Ufungashaji na uwekaji nembo katika bidhaa kuwaingiza wajasiriamali kwenye soko la ushindani

Jamii Africa

UFUNGASHAJI bora wa bidhaa za kilimo pamoja na uwekaji wa nembo umeleezwa kwamba ndiyo njia pekee itakayowakomboa wajasiriamali ili kuingia kwenye soko la ushindani.

Hayo yalielezwa na Linus Gedi, mtaalam wa ubora wa chakula na viwango, wakati wa mafunzo kwa akinamama wanaotekeleza mradi wa Green Voices nchini Tanzania, ambao sasa wanalenga kilimobiashara kwa kuboresha bidhaa wanazozalisha ili kuongeza tija ikiwa ni pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

Baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na akinamama wa Green Voices Tanzania ambazo zinatokana na mazao mbalimbali kama mihogo, viazi na asali ambazo hazijafungashwa vizuri.

“Ili kuingia kwenye biashara ya ushindani, ni vyema kuzingatia ubora na usafi wa vyakula, lakini ni muhimu zaidi kuangalia vifungashio na kuweka nembo za utambulisho wa bidhaa,” alisema Linus kutoka taasisi ya IMED.

Wakizungumza baada ya semina hiyo iliyofanyika katika Idara ya Uhandisi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hivi karibuni, akinamama hao walisema elimu waliyoipata imewapa mwanga wa kuendeleza miradi yao na kuhakikisha wanaboresha bidhaa zao ili ziwezi kuingia katika soko la ushindani.

Miradi inayotekelezwa kupitia Green Voices Tanzania ni kilimo cha mihogo, kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mbogamboga na utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira ambayo inatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.

“Nilikuwa nimekata tamaa nisijue nitauendelezaje mradi wangu, lakini kwa mafunzo niliyoyapata kutoka kwa wataalam mbalimbali, hakika nimehamasika na kuona kwamba ninaweza kusimama na kusonga mbele,” alisema Farida Makame ambaye anasimamia mradi wa Majiko ya Umeme-Jua mkoani Kilimanjaro.

Farida alisema amehamasishwa zaidi na mafunzo hayo, hususan kutoka kwa Biubwa Ibrahim, Mkurugenzi wa kampuni ya Namaingo Business Agency, ambayo yamefufua matumaini kuhusu kuendeleza mradi huo kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Abiah Magembe anayesimamia mradi wa Usindikaji wa Muhogo na Mtama katika Kijiji cha Kitanga, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, amesema mafunzo ya jinsi ya kufungasha na kuweka nembo kwenye bidhaa yamempa mwanga mkubwa na kwamba sasa yeye na wenzake watazalisha bidhaa zao kwa kujiamini na kuziingiza kwenye soko la ndani na la kimataifa.

“Tunatengeneza bidhaa nyingi zinazotokana na muhogo na zina viwango vizuri, lakini kwa mafunzo tuliyoyapata, sasa tunaweza kuziboresha kwa kuhusisha taasisi husika kama Shirika la Taifa la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ili tuingie kwenye ushindani wa kitaifa na kimataifa,” alisema Bi. Magembe.

Bi. Magembe alisema kwamba, bidhaa wanazozalisha kutokana na zao la muhogo ni unga unaotumika kwa uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate, skonzi, biskuiti, mandazi, mafuta ya lishe, sabuni ya unga, huksi pamoja na bidhaa nyingine nyingi.

Lakini mazao mengine yanayopatikana katika muhogo ni kwamba, mzizi wenyewe ambao unatafunwa mbichi au ukiwa umepikwa au kukaangwa, kwenye futari, miti na majani huweza kuzalisha bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo, karatasi, mafuta, kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo wanga (starch) hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup).

Takwimu za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalisha takriban tani milioni 102.6 kila mwaka.

Tanzania ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika baada ya Nigeria, Ghana na Congo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima na karibu kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.

Regina Kamuli ambaye anasimamia mradi wa Majiko Banifu wilayani Mkuranga, alisema anashukuru wanakikundi wenzake wamejizatiti na sasa wanapata fursa ya kushiriki katika maonyesho mbalimbali yakiwemo ya kilimo kuonyesha majiko hayo ambayo ni rafiki wa mazingira.

“Hivi sasa baada ya kikundi kusajiliwa akinamama wamenufaika na mikopo nafuu kutoka Halmashauri ya Wilaya na kwa mafunzo haya tutaboresha majiko yetu ili tuyanadi katika maeneo mengi nchini Tanzania kwa sababu yanatumia kuni kidogo, hivyo kuokoa mazingira,” alisema Regina.

Magdalena Bukuku anaongoza kikundi cha akinamama wanaoshiriki Kilimo cha Uyoga huko Bunju jijini Dar es Salaam, ambapo anasema mafunzo ya ufungashaji na uwekaji wa nembo yamempa mwanga mkubwa ili kwenda kuboresha bidhaa zao ziingie kwenye ushindani.

“Tunazalisha uyoga kwa wingi kwa sasa na wateja wameongezeka, hata hivyo, ikiwa tutafungasha vizuri na kupanua kilimo chetu tunaweza kulifikia hata soko la kimataifa,” alisema.

 Mariam Bigambo na Monica Kagya wao wanashiriki ufugaji wa nyuki ambapo mbali ya kuvuna asali, lakini wanasaidia kutunza mazingira na kuongeza tija katika mazao ya kilimo kutokana na uchavushaji.

Wakati Mama Bigambo anaendesha Ufugaji wa Nyuki huko Dakawa, Morogoro, Bi. Monica yeye na akinamama wenzake wana jukumu kubwa la kutunza misitu ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe kutokana na Ufugaji wa Nyuki.

“Tunataka tujikite katika kufungasha vizuri asali na kuziwekea nembo ili tuingie kwenye ushindani,” walisema.

Suala la ufungashaji na uwekaji wa nembo nalo limewagusa Esther Muffui, Dkt. Sophia Mlote na Leocadia Vedasto ambao wanashiriki katika kilimo na ukaushaji wa mboga na matunda.

“Tunajihusisha na Ukaushaji wa Mboga na Matunda kule Morogoro, sasa tulikuwa tunashindwa kufungasha vizuri, naamini tumepata mwanga wa namna ya kufungasha bidhaa zetu ili tupate tija zaidi,” alisema Bi. Esther.

Leocadia yeye anashiriki mradi wa Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe huko Ukerewe mkoani Mwanza wakati Dkt. Mlote anashiriki mradi wa Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga Kinyerezi jijini Dar es Salaam.

Naye Evelyn Kahembe ambaye anaendesha Kilimo cha Matunda huko Uvinza, Kigoma, amesema mafunzo hayo yamemuongezea ujasiri wa kuendeleza mradi huo akishirikiana na wanawake wengine huko Kigoma.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela Balisidya, alisema mafunzo waliyoyapata yametoa mwanga mkubwa kwa washiriki na kuleta mtazamo wa kibiashara zaidi tofauti na hapo mwanzo.

“Suala la ufungashaji wa bidhaa ni la muhimu na imekuwa vyema tumepata mafunzo ya kina pamoja na kutembelea taasisi kama Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), tumejifunza mengi ambayo yamebadili mtazamo wetu,” alisema Secelela.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *