Hizi ndizo sababu zinazoifanya China kupiga hatua ya maendeleo kiuchumi na kiteknolojia

Daniel Mbega

WENGI wetu tunadhani ili kuwa wa kisasa na kupata maendeleo lazima tuwe kama nchi za Magharibi, hasa Marekani, lakini ukweli hauko hivyo.

Tunafikiri kuacha na kuua tamaduni zetu kama Waafrika na Watanzania na kuakisi zile za nchi zilizoendelea ndiyo njia sahihi za maendeleo, na hii ni moja ya sababu inayoifanya Tanzania kushindwa kupiga hatua ya maendeleo.

Historia inatuambia kuwa, mnamo mwaka 1820 China lilikuwa taifa lenye uchumi imara zaidi duniani ambapo wakati huo Pato lake la Taifa (GDP) lilikuwa mara sita ya lile la Uingereza na mara ishirini ya lile la Marekani.

Kuanzia karne ya 19 uchumi wa China ulianza kuporomoka kutokana na vita za ‘afyuni’ (Opium Wars) na mataifa ya Magharibi kuanza kupata utajiri kutokana na mapinduzi ya viwanda.

Hata hivyo, uchumi wa China ulianza kuimarika tena kuanzia miaka ya 1970 ambapo kiongozi wa Chama cha Kikomunisti (CCP) Deng Xiaoping alileta mageuzi na msisitizo katika ukuaji wa uchumi wa soko na akahakikisha ya kuwa Wachina wanaendelea kuthamini tamaduni zao.

Kwa upande mwingine, ni muhimu kutambua ya kuwa katika karne ya 15 na 16 China ilikuwa chini ya tawala mbalimbali kutoka nchi za Magharibi hasa Waingereza ambao walishiriki kiasi kikubwa katika kupigania afyuni (Opium).

Lakini pamoja na China kupitia chini ya tawala za kikoloni na kuhamasishwa kwa kiasi kikubwa kuwa kama watawala wao, bado waliweza kubaki na tamaduni zao imara kama tunavyoziona leo.

Tuangazie sehemu kubwa nne ambazo zimeifanya China kupiga hatua za maendeleo tunayoyaona leo hii.

Mosi, China ni taifa lenye kuheshimu tamaduni (Civilization State) na ni tofauti na vile ambavyo mataifa mengi hujiona kama ‘Nation States’. Ni kweli kwamba China inaonekana kama ‘Nation State’, lakini ukweli ni kwamba kinachoiongoza China kwa karne nyingi katika maendeleo ni kuwa na tamaduni imara jambo ambalo huwafanya Wachina wenyewe kujiona kuwa na tamaduni bora kuliko taifa lolote duniani.

Ukweli ni kwamba, mataifa mengi yenye kuthamini tamaduni zao yamewafanya wasonge mbele kimaendeleo kwani hufanya mambo kama tamaduni zao zinavyohitaji.

Mfano mzuri angalia nchi kama India, Taiwan, Japan, Korea na China yenyewe wameweza kubaki na tamaduni zao imara zinazowatambulisha leo hii.

Tamaduni ambazo zimebaki imara kwa China ziko nyingi ila nitazitaja kwa uchache tu kama vile muziki wao wa asili, sanaa ya mapigano (Kung Fu), tiba za asili, namna ya kula (hasa kwa vijiti), mavazi, salamu na nyingine nyingi.

Tamaduni hizo zote ndizo zinazofanya China kusonga mbele kimaendeleo kwani mfumo wao wa kuongoza nchi unaendana na tamaduni hizo na unaheshimu umoja unaoletwa na tamaduni hizo na kuwapa utambulisho kama taifa.

Lakini jaribu kutafakari Tanzania yetu leo hii tumepeleka wapi tamaduni zetu? Je, Tanzania inawezaje kutambulika huko nje na kwa tamaduni zipi tulizobakisha? Tunadhani kupata maendeleo ni kuwa kama nchi za Magharibi na Marekani kutupa kila kitu chetu na kuiga vya kwao.

Leo hii hata vyakula tunataka kula kama Wazungu, mavazi, tiba, sanaa na mengine mengi. Taifa lisilo na tamaduni imara haliwezi kusonga mbele na ndio maana mabepari kwa kutambua hilo wanaua tamaduni zetu kwa kasi wakisema ni mambo ya kale.

China kwa upande wa pili inathamini sana familia (Value for Family) kama sehemu imara ya kuunganisha taifa.

Ni wazi kwamba familia ndiyo chanzo cha watu na pia ndiyo hujenga watu wenye heshima na adabu. Kama familia itashindwa kufanya kazi yake ni kweli kwamba taifa halitakuwa na watu wenye tija na uzalendo kwa nchi yao.

Wachina wanaheshimu sana familia zao kuliko mtu mmoja mmoja. Mfano, ndoa ikifanyika ni muunganiko wa familia na siyo mume na mke tu na familia hizo zitashirikiana kwa hali na mali. Umuhimu wa familia kwa Wachina umekwenda mbali zaidi kwani jina la familia ndilo huwa la kwanza kabla ya jina la kupewa lakini kizuri zaidi majina yao huwa ni ya asili na siyo ya Wazungu kama tupewavyo sisi.

