KWA miaka mingi karibu wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma zimekuwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji, hasa kipindi cha kiangazi mbali na kuwa mkoa huo umepitiwa na mito kadhaa ukiwemo Ruvuma na Luhuhu, ambao unamwaga maji yake Ziwa Nyasa.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, ukosefu huo wa maji umekuwa ukiwapa tabu na wakati mgumu wakazi wengi wa mkoa huo, wakiwemo wale waishio vijijini.
Maendeleo ya upatikanaji maji yamekuwa yakiboreshwa zaidi kwenye Halmashauri ya Manispaa Songea ambayo ina wakazi zaidi ya laki mbili, lakini wilaya zingine kama Namtumbo, Mbinga, Nyasa na Tunduru zimekuwa na maendeleo duni ya upatikanaji wa maji safi na salama.
FikraPevu inazo kumbukumbu kwamba, mnamo Septemba 2016 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk. Binilith Mahenge, alisema bado mkoa huo una hali mbaya ya upatikanaji wa maji kutokana na kuwepo kwa miundombinu duni isiyoweza kuhudumia ipasavyo mkoa huo na iliyo na changamoto nyingi.
Hata hivyo, mwezi mmoja baadaye ujenzi wa Bwawa la Maji la Luhira ulitarajiwa kukamilika ambalo lingeweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu na kuhudumia idadi kubwa ya wakazi wa Manispaa ya Songea, japokuwa maeneo mengine yangeendelea kukabiliwa na uhaba.
Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Luhira ulitarajiwa kugharimu Shs. 2.7 bilioni hadi kukamilika, ambapo ungeongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 17 iliyokuwepo hadi kufikia asimilia 68 ya watu 200,000 waishio ndani ya Manispaa ya Songea.
Jambo la kushangaza ni kwamba, wakati wananchi wa mkoa huo wanaendelea kuteseka na uhaba wa maji, katika hotuba ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2012/2013 waziri wa wakati huo alisema kuna maeneo 49 mkoani Ruvuma ambayo yamefanyiwa utafiti na kuonekana kuwa mazuri kwa ajili ya ujenzi wa visima ambavyo vingetumiwa na wananchi.
Hatua ya Dk. Mahenge kukiri tena mwaka 2016, ikiwa ni baada ya kipindi cha miaka takriban minne, kwamba bado mkoa una changamoto kubwa za upatakinaji wa maji inaonyesha hakukuwa na muendelezo unaoridhisha katika hayo maeneo ambayo yaligundulika kwamba yangeweza kujengwa visima.
Idadi ya visima ambavyo vilichimbwa, kwa mujibu hotuba ya waziri mwaka 2012/2013, vilikuwa sita tu kati ya maeneo ya maeneo 49 yanayofaa kwa ajili ya visima.
Visima vilivyochimbwa wakati huo ni Halmashauri ya Wilaya ya Songea (kimoja), Tunduru (vinne) na kingine kikachimbwa wilayani Mbinga, huku Wilaya ya Namtumbo ikiendelea kusubiri.
Jitihada kubwa za serikali katika usambazaji wa maji safi na salama zinaonekana kujikita zaidi katika Manispaa ya Songea ambako kwenye maeneo mengi maji yanapatikana kwa saa 24.
Lakini upatikanaji wa maji katika wilaya zingine umekuwa ukifanywa hasa kwa misaada ya taasisi zingine ikiwemo binafsi kama CDCF katika Wilaya ya Namtumbo na TASAF kwa Wilaya ya Tunduru.
Jumuiya ya Nchi zilizo Kusini mwa Afrika (SADC) iliwahi kutoa msaada wa Dola 800,000 za Kimarekani ili kushughulikia suala la maji katika Bonde la Mto Ruvuma kwa ajili ya wilaya tano za mikoa ya Ruvuma na Mtwara, lakini mradi huo unaonekana haukuwa na matokeo makubwa.
Tangu kutengwa kwa fedha hizo miaka minne iliyopita, bado wilaya hizo zimeendelea kukabiliwa na uhaba wa maji safi na salama.
Nyakati za kiangazi uwezo wa kuzalisha maji katika Manispaa ya Songea hupungua na kufikia meta za ujazo 2,300 kutoka meta za ujazo 17,000, hivyo kuongeza tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa jamii.
Hata hivyo, hali huwa mbaya zaidi katika wilaya zingine hasa vijijini na kuwalazimu wakazi wa huko kufuata maji umbali mrefu.
Sera ya Maji inasisitiza kwamba, wananchi hawapaswi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu kwa jamii.
Moja ya vitu ambavyo huwavutia watu kuchagua makazi ya kuishi ni maji lakini kama hakuna, wengi huyakimbia makazi yao.
Hivi karibuni shule moja katika Wilaya ya Nyasa imeripotiwa kuwa na mwalimu mmoja, lakini kimtazamo, ukosefu wa huduma muhimu kama maji na nyinginezo unaweza kuwafanya watumishi wengi, wakiwemo walimu kutokuwa na hamasa ya kuishi huko na kusababisha kushuka kwa elimu maeneo hayo.