MPANGO wa Afya Bora kwa Wote (Universal Health Coverage) bado unasuasua Tanzania.
Mpango huu wa dunia wenye historia ndefu na ambao unapigiwa chepuo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa mpango thabiti katika kuhakikisha huduma bora ya afya kwa wakazi wa dunia.
Historia ya mpango huu unaanzia miaka ya 1800 nchini Ujerumani, pale ulipoanzishwa mpango wa bima ya lazima kwa wafanyakazi wa viwandani ambayo ilimlazimisha mwajiri kumlipia bima mwajiriwa kwa ajili ya majanga kama kuumwa, kuumia na ajali.
Historia ya Mpango wa Afya kwa Tanzania unaanza rasmi mwaka 1967 ambapo Azimio la Arusha lilitangazwa, chini ya Siasa ya Ujamaa, ambapo lengo kuu lilikuwa kueneza huduma za jamii ikiwamo afya hasa kwa makundi yasikuwa na uwezo na yaliyoachwa nyuma.
Mwaka 1977, huduma binafsi za afya zilipigwa marufuku na huduma zote za afya zilifanywa kuwa bure na serikali.
Kutokana na hali mbaya ya uchumi, mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tanzania ilianzisha utaratibu wa uchangiaji wa huduma za afya kwa awamu. Huduma bure ya afya ilikoma rasmi.
Katika kufikia malengo ya Mpango wa Afya Bora kwa Wote, Serikali ya Tanzania ilianzisha bima mbili za afya mnamo mwaka 2001, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Tiba kwa Kadi (TIKA/CHF). NHIF ilianzishwa mahususi kwa ajili ya wafanyakazi wa serikali ila baadaye wanachama binafsi waliruhusiwa.
TIKA ilianzishwa maalumu kwa ajili ya wananchi wa maeneo ya vijijini mpaka wilayani. Mpango huu ni wa hiyari.
Pamoja na juhudi hizi, mpaka mwaka 2013, ni asilimia 6.6 tu ya wananchi waliokuwa wanahudumiwa na NHIF na asilimia 7.3 tu ya wananchi walikuwa wanahudumiwa na CHF.
Kiwango hichi ni cha chini sana katika kufikia malengo ya Mpango wa Afya Bora Kwa wote ukilinganisha na nchi kama Rwanda ambayo imefanikiwa kupitia mpango wa Community Based Health Insurance (CBHI), ambapo asilimia 75 ya wananchi wa Rwanda wanahudumiwa na mpango huo wa bima.
Nini changamoto zinazoikabili Tanzania?
Kwanza kabisa ni ufinyu wa bajeti. Mpaka mwaka 2016, serikali imeendelea kutenga chini ya asilimia 10 ya bajeti kwa ajili ya afya wakati maazimio ya Abuja (2001), yaliainisha malengo ya angalau asilimia 15 ya bajeti kwa ajili ya afya.
Pili ni sera mbovu zisizokidhi mahitaji ya Watanzania wengi. Kulingana na shirika la afya duniani, ili kufikia malengo ya UHC, sera ya afya inatakiwa kuongozwa na malengo na sio uwezo wa bajeti. Malengo makuu matatu ni Uhitaji, Ubora na Ulinzi wa Uchumi.
Uhitaji maana yake jamii ipate huduma inazohitaji na sio zinazopangwa na wapanga sera. Mfano mzuri ni dawa nyingi zisizohitajika na kuacha dawa muhimu zenye mahitaji makubwa katika jamii.
Ubora maana yake huduma zinazosimamiwa na sera ya afya zinatakiwa ziwe zenye kiwango bora. Mfano mzuri ni pamoja na serikali kuweka mpango wa huduma bure kwa wajawazito, bado ni asilimia chache ya wajawazito wanaojifungua uhudumiwa na wafanyakazi wa afya wenye elimu stahiki.
Takwimu zinaonesha mpaka mwaka 2010 Tanzania, bado ni asilimia 50 tu ya wanawake wajawazito hujifungua chini ya uangalizi wa wahudumu wa afya wenye elimu stahiki.
Rwanda imefanikiwa kufikia asilimia 70 mwaka 2010 kutoka asilimia 35 mwaka 2000 kutokana na uanzishwaji wa mpango wa jumla na lazima wa bima ya afya wa CBHI.
Ulinzi wa kiuchumi maana yake ni gharama za huduma hizi hazitakiwi kuwa kubwa kiasi cha kuwaingiza wananchi katika umasikini zaidi.
Tanzania inaweza kuiga mfano wa nchi ya Chile ambayo imefanikiwa kufikia malengo ya afya bora kwa wote.
Mfumo wa afya wa Chile unazingatia kanuni zote tatu za sera bora. Wananchi wote wa Chile wapo chini ya mpango wa bima ya afya. Sera hiyo imehakikisha pesa inayotoka mfukoni mwa mwananchib haizidi asilimia 20 ya gharama za huduma, hii inamaanisha gharama za afya kwa mwananchi wa Chile hazizidi kipato chake cha mwezi kwa mwaka mzima.
Pia sera ya afya ya Chile imeweka muda maalumu wa kusubiria huduma ya afya pamoja na kuhakikisha huduma hiyo ni ya kiwango cha kutosha.
“Wagonjwa wengi wanaopokelewa hapa hawana bima, jambo ambalo linachangia ugumu wa uchangiaji wa huduma na kufanya tiba kusuasua maana gharama hasa za upasuaji ni kubwa sana” anasema Dk. John Kweyamba wa idara ya upasuaji, Hospitali ya Rufaa Bugando iliyoko Mwanza.
Kutokana na changamoto zinazoikabili sera ya huduma ya afya Tanzania, mnamo mwaka 2016, naibu waziri wa afya Dk. Hamis Kigwangalla kupitia maelekezo ya waziri, ameunda kikosi kazi kujaribu kuboresha mfuko wa afya ya jamii (CHF).
Kikazi hicho kinaendelea kufanya kazi na kuhakikisha kinaibua njia nzuri na yenye kugusa wananchi wengi, ili kwamba Tanzania iwe na watu wenye uhakika wa afya bora kwa kupata tiba sahihi na kwa wakati.