Kilimo cha Uyoga chaongeza uchumi kwa wanawake Dar

Jamii Africa

Sophia Chove, Mwenyekiti wa kikundi cha akinamama cha Tunza cha Mtaa wa Kilungule – Bunju, jijini Dar es Salaam, anaonekana akichanganya pumba za mchele, maranda, sukari pamoja na maganda ya alizeti.

Haya ni maandalizi ya kutengeneza udongo maalum kwa ajili ya kuoteshea uyoga.

Akinamama wengine wa kikundi hiki wanaandaa mifuko maalum ili kujaza mchanganyiko huo wa vimeng’enya.

“Tumekwishavuna mara nyingi tu, sasa tunaandaa tena tuendelee kulima, maana wateja ni wengi na kipato kimeongezeka,” anaeleza Bi. Chove akiwa amezungukwa na akinamama wengine.

Anaongeza: “Ili tupate faida kubwa tunafikiria kuongeza shamba jingine, maana hili tulilonalo halitoshi, changamoto yetu kubwa ni mtaji, lakini tukiwezeshwa tunaweza.”

Anasema, miezi sita tangu walipoanza mradi huo wa kilimo chau yoga tayari wamepata wateja wa maduka makubwa ya bidhaa (super markets) pamoja na jamii inayowazunguka, mahitaji ambayo ni makubwa kuliko uwezo wa kuzalisha.

“Uyoga una faida kubwa, fikiria robo kilo ya uyoga inauzwa Shs. 2,500 wakati kilo moja ni Shs. 10,000,” anaongeza Sophia.

Sophia anasema kwamba, kilimo hicho kimewaondoa akinamama kwenye mikeka na kuanza kujishughulisha ili kuongeza kipato cha familia badala ya kuwasubiri akinababa wahemee peke yao.

“Maisha ya sasa kila mmoja inabidi ahangaike, baba anapitia huku na mama anakwenda kule, halafu hata wanawake wanaweza kuongeza pato la familia kuliko jamii inavyofikiria,” anasema.

Kikundi cha Tunza chenye wanachama 10, kiliundwa kabla ya ujio wa mradi wa kilimo chau yoga ambapo akinamama hao walikuwa wakishirikiana katika michezo ya kupeana kabla ya kuanzisha Vicoba, lakini baada ya kuanzisha mradi huo, wanawake wengi wa mtaani wamevutiwa na kutaka kujiunga nacho.

“Tulichokifanya ni kutumia kikundi chetu kama kituo cha mafunzo kwa kuwafundisha wanawake wengine ili nao wakaunde vikundi ama wakaanzishe mradi wa kilimo hiki mmoja mmoja kwa sababu inawezekana,” anasema Sophia ambaye pamoja na wenzake walipatiwa mafunzo ya kutosha na mshiriki kiongozi wa mradi huo, Magdalena Bukuku pamoja na Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni, Esther Chiombola.

Pamoja na umuhimu wa zao hilo kwa afya, lakini kilimo cha uyoga ni kilimo hifadhi ambacho kinapambana na uharibifu wa mazingira, hivyo kuwafanya wanawake hao kuwa sehemu ya jamii inayopambana na mabadiliko ya tabianchi.

Miradi hiyo ya Green Voices nchini inalenga pia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 pamoja na Malengo Endelevu ya Dunia katika kuondoa umaskini, kuongeza ajira, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kilimo hiki hakihitaji ardhi kubwa wala hakitumii maji mengi, ni rafiki wa mazingira na katika kipindi hiki ambacho ulimwengu unalia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, hiki ndicho kinachofaa,” anaongeza Sophia, ambaye kabla ya hapo alikuwa akijihusisha na kilimo cha viazi vitamu na mboga mboga kwenye eneo la nyumba yake.

Ni katika eneo hilo ambako alikubali ombi la wanakikundi wenzake wajenge banda la kuzalishia uyoga lenye uwezo wa kuhifadhi mifuko zaidi ya 1,000 kwa wakati mmoja, ingawa anasema, wana mpango wa kujenga banda jingine.

“Sehemu ipo ya kutosha, na kwa vile mahitaji yanaonekana kuwa makubwa, tunatarajia kujenga banda jingine kuba zaidi ya hili ili tupanue kilimo chetu,” anasema na kuongeza kuwa kilimo hicho kimefanikiwa kupitia mradi wa Green Voices ambao ndio uliowafadhili kwa kuwapatia mafunzo, vifaa na ujuzi.

Bi. Magdalena ndiye aliyeupeleka mradi wau yoga Bunju baada ya kupatiwa mafunzo ya karibu mwezi mmoja nchini Hispania mapema mwaka 2016 akiwa na wanawake wengine 14, kwa ufadhili wa taasisi inayojihusisha na maendeleo ya wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de la Vega.

Akinamama wengine wanaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Pwani na Mwanza.

“Sikutegemea kama ningepata mwitikio kama hivi wakati nilipoanzisha wazo hili baada ya kuwakusanya, lakini sasa vipo vikundi viwili – hiki cha Bunju na kingine Kiko Boko – ambavyo vina wanachama 10 kila kimoja, ingawa kila siku wanakuja wanawake wengi wakitaka kujiunga navyo,” anabainisha Magdalena.

Hata hivyo, amesema kuwagawa tu hakukuwazuia wanawake wengine kwenda kujifunza, kwani tayari wanajamii katika maeneo hayo wamekuwa wakimiminika kujifunza namna ya kuanzisha mashamba ya uyoga majumbani mwao.

“Mpaka sasa nimekwishawafundisha wanawake wengine zaidi ya 50, wengine wanatoka Zanzibar, Kibaha na Bagamoyo,” alisema.

Anaongeza: “Ni mradi unaotumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu, hapa Bunju tayari akinamama wameanza kuvuna.”

Anasema, uyoga ni zao linalohitaji eneo dogo na matumizi kidogo lakini endelevu ya rasilimali maji, hivyo kuwa rafiki mkubwa wa mazingira licha ya umuhimu wake kwa afya ya binadamu.

Uyoga ni aina ya kuvu (fungi) na hauna uwezo wa kujitengenezea chakula kama ilivyo mimea mingine ya rangi ya kijani, hivyo ili kuota na kustawi, inahitaji chakula ambacho kimekwishatengenezwa kutoka katika mimea iliyooza, hali ambayo inasaidia kusafisha mazingira.

Mhazini wa kikundi hicho ambaye pia ndiye mwalimu wa ukulima wa uyoga na Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni, Esther Chiombola, anasema kila wiki wamekuwa wakiwafundisha akinamama kati ya watano hadi 10 kutoka maeneo mbalimbali.

“Hapa pamekuwa kama kituo cha mafunzo, wanawake wengi wamehamasika na tunawafundisha namna ya kuanzisha kilimo hiki ambacho ni rafiki wa mazingira na kina tija kubwa kwa uchumi,” anasema Mama Chiombola.

Anaongeza: “Ni mradi unaotumia gharama kidogo huku mavuno yake yakiwa endelevu, hapa Bunju tayari akinamama wameanza kunufaika.”

Mradi wa Green Voices ni wa pekee nchini Tanzania kufadhiliwa na taasisi ya Foundation for Women of Africa, ambao lengo lake kubwa ni kuwasaidia akinamama kupaza sauti katika masuala ya mazingira kwa kutumia njia ya ujasiriamali.

“Mama Teresa, baada ya kutoka madarakani, alianzisha taasisi hiyo kwa nia ya kuwakomboa wanawake wa Afrika, ambao ndio waathirika wakubwa wa athari za uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabianchi,” anaeleza Secelela Balisidya, Mratibu na msimamizi wa mradi huo nchini.

Secelela, ambaye kitaaluma ni mwandishi aliyejikita zaidi katika habari za mazingira, anasema ujio wa Green Voices utawakomboa wanawake wengi wa Tanzania kupitia miradi waliyoibuni ambayo itasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kama inayoelekezwa katika Malengo Endelevu ya Dunia.

Anasema, mwanamke ndiye muathirika mkubwa wa mazingira kwani anatumia muda mwingi kutafuta maji na nishati, hasa kuni, kwa ajili ya matumizi ya familia, kuliko kufanya shughuli zingine za maendeleo.

“Mradi kama huu wa kilimo cha uyoga ni rafiki wa mazingira tena ni kilimo hifadhi kwa sababu hauhitaji maji mengi, lakini una faida kubwa kiafya hasa kutokana na ukweli kwamba, hivi sasa watu wengi wameathirika kwa kula vyakula vinavyozalishwa kwa kemikali,” anaongeza.

Serikali katika bajeti zake imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuendeleza matumizi ya teknolojia ya Kilimo Hifadhi ingawa teknolojia hiyo bado haijawafikia watu wengi.

Namna ya kulima uyoga na faida zake

Bi. Chiombola ‘Mama Uyoga’ anasema uyoga ni lishe bora ambayo imejaa kiasi cha asilimia 20 hadi 49 cha protini pamoja na Vitamini B, C, D, E, na K, na madini joto, chuma, fosforas, potashi, zinki na shaba na kwamba hauna lehemu (cholesterol).

Anasema, baadhi ya aina za uyoga kama Ganoderma husaidia kuzuia na kupunguza kasi ya magonjwa sugu kama saratani, kisukari, kifua kikuu, moyo, shinikizo la damu na figo.

“Lakini kilimo cha uyoga ni ajira kubwa kwa akinamama, vijana, wazee na wastaafu na ni kilimo rafiki kinachopunguza uchafuzi wa mazingira kwa vile kinatumia mabaki ya shambani na viwandani,” anafafanua.

Anataja faida nyingine kama kilimo endelevu cha mwaka mzima na kwamba mabaki yake baada ya mavuno kukoma ni mbolea nzuri na chakula cha mifugo.

“Kilimo cha uyoga kinasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na kula vyakula vyenye sumu kwani mbegu zinazotumika zimefanyiwa utafiti na zinapatikana kutoka taasisi maalumu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kituo cha Utafiti wa Kilimo-Uyole, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Bustani Tengeru na Shirika la TIRDO,” anasema.

Bi. Chiombola anasema, aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C na kiasi cha unyevunyevu cha asilimia 75.

Hata hivyo, anasema kutokana na hali ya joto la Dar es Salaam, aina inayolimwa zaidi ni Chaza (Oyster mushroom) ambayo inastahimili hali ya joto kwa nyuzi joto 12 – 30 ambapo kundi hilo linahusisha aina ya Pleurotus sapidus(mweupe na mwingine rangi ya udongo) pamoja na Pleurotus sajor – caju.

Mahitaji muhimu ya kilimo cha uyoga yanatajwa kwamba ni banda la kuanzia ukubwa wa meta 4 kwa 5 ambalo linatosha kuotesha mifuko 450 hadi 500, vimeng’enywa ambavyo ni masalia makavu kama mabua ya mahindi, majani makavu ya mgomba na ya viwandani kama maganda ya alizeti.

Pia inahitajika mifuko maalum inayostahimili joto ambayo hutumika kujazia vimeng’enya, vifaa vya kazi kama mapipa ya kuchemshia maji, turubai la plastiki, vipete, pampu ya kumwagilia, mbegu za uyoga, vifungashio vya plastiki, visahani, virutubisho hasa pumba laini, sukari au molasses, chokaa na dawa kwa ajili ya usafi, hasa Dettol na spiriti.

Uoteshaji na upandaji

Kabla ya kuanza uzalishaji ni lazima kiwepo chumba chenye paa linalozuia jua, mvua, na vumbi ambacho pia kinapaswa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga.

“Baada ya hapo kuandaa masalia na mambo mengine kama utakavyoelekezwa na mtaalamu, jaza vimeng’enyo hivyo kwenye mfuko wa sandarusi wenye upana wa sm 40 – 45 na kimo cha sm 75. Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko,” anasema Bi. Chiombola.

Anasema baada ya hapo unatakiwa kufunga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha sm 1 kwa kila umbali wa sm 6 hadi 10 kwa kila mfuko ili yaweze ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko.

“Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza au funika kwa kaniki. Acha mifuko humo kwa muda wa wiki tatu hadi nne bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.

“Utando mweupe ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea fungua mifuko, visha viringi, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Mifuko inaweza kuwekwa kwenye, meza, chanja la waya au miti.  Anza kumwagilia kwa pampu (mvuke wa maji baridi) na baada ya wiki moja na nusu uyoga utaanza kuchomoza,” anaeleza Bi. Chiombola.

Uvunaji

Bi. Chiombola anasema kwamba, uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung'oke.

“Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe kabla haujaharibika,” anaeleza.

Inaelezwa kwamba, uyoga ukishavunwa unaweza kuhafadhiwa kwenye jokofu kwa muda wa siku 7 kabla ya kuharibika, lakini haipaswi kuhifadhi kwenye friza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *