Ujenzi wa hosteli shule ya Nandembo kuwalinda wasichana dhidi ya ‘mafataki’

Jamii Africa

Umbali kutoka shule na mazingira wanayoishi wanafunzi una nafasi kubwa ya kuathiri maendeleo ya wanafunzi kielimu. ili kukabiliana na changamoto hiyo baadhi ya shule zimejenga hosteli karibu na shule ili kuwawezesha wanafunzi kufuatilia masomo na kuwaepusha na hadha ya kusafiri umbali mrefu.

Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu Sekonari (MMES) inatekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari ikiwemo ujenzi wa hosteli  za wanafunzi wa kike ambao hukumbana na ukatili wa kijinsia wakati wakirejea nyumbani.

Kutatua kero hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa kushirikiana na Serikali Kuu inatekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya shule za sekondari katika wilaya hiyo.

Katika mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 259 ambazo zimeelekezwa katika shule ya sekondari Nandembo iliyopo kata ya Nandembo ambayo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa, vyoo, maabara na hosteli za wanafunzi.

 Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Halmashauri ya Tunduru kinaeleza kuwa fedha hizo zitajenga vyumba vinne vya madarasa, hosteli mbili, matundu 10 ya vyoo na ukarabati wa maabara tatu za masomo ya sayansi. Na ujenzi huo tayari umekamilika kwa asilimia 90 na kukamilika kwake kutapunguza tatizo la ubovu wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Ujenzi wa hosteli  katika shule hiyo kwa kiasi kikubwa itapunguza changamoto za wanafunzi kutembea umbali mrefu, ikizingatiwa kuwa Kata ya Nandembo ina shule moja ya sekondari ambayo hutegemewa na shule za msingi 5 za Naluwale, Majala, Nangunguru, Tumaini na Nandembo.

Umbali wa shule hiyo ya sekondari huwa kikwazo kwa wanafunzi kufuatilia masomo kwa sababu hutumia muda mwingi kutembea na wafikapo shuleni wanakuwa wamechoka na kushindwa kufuatilia masomo inavyotakiwa.

Shue hiyo ina hosteli moja tu ya wasichana ambayo haikidhi mahitaji yote ya wanafunzi. Hali hiyo inaathiri ufaulu na wa wanafunzi wa shule hiyo hasa wasichana ambao wangewekewa mazingira rafiki wangefanya vizuri zaidi katika masomo yao.

Ujenzi wa hosteli mbili katika shule hiyo unaonekana kuwa mkombozi kwa wanafunzi ikizingatiwa kuwa shule hiyo inafanya vizuri katika mitihani ya kitaifa licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za uhaba wa miundombinu ya kujifunzia.  

Mathalani, katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2016/2017 shule hiyo ilishika nafasi ya 31 kati ya shule 82 zilipo katika mkoa wa Ruvuma. Pia ilikuwa ya 835 kitaifa katika ya shule 3280 zilizopo Tanzania. Wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 56 lakini waliofeli ni 7 pekee.

 

Mwalimu Mkuu Nandembo atoa neno

 Mwalimu Mkuu wa shule msingi Nandembo, Marry Ndunguru anasema ujenzi wa hosteli hizo upo katika hatua ya mwisho na zitaanza kutumika muda si mrefu. Anaeleza kuwa maboresho yaliyofanyika katika shule yake hasa ujenzi wa hosteli yatainua kiwango cha elimu katika shule hiyo kwa kuweka mazingira salama kwa wanafunzi kujisomea.

 “Hosteli hizi zitaongeza tija kwa wanafunzi kuishi katika mazingira ya shule, kupata muda mwingi wa kujisomea, kuishi mazingira salama hasa wanafunzi wasichana na kuthibiti nidhamu ya wanafunzi wetu”, amesema Mwalimu Marry Ndunguru.

Hata hivyo,  wamefanikiwa kupata milioni 259 za ujenzi wa matundu kumi ya vyoo na ukarabati wa maabara tatu za masomo ya sayansi ambao uko katika hatua nzuri ya ujenzi.

“Kukamilika kwa ujenzi wa maabara kutaongeza tija kwa wanafunzi wa masomo ya sayansi kwa sababu watakuwa wanafanya mazoezi kwa vitendo tofauti na ilivyokuwa hapo awali”.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *