Ukosefu wa vitamini D kwa wajawazito sababu kubwa watoto kupata Usonji

Jamii Africa

Duniani kote , Aprili 2 ya kila mwaka ni siku iliyotengwa kueneza ufahamu, kujenga uelewa na kukubali juu ya hali ya usonji, ambayo kitaalamu inajulikana kama “Autism”.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘ Watoto wenye Usonji tuwapende na tuwalinde’. Kauli mbiu ya mwaka huu ilipendekezwa na Umoja wa Mataifa ili kuwatazama wanawake, wasichana na watoto ambao mara nyingi wanasahaulika katika maswala muhimu ya kijamii.

Usonji ni hali ambayo mtu huwa nayo tangu utotoni ambayo hutambulika kwa mhusika kushindwa kuwasiliana vizuri (communicate) na pia kushindwa kujihusisha na watu wengine katika mambo mbalimbali ya kijamii (socialize) katika hali ya kawaida.

Ishara za usonji zinaweza kuonekana mapema, hata katika umri mdogo wa mtoto wa miezi 6 hadi18, ingawa mara nyingi inaweza kutambulika hadi kwa watoto wenye umri wa miaka 2 hadi 5.

Uchunguzi wa uwepo wa usonji hufanywa na madaktari watalaamu wa tatizo hili pamoja na wanasaikolojia kwa kutumia vipimo tofauti tofauti, ikiwa ni pamoja na kuwauliza maswali walezi wa mtoto, kuangalia na kusoma tabia za mtoto. Ni muhimu kugundulika mapema ili huduma za kumsaidia mtoto zianze mapema.

Utafiti uliofanywa na Prof. Karim Manji ulionyesha kuwa nchini Tanzania kuna shule 8 za serikali na vituo 8 binafsi vinavyotoa huduma kwa watoto wenye Usonji. Pia kuna ufinyu wa taarifa kuhusu ukubwa wa tatizo hili Tanzania.

Wanasayansi wamekuwa wakitafiti kwa muda mrefu chanzo cha usonji. Kwa sasa, dunia inajua kwamba hakuna chanzo kimoja cha usonji. Tafiti zinaonesha mchanganyiko wa sababu za kijenetiki na zisizo za kijenetiki, au mazingira zinazopelekea mtoto kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata hali ya usonji.

                Ishara za usonji zinaweza kuonekana mapema, hata katika umri mdogo wa mtoto

Sababu za kijenetiki
Tafiti zinaonesha tatizo la usonji linaweza kuanzia kwenye familia. Mabadiliko ya kijenetiki yanapelekea mtoto kuwa na uwezekano mkubwa kupata hali ya usonji. Kama mzazi ana mabadiliko hayo, anaweza kumpitisha mtoto (hata kama mzazi hana usonji).

Wakati mwingine, mabadiliko hayo ya kijenetiki yanaweza kutokea ghafla wakati yai na mbegu zikikutana. Lakini, mabadiliko mengi yanayotokea hayapelekei mtoto kuwa na usonji, bali yanaongeza uwezekano wa kuwa na hali hiyo.

Sababu za Mazingira
Tafiti zinaonesha sababu za kimazingira zinazoweza kuongeza ama kupunguza uwezekano wa mtoto, ambaye tayari ana mabadiliko ya kijenetiki kuwa na hali ya usonji. Tafiti pia zinaonesha kwamba ukubwa wa uchangiaji wa sababu za mazingira ni mdogo.

Hali za kimazingira zinazoongeza uwezekano wa mtoto kupata usonji ni kama: Umri mkubwa wa wazazi (mama mwenye umri zaidi ya miaka 35, na baba zaidi ya miaka 40).

Sababu zingine ni matatizo ya ujauzito au wakati wa kuzaa (mfano: uzito mdogo, mimba pacha na kuzaa watoto njiti, wanaozaliwa kabla ya wiki ya 26 ya ujauzito), na mimba zinazofuatana kwa karibu sana, chini ya mwaka mmoja.

Aidha, inashauriwa kuwa wanawake wakati wa ujauzito watumia vitamini yenye ‘folic acid’ ambayo inaweza kupatikana kwenye matunda na mbogamboga ili kupunguza uwezekano wa mtoto aliye tumboni kupata usonji.

Utafiti uliofanywa kwa miaka mingi na Dr John Cannell umeonesha uhusiano wa moja kwa moja wa upungufu/ukosefu wa Vitamin D wakati wa ujauzito wa mtoto mwenye usonji. Utafiti bado unaendelea kuhusiana na hii sababu ya Vitamin D ili kutathmini kwa uhakika kwamba usonji unahusishwa na upungufu wa Vitamini D kwa mama wakati wa ujauzito.

Kupata mimba zinazofuatana kwa karibu sana, chini ya mwaka mmoja, nayo ni sababu ya mtoto kupata usonji

 

Matibabu ya Usonji
Mafunzo katika shule maalumu, tiba ya kuongea (speech therapy), tiba ya tabia (behavior therapy) , tiba ya mazoezi (physiotherapy) na tiba ya kuimarisha stadi(occupational therapy). Pia wanaweza matibabu ya dawa kulingana na maelekezo ya daktari.

Benki ya I&M imeendelea kushirikiana na Shule za Al Muntazir katika matembezi ya hisani yanayolenga kuongeza ufahamu wa jamii kuhusiana na tatizo la Usonji (Autism) na kukusanya fedha zitakazoweza kuwasaidia wale ambao wamekumbwa na tatizo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa shule za Almuntazir, Mohammad Ladack amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuelimisha jamii kuhusu watoto wenye Usonji (autism) na kuondoa dhana ya kuwaona watoto hao kama hawawezi badala yake wapewe nafasi katika shughuli za kijamii.

“Wazazi tunapaswa kuwapa nafasi watoto hawa na kuona kuwa wanaweza kufanya na wana haki ya kupata elimu hivyo wazazi wawape nafasi ya elimu kwani wanaweza kufanya mambo mbalimbali hivyo tuwalinde na tuwapende pia” Amesema Mkurugenzi Ladack.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *