WALIMU wengi wa shule za msingi Dar es Salaam, wanahemewa kwa wingi wa vipindi wanavyofundisha madarasani.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu kwa zaidi ya wiki mbili umebaini kuwa katika shule nyingi za Jiji la Dar es Salaam, mwalimu mmoja anaweza kufundisha vipindi hadi sita kwa siku moja.
Imebainika pia kuwa walimu wengi hufundisha hata masomo ambayo hawayamudu vyema; hasa Hisabati, Kiingereza, Sayansi.
“Ipo siku moja kwa wiki, Ijumaa, nafundidha hata vipindi sita, kwani nina vipindi darasa la nne, tano, sita na saba na huko darasani lazima nifike na kufundisha,” ameiambia FikraPevu, mwalimu ambaye ameomba kuhfadhiwa kwa jina lake.
Hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za msingi. Tatizo hili lipo nchi nzima.
Mwalimu huyo amesema analazimika kufundidha vipindi vingi kwa kuwa shule yao ya Mwongozo, iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam, haina walimu wengi wa masomo anayofundisha; hisabati, Kiingereza na Sayansi.
Profesa Ignas Lyaruu, ameiambia FikraPevu kuwa kuruhusu mwalimu mmoja kufundisha masomo na vipindi vingi kwa siku, ni chanzo cha kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini.
“Hivi inawezekana namna gani mwalimu kufundisha vipindi zaidi ya sita kwa siku, huyu ana uwezo gani, hali hii ndiyo inafanya wanafunzi kushindwa mitihani. Haiwezekanai mwalimu akaandaa masomo yote hayo kwa umakini, atakuwa anafanya tu, bora liende na apate mshahara,” anasema profesa huyo ambaye aliwahi kufundisha vyuo vikuu ndani na nje ya Tanzania.
Msemaji wa Wizara ya Elimu, Mwasu Swale alipoulizwa kuwepo kwa hali hiyo katika Jiji la Dar es Salaa, alisema ni kweli maeneo mengi ya Tanzania yana upungufu wa walimu, ikiwamo Dar es Salaam, lakini sio kwa kiwango cha mwalimu mmoja kufundisha vipindi sita kwa siku.
“Vipindi sita kwa siku haiwezekani, ni muda mrefu sana huo na mwalimu mkuu hawezi kuruhusu kuwepo kwa hali hiyo,” anasisitiza Mwasu.
Sera ya Elimu inaonesha kuwa kipindi kimoja cha mwalimu kufundiha darasani ni dakika 45, ingawa mwalimu anaweza kuomba kuongeza muda.
Wakati hili likiripotiwa, FikraPevu imewahi kuchapisha habari juu ya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 195 katika Shule ya Msingi Matarawe katika Kijiji cha Marungu, Tarafa ya Mpepo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Hali hii ndiyo inaonekana kutawala shule nyingi za msingi nchini, hasa maeneo ya pembezoni.
Hata hivyo, baada ya wiki tatu tangu habari hiyo kusambaa, uongozi wa Ruvuma ulipeleka mwalimu mwingine katika shule hiyo. Sasa ina walimu wawili.
Walimu wa Tanzania, hasa katika shule za msingi, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapunguza ufanisi wa kufundisha. Hali hii inatokana na ukweli kuwa serikali haijawekeza rasilimali za kutosha kwa walimu.
Maeneo ya vijijini tatizo ni kubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo ya mijini. Uhaba wa walimu na maslahi duni, vimechangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa ubora wa elimu ya Tanzania.
Takwimu za Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaonesha hadi Desemba 2016, bado kulikuwa na uhaba wa walimu 47,151 wa shule za msingi.
FikraPevu ina takwimu zinazoonesha kuwa idadi hiyo inayozidi kidogo jumla ya walimu walioajiriwa katika shule za msingi za umma na binafsi kwa miaka 10 iliyopita ambao ni 45,528.
Kama ilivyo kwa Tanzania, tatizo la uhaba wa walimu linajitokeza katika nchi nyingine za Afrika, ambapo jitihada za kutatua tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi zinahitajika ili kuinusuru elimu ya watoto wa Afrika.
Ripoti ya Taasisi ya Takwimu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni Duniani (UNESCO) ya mwaka 2016 inaeleza kuwa uhaba mkubwa wa walimu uko zaidi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo walimu wanoahitajika ni milioni 17 ili kufikia lengo la kuwa na elimu bora katika shule za msingi na sekondari mwaka 2030.
Walimu milioni 6.3 wa shule za msingi wanahitajika; walimu milioni 2.4 wanatarajiwa kuajiriwa na walimu milioni 3.9 kujaza nafasi za walimu wanaotarajia kuacha taaluma ya ualimu; ama kwa kupata kazi zingine au kwa kustaafu.
Licha ya uhitaji wa walimu kuwa mkubwa, bado walimu waliopo wanalemewa na majukumu ya kufundisha na kuwahudumia wanafunzi. Ipo dhana kuwa maeneo ya mijini yana walimu wengi ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Dhana hiyo inaweza kuwa na ukweli ikizingatiwa kuwa shule nyingi za msingi za mjini zina uwiano mzuri wa walimu na wanafunzi. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2007 inabainisha uwiano sahihi wa mwalimu kwa wanafunzi katika shule za msingi kuwa ni mwalimu mmoja kwa watoto 40 (1:40).
Shule nyingi za mijini zina uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi, zipo baadhi ya shule ambazo hazijakidhi maelekezo ya sera kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.
FikraPevu ilitembelea Shule ya Msingi Makumbusho iliyopo Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, ambayo ina walimu 28 na wanafunzi 1133, kwa muktadha huo, uwiano wa mwalimu na mwanafunzi ni 1:40 ambao ni kiwango sawa na maelekezo ya sera.
“Darasa la kwanza lina mikondo mitatu ambapo kwa wastani kila chumba kina wanafunzi 36 kwa mwaka huu ikilinganishwa na wanafunzi 56 mwaka 2016,” anasema mwalimu mmoja wa Shule ya Makumbusho ambaye anaomba jina lihifadhiwe na kuongeza kwamba kipindi cha nyuma hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi iliyokuwepo.
Licha ya uwiano mzuri katika shule za mijini, bado iko changamoto kubwa kwa walimu waliopo kulemewa na vipindi vya masomo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba, wanasoma masomo kumi kwa mwaka mzima, ambapo huwalazimu walimu kufundisha vipindi vyingi kila siku vya masomo tofauti tofauti.
“Hapa tunao walimu 28 na walimu watatu tu ndio wanaofundisha darasa la kwanza, lakini kusema kweli tunatakiwa tupatiwe walimu watano zaidi kwa darasa la kwanza kutokana na wingi wa vipindi,” anaeleza mwalimu huyo Makumbusho na kuongeza kwamba, kwa wastani mwalimu mmoja anafundisha vipindi vitano vya masomo tofauti kwa siku.
Uhitaji wa walimu lazima uendane na idadi ya masomo ambayo mwanafunzi anasoma ili kumpunguzia mwalimu mzigo wa vipindi anavyofundisha kila siku, ambapo katika shule nyingine mwalimu hufundisha wastani wa vipindi 5 mpaka 7 kwa siku.
Wingi wa vipindi hupunguza ufanisi wa mwalimu katika kufundisha matokeo yake wanafunzi wanakosa uangalizi wa karibu kutoka kwa mwalimu kwa sababu muda mwingi anatumia kuaandaa masomo na kupitia kazi za wanafunzi.
Mwalimu mwingine katika Shule ya Msingi Mapambano (jina tunalihifadhi) iliyopo Wilaya ya Kinondoni, amezungumza na FikraPevu na kulalamikia wingi wa vipindi anavyofundisha kila siku na kusema “darasa la sita lina walimu wawili ambao wanafundisha masomo 10 na vipindi ni vingi kwa siku, inatulazimu kufundisha masomo ambayo hatujayasomea, wanasema hakuna upungufu wa walimu lakini tatizo ni vipindi vingi tunavyofundisha kila siku”
Kwa miaka mingi sasa serikali imekuwa ikilalamika kuwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi katika shule za umma na hali hii huwalazimisha walimu wasio na taaluma ya sayansi kufundisha masomo ambayo hawana uzoefu nayo.
Lakini upungufu wa walimu katika shule, unawalazimu kufundisha masomo ambayo hawana uzoefu nayo. Katika hili ufanisi wa mwalimu unakuwa mdogo na wanafunzi hawawezi kupata maarifa yaliyokusudiwa.
Ripoti ya utafiti ya ‘Ufanisi katika Ufundishaji’ ya Shirika la HakiElimu (2014) inaeleza kuwa katika shule nyingi za umma, walimu hufundisha masomo ambayo hawajasomea kutokana na upungufu wa walimu.
“Kwa hakika Shule ya Msingi Hurui iliyopo katika Wilaya ya Tanga Vijijini haikuwa na mwalimu wa somo la Bailojia, lakini mwalimu wa somo la Kiingereza alijitolea kufundisha somo hili. Vilevile, kulikuwa hakuna mwalimu wa Hisabati lakini kulikuwa na mhitimu wa Kidato cha Sita aliyekuwa akifundisha somo hili kwa kujitolea”, inaeleza ripoti hiyo.
Ikiwa imebaki miaka tisa kutekeleza Mpango wa Taifa wa Maendeleo (2025) ambao unalenga kufainya jamii ya kitanzania kuwa ya watu walioelimika ambapo nchi itajikita katika ubunifu na ugunduzi.
Kwa changamoto hizi za walimu, je, Tanzania itaweza kuwa na elimu bora na kushindana na mataifa mengine katika nyanja za sayansi na teknolojia ifikapo 2025?