Umuhimu huo wa familia unakwenda mbali kwa kuonyesha vile ambavyo wanatunza wazee na wale wasiojiweza na siyo kuachwa mitaani wakiombaomba.

Hii haimaanishi kwamba China hakuna ombaomba, la hasha! ila familia nyingi hujitahidi kuhakikisha wanasaidiana vya kutosha.

Thamani kwa familia inapungua kwa kasi nchini Tanzania kutokana na mfumo wa kibepari ambao unasisitiza ubinafsi zaidi.

Miaka ya nyuma familia zetu zilikuwa imara, tuliweza kusaidiana kwa namna mbalimbali lakini leo hii tunaona hili likipungua na kila mtu anajali maisha yake zaidi na siyo ya mwingine.

Jambo lingine la muhimu kwa Wachina ni namna wanavyoitazama dunia (Perception of the world).

Hapa tunaona tofauti kubwa kati ya China na nchi zingine za Magharibi na Marekani. Wachina wanaamini wana tamaduni bora na imara hivyo hawana sababu ya kuondoka na kuziacha na kwenda kuhangaika na tamaduni zingine.

Lakini Wachina wanaamini dunia ni sehemu ya kubadilishana malighafi usizonazo kwa zile ulizonazo (kufanya biashara).

Mtazamo wa nchi za Magharibi na Marekani ni tofauti kabisa kwani wao huwaza kuendelea kupanua mipaka na kutoka nje ya mipaka yao ili kupata malighafi zaidi, kubadili tamaduni za watu ili zifanane na zao, kubadili mifumo ya siasa na kubadili mifumo ya imani.

Ndiyo maana ujio wa wakoloni Afrika ulikuwa tofauti na ujio wa Wachina. Wakoloni walitutawala kwa nguvu, wakaiba kwa nguvu, wakatulazimisha kuwa wastaarabu na kuabudu kwa nguvu na mwisho wakatufanya watumwa kwa mateso makubwa.

Haya yote yanaendelea leo hii japo siyo kwa viboko ila kwa masharti magumu sana ya Benki ya Dunia na IMF.

Lakini tunaweza kujiuliza, hivi Wachina walishawahi kuja Afrika hapo awali kama tunavyowaona leo hii?

Tafiti zinaonyesha kuanzia karne ya 14 na 15 meli za Kichina zilishuhudiwa zikifanya biashara na nchi zilizomo pembezoni mwa Bahari ya Hindi kabla ya ujio wa Wazungu. Sehemu za kwanza kuanza kutembelewa na Wachina ilikuwa Pwani za Malindi, Zanzibar na Ethiopia, japo darasani tumekuwa tukiambiwa kuwa Mreno Vasco Da Gama ndiyo wa kwanza kufika kwenye pwani ya Afrika Mashariki kuanzia karne ya 15 na 16.

Hii inadhihirisha kwamba Wachina wao hutaka kufanya biashara na siyo kuingilia mifumo ya nchi nyingine kama wafanyavyo mabepari wenye uchu na mali zetu.

Jambo la mwisho, ni thamani kwa serikali (Value of State). Wachina wanathamini sana serikali yao kwani ndio mlinzi, kiongozi, mtoa huduma kwa wote.

Hii inatokana na ukweli kwamba, China inaongozwa na mfumo wa ubepari wa serikali (State Capitalism). Mfumo huu unaifanya serikali kuwa msimamizi wa nyanja zote muhimu za uzalishaji kuanzia viwanda, benki, shule, hospitali na nyinginezo.

Nyanja hizi hazijaachwa chini ya mikono ya watu binafsi kwani wanaamini serikali ndiyo yenye jukukumu kwa watu wake na kwa mfumo huo China imeweza kuwatoa takriban watu milioni 500 katika dimbwi la umaskini kuanzia miaka ya 1980 (Benki ya Dunia, 2015).

Lakini Tanzania inayofuata mfumo wa ubepari binafsi (Private Capitalism) imetuondoa Watanzania wangapi katika dimbwi la umaskini? Ukienda mbali zaidi na kujiuliza je, tunaithamini vipi serikali yetu iliyoacha nyanja zote za uzalishaji kwa wawekezaji? Je, tuithamini serikali ama wawekezaji wanaoendesha uchumi wetu leo hii?

Kwa kuhitimisha, Tanzania imewahi kupitia mambo yote haya manne ambayo China imeyakumbatia mpaka leo ila tukaona hayana maana katika maendeleo tukaamua kuyatupilia mbali.

Katika misingi imara iliyowekwa na Ujamaa na Kujitegemea kupitia Azimio la Arusha yalisisitizwa mambo mengine ikiwamo hayo niliyoyajadili hapo juu kama nguzo muhimu ya maendeleo.

Ni wakati sasa wa kujifunza kutoka China ili tuweze kupiga hatua za maendeleo.

Mtaalamu na mwandishi mashuhuri Martin Jacques aliyepata umaarufu kwa kitabu chake cha When China Rules the World amesisitiza ya kuwa siyo muda mrefu China itakuwa taifa lenye nguvu na imara na mfumo wake ndio utakuwa wa kuigwa, hivyo ni wazi sasa tuanze kujifunza kutoka kwao kabla hatujachelewa.

Niwatakie wote Heri ya Mwaka Mpya 2017.  

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *