaji wa ndege yenye makao yake makuu nchini Marekani, Ndg. Jim Deboo.

Serikali iko kwenye mpango wa kununua ndege aina ya Boeing 787 Dash 8 Dreamliner itakayokuwa ina uwezo wa kubeba abiria 262, itawasili nchini mnamo Juni mwaka 2018.

2

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitazama kitabu cha  picha ya ndege aina ya Boeing 787-8 Dream liner wakati alipokuwa akisikiliza maelezo yake kutoka kwa Mkurugenzi wa mauzo wa kampuni ya Ndege ya Boeing Jim Deboo. Ndege hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 262 na itakuwa na uwezo wa kuruka kutoka nchini Marekani hadi Tanzania bila kutua mahali popote.

Pia amesema kuwa Serikali itanunua ndge moja aina ya Bombadier Q400 Dash NextGen itakayowasili Mwezi Juni mwaka 2017. Ameongeza kuwa ndege mbili aina ya Bombadier CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria 137 na 150 ambazo zitawasili nchini kati ya Mei na Juni, 2018.

Rais Magufuli amesema kuwa malipo ya awali kwa ajili ya ununuzi wa ndege hizo yameshafanyika.

Makubaliano haya ya kununua ndege hizo yanakuja wakati washindani wakuu wa ATCL ambao ni Precision Air na FastJet hapa nchini wakiwa kwenye mkwamo wa kifedha baada ya kufuta baadhi ya safari na kupunguza wafanyakazi.

Pia katika Ukanda wa Afrika Mashariki Shirika la Ndege la Kenya(Kenya Airways) linakumbwa na mgogoro wa kiutawala Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo kujiuzulu baada mashinikizo ya muda mrefu kutoka kwa wafanyakazi wa shirika hilo wakimlaumu kwa utendaji mbovu.

Hata leo, Shirika hilo la Kenya Airways safari zake 9 zilichelewa kufuatia mgomo wa baadhi ya wafanyakazi wake.

Kwa upande wa Uganda, Shirika la Ndege la Air Uganda limesitisha safari zake kwa takribani mwaka wa pili sasa baada ya kushindwa kudumu katika ushindani wa soko.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *