Kampuni nyingine ya maji yahitajika Dar kukabiliana na ongezeko la mahitaji?

Jamii Africa

KAMPUNI nyingine ya huduma ya maji inahitajika ili kukabiliana na ongezeko kubwa la mahitaji kutokana na kile kinachoonekana kuzidiwa kwa Kampuni ya Huduma za Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO), FikraPevu inaripoti.

Taarifa ya Mkoa ya Dar es Salaam inaonyesha kuna kasi kubwa ya ongezeko la watu kulinganisha na mikoa mingine.

FikraPevu inafahamu kwamba, idadi ya watu jijini Dar es Salaam inaongezeka kwa asilimia 6 kwa mwaka huku DAWASCO ikiwa na wakati mgumu kuhudumia kikamilifu idadi ya watu wasiofika hata robo ambao wameunganishwa na mtandao wa maji wa kampuni hiyo ya umma.

Licha ya jitihada kadhaa zinazofanyika, lakini Mamlaka ya Maji ya mkoani humo (DAWASA) imeendelea kuwa na uwekezaji usioendana na kasi kubwa ya ongezeko hilo la watu, ambapo wengi wao wanalazimika kutumia maji ya siyo salama.

Maeneo mengi ya Dar es Salaam wakazi wake bado hawajafikiwa na mtandao ambao unasambaza maji na hivyo wakazi wengi hutumia maji ya visima kama njia mbadala.

Maeneo kama ya Chanika ambayo miaka 10 iliyopita kwa kiasi kikubwa yalikuwa ni pori, lakini kwa sasa idadi kubwa ya watu inazidi kuongezeka, na bomba linalosambaza maji halikupita maeneo ya huko, hivyo kwa kiasi kikubwa wakazi wa maeneo hayo hawajawahi kabisa kutumia maji ya DWASCO.

Manispaa ya Temeke ndiyo ambayo ina wateja wachache sana kati ya wateja wote wa DAWASCO kwani ina idadi ya wateja kiasi cha asilimia 10 tu kulinganisha na manispaa nyingine.

Hii inatokana na eneo hilo kuwa mbali na mabomba ya kusambazia maji hasa yanayotoka Ruvu Juu ambayo yanasimamiwa na DAWASCO, hali inayolifanya eneo kubwa kutotumia maji safi.

Ni maeneo machache tu katika manispaa hiyo ambayo yanatumia maji ya bomba, lakini sehemu kubwa wananchi wake wanatumia maji ya visima vifupi na virefu pamoja na visima vidogo kwenye mabonde ya mito midogo ambayo mara nyingi siyo salama kwani huwa yamechanganyika na uchafu ambao unaweza kuleta hatari ya magonjwa ya milipuko, kama kipindupindu na homa za matumbo.

FikraPevu inafahamu kwamba, Manispaa ya Temeke hasa maeneo ya Mbagala ina wakazi wengi na idadi ya watu inaongezeka kila siku kuliko maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam.

Uchunguzi wa FikraPevu umeonyesha kwamba, asilimia 70 maji ambayo wanatumia wakazi wa jijini Dar es Salaam yanatokana na visima kutokana na wakazi wengi kutounganishiwa na mifumo ya maji.

Kwa bahati mbaya zaidi ya asilimia 60 ya visima vilivyojengwa jijini humo maji yake si salama na mamlaka ya maji imeshindwa kabisa kutanua wigo wa kuwaunganishia maji wakazi wengi wa jiji hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa wa Dar es Salaam, kuna mahitaji kwa wastani wa zaidi lita milioni 400 kwa siku huku asilimia 40 ya maeneo ya jijini hayakupitiwa na mtandao wa maji achilia mbali idadi ndogo sana ya wateja wanaotumia maji yanayosambazwa na DAWASCO.

Ongezeko la asilimia 6 la watu kwa mwaka linafanya ongezeko la mahitaji ya maji kuwa lita milioni 27.

DAWASCO inakiri kwamba, moja ya changamoto ni uwekezaji mdogo na mahitaji ya maji yanazidi uwezo wa mitambo iliyopo.

Uhitaji wa maji unaoongezeka kwa kiwango hiki unaipa wakati mgumu DAWASCO kutoa maji kwa kiwango kinachostahili.

Aidha, idadi ya wataalam wanaohitajika bado imeendelea kuwa chini kulinganisha na kiwango halisi kinachohitajika ambacho ni zaidi ya wataalam 8,000.

Taarifa kutoka ndani ya mamlaka hiyo zinadokeza kwamba, kuajiri wafanyakazi ni kuongeza gharama za uendeshaji huku changamoto nyingine ya ulipaji wa Ankara za malipo kwa wateja bado ni kubwa kwani baadhi ya wateja ni wagumu kufanya malipo.

Baadhi ya miradi kama ule wa Kidunda mkoani Morogoro ambao ulitarajiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji maji jijini Dar es Salaam umekuwa ukisuasua tangu mwaka 2012.

FikraPevu inatambua kwamba, kuna miradi mingine inayotarajiwa kuanzishwa kwa msaada Serikali ya Korea Kusini, lakini mradi huo wa Kidunda haujulikani lini utakamilika.

Changamoto nyingine ni suala la majitaka ambapo uondoaji wake umekuwa ni mdogo.

Taarifa zinasema, ni asilimia 10 tu ya miundombinu iliyopo inaweza kuhudumia jiji la Dar es Salaam, hali ambayo inachangiwa pia na ujenzi holela wa makazi jijini humo kwani maeneo mengi hayakujengwa kwa kufuata ramani na kanuni za mipango miji hali ambayo imekuwa vigumu kupitisha mitaro ya majitaka pamoja na huduma ya kunyonya maji hayo kwa kutumia magari.

Kwa jijini Dar es Salaam ni kawaida kukuta mitaro ya majitaka ikituwama maji, mabomba ya maji machafu kufumuka hata kipindi cha kiangazi huku mitaro mingi ikiwa imeziba kutokana na watu kujenga holela na kuziba njia za kupitisha mitaro hiyo.

FikraPevu inaona kwamba, bajeti inayotolewa kwa Wizara ya Maji hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam inaweza isitosheleze kwa kiwango kikubwa kutatua matatizo ya majisafi na majitaka mkoani humo.

Kwa maana hiyo, kuna haja DAWASA kukaribisha makampuni mengine ambayo yatagawana majukumu kwenye wilaya zingine za Mkoa wa Dar es Salaam na kupunguza mzigo kwa DAWASCO.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *