Mmiliki wa basi atozwa faini kwa kusafirisha samaki wachanga Mwanza

Jamii Africa
WAFANYABIASHARA  wanne  wametozwa faini,  akiwemo mmiliki wa basi liitwalo  Bariadi Express, Maduhu Katalima, mkazi wa  wilaya ya Bariadi mkoani Shinyanga ambaye  ametozwa faini ya shilingi milioni 2 baada ya basi lake kukamatwa likijaribu kusafirisha tani 2.5 za  samaki  wachanga.

Taarifa hiyo  ilitolewa jana Jijini hapa na  Afisa wa Doria katika ofisi ya Uvuvi mkoani Mwanza, Juma  Makongoro  wakati  akizungumza na mwandishi wa habari  hizi kwa njia ya simu.

Alisema mmiliki wa basi hilo alitozwa  faini  kwa kosa la kushirikiana na wafanyabiashara na kusafirisha samaki wachanga.
” Hata hivyo, siyo kazi ya basi kusafirisha mizigo  ya samaki; hiyo ni kazi ya malori” alisema Makongoro.
Alisema  watuhumiwa wengine watatu ambao walikuwa wakijaribu kutorosha  samaki hao  walitozwa faini ya shilingi milioni moja moja kila mmoja.

Alifafanua kuwa samaki  waliokamatwa  walivuliwa huku wakiwa na  urefu wa chini ya inchi 50, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za uvuvi.

” Ni  kweli   kwamba Mei 10 mwaka huu majira ya saa 10 jioni tulikamata  basi lenye namba za usajili T275 BLE likiwa na tani 2.5 za samaki wachanga  aina ya sangara’ alisema Makongoro.

Alisema  basi hilo  lilikamatwa katika barabara kuu lami, Musoma – Mwanza na kwamba libambwa  wakati likiwa katika eneo la Igoma  Jijini Mwanza.

Kwa mujibu wa Makongoro, gali hilo  lilikuwa likitokea  Musoma  kuelekea Jijini Mwanza.

Makongoro aliwataja  wafanyabiashara  waliokuwa wakisafirisha  samaki hao kuwa ni Hamisi  Jackson(25) mkazi wa Nyakato  Jijini Mwanza, William Maige (40) mkazi wa Igoma pamoja na Mashiku Buzuka(42) mkazi wa Nyashimio wilayani Magu.

Afisa huyo alisema  licha ya kupakia samaki, basi  hilo lilikuwa limebeba  wasafiri zaidi ya 60.

Alisema  watu hao walikamatwa  kutokana na taarifa za siri zilizotolewa na wasamaria wema.

Mwezi  jana kikosi  hicho  kiliteketeza  makokoro, nyavu pamoja na zana mbalimbali za uvuvi haramu vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 5.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *