Nilipata fursa ya kusikiliza kongamano lililoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika lililofanyika nchini Rwanda mwaka 2014. Kongamano hilo lililoandaliwa kama sehemu ya kuazimisha mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika liliongozwa na tafakuri isemayo ‘Uongozi na Afrika tuitakayo’.
Katika kongamano hilo kulikuwa na wageni waalikwa kutoka sehemu mbalimbali Afrika na duaniani kwa ujumla ila, kilichonifurahisha ni uwepo wa marais waliopo madarakani na wale waliopata kuwa madarakani wakijadili namna uongozi utapelekea kupata Afrika mpya.
Marais waliopata fursa ya kufanya majadiliano walikuwa Rais wa Rwanda Paul Kagame, Makamu wa Rais Kenya William Ruto, Rais mstaafu wa Nigeria Olusegun Obasanjo, Rais mstaafu wa Afrika Kusini Thabo Mbeki na Rais mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa.
Kongamano hili lilikuwa la faraja sana kwangu kusikiliza kwani nilifikiri mengi ila cha msingi kabisa nilichoanza kufikiri hapa na kuona umuhimu wa kuandika makala hii ni je, tunajua Tanzania tuitakayo ni ipi kama taifa?
Bila shaka kwa karne hii ya ishirini na moja ni vyema tukaanza kufikiri kama Afrika kwa pamoja na kuacha hii mipaka tuliyowekewa na wakoloni wakitaka kutufanya dhaifu ili waweze kutunyonya vile walivyotaka. Ila nikitafakari naona ni vigumu kufikiri kama Afrika kwa sasa kwa kuwa bado kama Tanzania hatujajua tunataka kuwa nini kwa sasa.
Ni vema nikaanza kutambua ya kuwa kama taifa tumepiga hatua katika maendeleo mpaka hapa tulipofika leo. Lakini ni vyema pia tukatambua tunachangamoto nyingi sana kiasi kana kwamba tunaweza kushindwa kujivunia maendeleo tuliyonayo leo. Ila leo si vema kuangazia matatizo bali ningependa tuangalie tunahitaji kuwa na Tanzania gani itakayotupatia maendeleo endelevu.
Kitu cha msingi tunachohitaji kama taifa leo ni kuwa na mfumo bora utakaoongoza taifa letu kufika maendeleo tunayoyahitaji. Mfumo huu utatufanya sote kwa pamoja tuamini na kutenda vile ambavyo mfumo utatuongoza. Ila ni vyema tukatambua ya kuwa ili tuwe na mfumo imara wa kuongoza nchi hii lazima uwe shirikishi na utokane na watanzania wenyewe.
Kwa sasa nachelea kusema sijaona Tanzania yetu inaamini na kuongozwa katika mfumo gani ambao sote tunaweza kujivunia. Ili tupate Tanzania tunayoitaka hebu watawala wetu kwa sasa waanzishe mijadala na sisi wananchi kuona tunataka Tanzania ya namna gani. Je, tunaweza kurejea kwenye Azimio la Arusha na Ujamaa na kutizama nini tunaweza kuboresha kitakachoweza kuendana na wakati uliopo sasa.
Kuwa na mfumo thabiti kama taifa utatuwezesha kujitambulisha kama taifa na kuacha kutafuta maendeleo kwa kufanya yale tunayoamriwa na mabebari katika nchi za ulimwengu wa tatu. Leo hii kwa kuwa hatuna mfumo tunaouamini kama taifa tunajikuta tukisikiliza miluzi ya mabwanyenye na kutenda kila wasemalo na tukishindwa kukataa kwa uoga wa kukosa misaada na mikopo. Leo kama taifa tunaishia kuhusudu maendeleo ya wengine na kushindwa kujua nini tufanye kufika hapo.
Kwa sasa msisitizo uliopo ni kwamba tunataka Tanzania ya viwanda, hili ni jambo zuri na linavutia kusikia. Swali linakuja je hii nchi ya viwanda italetwa kwa hisani ya wawekezaji ama na watanzania wenyewe?
Kama tunataka Tanzania itakayopata maendeleo endelevu na tena ya viwanda ni dhahiri sasa lazima turudi katika ubao na kuanza kutafakari ya kuwa elimu tunayotoa kwa vijana wetu leo inakidhi mahitaji? Je, viwanda vitapatikana kwa aina hii ya elimu? Je, elimu yetu haibadiliki imebaki ile ya tangu ukoloni mpaka leo nini tatizo?
Kwa kifupi kama elimu tunayoitoa leo kuanzia shule za msingi mpaka vyuoni haitobadilika, kamwe, hatuwezi kuwa na Tanzania ya viwanda vya watanzania wenyewe ila tutakuwa na Tanzania ya viwanda vya wawekezaji huku watanzania wakibaki kuwa manamba katika viwanda hivyo wakilipwa mishahara kiduchu na kuleta migomo kila kukicha.
Kama dhamira ya kweli ni kupata Tanzania ya viwanda itakayokwenda kwenye uchumi wa kati ni wazi sasa tubadili mfumo wetu wa elimu utakaosaidia vijana wetu kuwa wabunifu. Na endapo elimu ya tija itatolewa kwa vijana wetu ni wazi ya kuwa hakuna haja ya kujiuliza maendeleo yatatoka wapi ila ni wazi vijana watayaleta wenyewe kutokana na elimu walioipata.
Tukiangazia swala la kilimo ni wazi bila kilimo chenye tija hatuwezi kuwa na Tanzania bora tuitakayo. Kila wakati tunasikia asilimia zaidi ama themanini ya watanzania wote huishi vijijini na ndio ambao hulisha taifa letu na mataifa mengine ya Ulaya na Marakeni. Kama taifa hili linapaswa kwenda mbele kwa kilimo ni dhahiri sasa kilimo kirudishwe kwa wakulima wenyewe na tuache kilimo cha propanda.
Najaribu kutafakari ni kwa kiasi gani wataalamu wetu wa kilimo katika vyuo vikuu na Wizara ya Kilimo wanafahamu mahitaji ya wakulima walio Tandahimba, Misungwi, Tarime na kwingineko. Je, tafiti zinazofanywa na wataalamu wa kilimo zinafanya nini ama zinatumika kama sehemu ya kuongeza shahada na kutupa sifa kwenye maandiko ya kimataifa ila zinashindwa kumsaidia mkulima aliyeko chini kabisa.
Siku tukiamua kutumia wataalamu wa kilimo nchini ambao naamini wako wengi na wakutosha kuinua kilimo chetu nchi yetu itasonga mbele. Hebu tafakari tuna watu wenye shahada nyingi na za hali ya juu katika kilimo ila hawana hata heka moja ya shamba kuwaonyesha majirani zake katika vitendo maana ya taaluma ya kilimo. Tunabaki na makabati yaliyojaa maandiko mengi ya kitafiti katika kilimo yakipigwa vumbi ili hali watanzania wanabaki wakilima kama enzi za ujima kwa kurusha mbegu na kusubiri mvua inyeshe ziote kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
Tuangazie swala la mwisho kama tunataka kuona Tanzania ile tunayoitamani na hapa ntazungumzia swala zima la uongozi. Yamkini tatizo kubwa la Afrika na Tanzania kwa ujumla ni uongozi. Je, tuna viongozi wa namna gani? Je, viongozi hawa wanaamini katika nini? Je, viongozi hawa wanatenda katika mienendo gani? Unaweza kujibu kutokana na uzoefu wako.
Ni ukweli usiopingika ya kuwa Tanzania bado tunashida ya uongozi kama taasisi ili hali kila mtu anamini ya kuwa anaweza kuwa kiongozi. Ila kama tutabaki na viongozi wabinafsi na wasiojali maisha ya watanzania maskini ni dhahiri hata kwarehema za Maulana hatuwezi fika. Viongozi wetu wengi wamebaki wakiwaza nini watafanya wanufaike na sio nini watafanya ili kuweza kuwasaidia viongozi watakao kuja. Tumesahau uongozi ni taasisi ya kurithishana na sio swala binafisi.
Kwa kuhitimsha, tunahitaji viongozi wabunifu na wenye kufanya mambo kwa weledi na sio wale wakuamriwa na kutenda bila kufikiri. Tunahitaji viongozi majasiri wanaoweza kusema ukweli wakati wote bila kujali watu watasemaje. Na pia tunahitaji viongozi ambao watajua ya kuwa maamuzi ya kisomi ni bora kuliko maamuzi ya kisiasa ambayo yatawafurahisha wanasiasa kwa kuwa wanawapa ugali wa kila siku. Tukishindwa kutofautisha siasa na uongozi tumekwisha kama taifa na giza nene liko mbele yetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika sote ni ndugu tutende kama taifa