Mfumo mbovu wa Elimu wachangia matokeo mabaya Darasa la IV, Darasa la VII, Kidato cha II na IV 2016 Lindi na Mtwara

Jamii Africa

KUTOWEPO kwa hamasa na ushirikishwaji wa jamii kwenye masuala ya elimu, umbali watumiao walimu na wanafunzi kusafiri kwenda shule kutoka kwenye makazi yao, upungufu walimu wa masomo ya sayansi na hisabati pamoja na mafundi sanifu wa maabara za shule, ufundishaji wa kusuasua, mazingira magumu waishiyo walimu na wanafunzi, upungufu wa vitendea kazi vya kufundishia na kujifunzia zimetajwa kama sababu zinazochangia matokeo mabaya kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hivi karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwaka 2016 kwa shule zote za msingi na sekondari nchini.

FikraPevu inafahamu kwamba, hatua hii imekuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu baraza hilo lilipotangaza matokeo ya upimaji wa mitihani ya kidato cha pili ambayo pia ilifanyika mwaka jana 2016.

Mnamo Desemba 2016, NECTA ilitangaza matokeo ya upimaji wa mitihani ya darasa la nne na darasa la saba yote ikiwa imefanyika mwaka jana 2016.

Katika matokeo yote hayo, kiwango cha ufaulu kimekuwa kikitofautiana shule hadi shule ukilinganisha na mwaka juzi 2015.

Ipo mikoa ambayo kiwango chake cha ufaulu kimeshuka kwa mfano mkoa wa Lindi huku mikoa mingine kiwango cha ufaulu kikiwa kimeongezeka kwa mfano mkoa wa Njombe ulioshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu nzuri wa jumla wa kidato cha nne.

Kwa ujumla mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikishika nafasi za mwishoni kwenye mitihani ya kitaifa.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii umebaini kuwepo kwa sababu kadha wa kadha zinazosababisha kushusha matokeo haya.

Zifuatazo ni takwimu za ufaulu wa mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2015 na 2016 kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara kama ilivyotolewa na baraza la Mitihani la Taifa.

 

MATOKEO YA UPIMAJI WA DARASA LA NNE MWAKA 2015&2016

MKOA

HALMASHAURI

KITAIFA

MKOA

HALMASHAURI

KITAIFA

 

 

2016

2015

 

 

2016

2015

MTWARA

 

21

17

LINDI

 

17

18

 

Newala (V)

74

21

 

 

 

 

 

Nachingwea

104

83

Masasi (M)

165

118

Kilwa

156

140

Mtwara (M)

98

81

Liwale

50

64

Nanyumbu

167

107

Ruangwa

120

129

Masasi (V)

170

147

Lindi (M)

75

74

Mtwara (V)

90

153

Lindi (V)

146

146

Newala (M)

97

 

 

 

Nanyamba (M)

139

 

 

 

Tandahimba

121

121

 

MATOKEO YA UPIMAJI WA KIDATO CHA PILI MWAKA 2015&2016

MTWARA

 

26

25

LINDI

 

25

24

 

Newala

164

153

 

Nachingwea

162

157

Masasi

161

137

Kilwa

134

148

Mtwara (M)

122

83

Liwale

159

154

Nanyumbu

167

159

Ruangwa

155

156

Tandahimba

166

160

Lindi (M)

140

147

Mtwara (V)

165

155

Lindi (V)

121

138

 

 

 

 

 

 

 

 

 

MATOKEO YA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2015&2016

MTWARA

 

25

25

LINDI

 

31

27

 

Newala

160

128

 

Nachingwea

178

168

Masasi

100

101

Kilwa

158

164

Mtwara (M)

60

43

Liwale

175

162

Nanyumbu

176

153

Ruangwa

173

165

Mtwara (V)

146

150

Lindi (M)

147

112

Tandahimba

163

169

Lindi (V)

135

110

 

 

 

 

 

 

 

Kama takwimu zinavyoonesha hapo juu, kiwango cha ufaulu kwa mikoa tajwa hapo juu yaani Lindi na Mtwara ni mbaya mwaka hadi mwaka. Viwango hivi haviendani na vile vya mikoa mingine ama halmashauri zingine.

Kwa miaka mitatu mfululizo yaani 2014, 2015 na 2016 mikoa hii imekuwa ikifanya vibaya kwenye matokeo ya kidato cha pili, kidato cha nne, darasa la saba na darasa la nne.

Mikoa hii imekuwa ikiingiza idadi kubwa ya shule kwenye orodha ya shule zenye matokeo mabay kitaifa.

Kwa mfano kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha pili iliyofanyika mwaka 2016, mkoa wa Mtwara pekee umeingiza shule tisa (9) miongoni mwa shule 10 za mwisho kitaifa.

Hali kadhalika, kwenye matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika mwaka 2016 mkoa wa Lindi umeingiza shule moja kutoka wilaya ya Nachingwea kwenye orodha ya shule zenye matokeo mabaya kitaifa.

Kati ya halmshauri 178 zilizosajiliwa kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka jana, wilaya ya Nachingwea kutoka mkoa wa Lindi imeshika nafasi ya mwisho yaani nafasi ya 178 huku mkoa wa Lindi kwa ujumla ukishika nafasi ya mwisho kitaifa yaani nafasi ya 31.

Mwandishi wa makala hii alibahatika kukutana na watendaji wa elimu ngazi ya wilaya na ngazi ya kata na shule lakini pia kupitia mahojiano na baadhi ya wasimamizi na waendeshaji wa elimu kwenye mikoa hii hali kadhalika jamii kwa ujumla katika kubaini sababu zilizopelekea mikoa ya Lindi na Mtwara kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani hiyo.

Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa Mtwara kupitia kwa msemaje wake katibu tawala wa mkoa (RAS) alikiri kuwepo kwa ufaulu mbaya wa shule nyingi mkoani humo huku mzigo mkubwa wakibebeshwa walimu.

Alipinga kuwepo kwa changamoto yoyote ya kijamii; kiuchumi au kimazingira kwani kupitia changamoto hizo ndimo ambamo walimu wengi wazembe wakificha uzembe wao.

Kwa mtazamo mwingine si kweli kuwa walimu ni wazembe au hawawajibiki ipasavyo kwenye majukumu yao, isipokuwa kilichofanywa hapa ni kupandikiza mizizi ya imani potofu kwa jamii kuwa walimu ndicho chanzo kikuu cha wanafunzi kutofaulu.

Hali hii inatengeneza hali ya kutoshirikikana kati ya jamii na shule.

Kupitia utafiti uliofanywa na mwandishi umebaini kuwepo kwa changamoto zifuatazo zinazokwamisha ufaulu kwa wanafunzi nazo ni;-

Katika mahojiano na baadhi ya walimu kutoka shule mbalimbali mkoani Mtwara wilayani Masasi, umbali watumiao walimu na wanafunzi kusafiri kwenda shule kutoka kwenye makazi yao umetajwa kama sababu kubwa na changamoto ya wanafunzi kutofanya vizuri kwenye masomo yao hali kadhalika kuwazuia walimu kuwajibika ipasavyo kwenye majukumu yao.

Baadhi ya watendaji wa elimu wakiwemo waratibu wa elimu kata wametaja umbali kuwa unachangia kwa asilimia kubwa kupunguza kiwango cha uwajibikaji kwa wanafunzi na walimu.

Kutokana na kutowepo kwa usawa kwenye mgawanyo wa shule ambazo nyingi ni za kata, baadhi ya wanafunzi wamejikuta wakitumia muda mrefu njiani kuelekea shule.

Umbali sambamba na jiografia ya mazingira ya mikoa hii yenye vilima, mabonde na mito wanafunzi wengi wamejikuta wakiishia njiani na kukata tama kwenda shule (utoro). Wanafunzi wengine huchukua maamuzi hata ya kutokwenda kabisa shule hali inayosababisha utoro wa kudumu.

Hali ngumu ya kiuchumi kwa familia za watoto hawa; wanafunzi hawa wanaoathiriwa na umbali hushindwa kumudu gharama za kupata vyombo vya usafiri kama vile baiskeli ambazo kwa mikoa hii ya kusini ndicho chombo kikuu cha usafiri.

Kutokana na kukosa pesa wanafunzi hawa hasa wa kike wamekuwa wakiingia kwenye vishawishi wakishawishiwa na madereva wa bodaboda wanaotumia vyombo vyao kuwasafirisha wanafunzi hawa kwenda shule.

Katika mazingira machache ya mji hususani Mtwara manispaa na Lindi manispaa wanafunzi pia hushindwa kumudu gharama za nauli ambapo kila siku mwanafunzi hutakiwa kusafiri zaidi ya kilometa tatu kwenda shule.

Shule ya sekondari Ruponda iliyoshika nafasi ya 3273 kitaifa kati ya shule 3280 za sekondari nchini nis shule ya kata ya Ruponda inayochukua wanafunzi kutoka vijiji mbalimbali vya kata hiyo.

Hata hivyo wanafunzi wengi wasomao kwenye shule hiyo ni wale watokao kwenyevijiji vilivyopo nje kidogo ya makao makuu ya kata ya Ruponda yapata kilometa tatu au zaidi.

Umbali huu ni mrefu sana kwa wanfunzi atembeaye bila ya usafiri.

Hali hii inarudisha nyuma matumaini wanafunzi wengi hivyo kujikuta wakiingia kwenye utoro wa kudumu.

Uwajibikaji, ushirikishwaji na uhamasishaji mdogo kwa wazazi wa wanfunzi;- jamii ya watu waishio mikoa ya kusini mwa Tanzania hasa Mtwara na Lindi ni jamii ambayo bado haijatilia mkazo kwenye suala la elimuna umuhimu wake.

Kimsingi hii inatokana na hamasa ndogo na kukatishwa tamaa na maendeleo ya watoto wao shule.

Kwa hali hii wazazi wengi wamekuwa wakiwatumia watoto wao kama chumio la vipato kupitia shughuli mbalimbali zinazowahusisha watoto hao kama vile kuwafanyia sherehe kwa ajili ya kupata pesa; mahari zipatikanazo kupitia kuwaozesha watoto wa kike na nguvukazi hasa kwa watoto wa kiume kwenye shughuli za kilimo.

Wananchi wengi ni wakulima wa mazao ya korosho, ufuta na mbaazi na huwatumia watoto wao kuwasaidi katika kilimo cha mazao hayo huku suala la shule likipatiwa muitikio mdogo.

Jukumu la kusisitiza elimu kwa watoto siku zote linapaswa kuanzia kwenye ngazi ya familia. Pale familia inapotoa muitikio na umuhimu mdogo hata watoto wenyewe wanalipa umuhimu mdogo.

Kama jamii haitasisitiza kuhusu maadili na tabia njema wakati wote kwa watoto na kuwajengea saikolojia ya kupenda elimu na kukemea masuala yanayoenda kinyume na maadili ya elimu.

Uchumi wa jamii ya watu wa kusini mwa Tanzania ni ule unaotegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile korosho na ufuta.

Katika msimu wa kilimo mwaka 2016-2017, mauzo ya zao la korosho yamekuwa ni ya kusuasua kwani wakulima wengi hawajapata pesa za malipo yao hadi hivi sasa hali iliyowafanya washindwe kumudu gharama kuwaandalia mahitaji ya shule watoto wao waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari.

Hadi kufikia tarehe 16/01/2017, siku ambayo mwaka wa masomo wa 2017 ulianza, ni wanafunzi 3 tu ndio walioweza kuripoti shule ya sekondari Ruponda kati ya wanafunzi 90 waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo.

Wakieleza sababu za watoto wao kutoripoti kama walivyotakiwa, wazazi wa wanafunzi wengi walitaja sababu kuwa ni ‘kukosa pesa ya kuwanunulia sare za shule (uniforms), viatu na daftari’.

Wazazi hawa wameshindwa kuwapeleka watoto wao shule kutokana na kukosa ya vitu hivyo. Hata hivyo sababu inayoonekana hapa ni kutowepo kwa hamasa baina yao kwani mwanafunzi anaruhusiwa kuripoti shule hata akiwa nje ya sare za shule kwani kufanya hivyo ni kumnyima haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Kutowepo kwa hamasa kunachochea mambo mengi ambayo waamuzi wakubwa ni wazazi kama vile, masomo ya ziada; kushiriki kwenye kambi za mada ngumu zifanyikazo shule.

Walimu; kwenye utekelezaji wa mikakati na mopango yoyote, walimu ndio kipaumbele kikubwa kikifuatiwa na wanafunzi na jamii kwa ujumla. Endapo mwalimu hatojaliwa japo kwa kupewa ‘motisha’, hatoweza kutekeleza mipango yoyote ipasavyo.

Mkoani Lindi na Mtwara jitihada zilifanyika katika ujenzi wa vyumba vya maabara ambazo nyingi ya hizo bado hazijakamilika toka mwaka 2012.

Baadhi ya maabara chache zilizokamilika bado hazijaletewa vifaa vya maabara.

Changamoto nyingine kubwa inayorudisha nyuma elimu na ufaulu wa watoto kwenye mitihani yao ni ukosefu wa walimu wa sayansi na hisabati sambamba na mafundi sanifu wa maabara (laboratory technicians) kuhudumia maabara hizo.

Mpango wa elimu bure ulioasisiwa na serikali ya awamu ya tano umekuja na changamoto ya ongezeko la idadi kubwa la wanafunzi huku idadi ya walimu ikibaki ile ile kutokana na kusitishwa kwa ajira za walimu. Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ni mkubwa. Walimu hasa wa masomo ya sayansi na hisabati wamekuwa shida.

Zipo shule ambazo hazina mwalimu wa sayansi au hisabati kabisa na zipo shule ambazo zina mwalimu  1 anayetakiwa kufundisha masomo mawili ya sayansi kuanzia kidato cha I hadi kidato cha IV.

Shule ya sekondari Nachingwea ni shule ambayo ina mwalimu 1 tu wa hisabati anayefundisha pia somo la fizikia.

Hali imekuwa ikipunguza kazi ya uelewa kwa wanafunzi kwani kwa muda mrefu wanabaki bila kufundishwa.

Vile vile shule zilizopo kwenye mikoa hii zinakosa walimu kutokana na dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kuwa mikoa ya kusini ina mazingira magumu zaidi ya kufanyia kazi hivyo basi wengi huwa hawaripoti pindi wanapopangiwa kwenye mikoa hii.

Ufaulu mdogo darasa la saba; alama za ufaulu darasa la saba kuingia kidato cha kwanza pia zimetajwa kama kiashiria na kipimo cha uwezo wa mwanafunzi. Kwa kawaida jumla ya alama 250 hadi 100 zinatakiwa kwa mwanafuzi kujiunga na shule ya sekondari.

Lakini kutokana na uwingi wa shule za kata, wanafunzi wenye alama za chini ya 100 pia hulazimika kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari.

Hali hii inachangia kushusha kiwango cha ufaulu kwani watoto wanakuwa na ugumu katika kuyamudu masomo yafundishwayo shule za sekondari kwa lugha za kiingereza. Kwa utafiti wa shule zilizofanya vibaya mkoani Mtwara ni wanafunzi waliopata alama za chini kwenye mitihani ya darasa la saba ndio wamechangia kushusha kwa ufaulu huo.

Usimamizi, uendeshaji na ugharimiaji mdogo wa elimu; kutokana na utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii, umebaini pia kutokana na usimamizi na uendeshaji mdogo na ugharimiaji mdogo, shule nyingi zinashindwa kujiendesha na kubuni mikakati mbalimbali ya kielimu. Shule nyingi zinategemea ruzuku kutoka serikalini ambayo wakati mwingine huchelewa kuwasilishwa ama kuwasilishwa chini ya kiwango cha mahitaji.

Kupitia mango wa elimu bure, serikali hupeleka kiasi cha shilingi bilioni 18 kwenye shule zote Tanzania.

Hata hivyo, nje ya pesa hizi serikali haijatenga pesa kwa ajili ya kuandaa mitihani ya ndani; ununuzi wa vifaa vya ufundihaji na ujifunzaji. Idara za ukaguzi wa elimu ngazi ya wilaya na mkoa zinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kuetndea kazi.

Kwa kawaida, ukaguzi na tathmini ni mojawapo ya misingi ya elimu bora na hutakiwa kufanyika mara kwa mara mashuleni lakini katika hali ya kustaajabisha kwenye mkoa wa Lindi na Mtwara ukaguzi hufanyika tu pindi matokeo ya mitihani yanapokuwa mabaya.

Kutowepo kwa mipango, na mikakati ya kuboresha elimu mashuleni; kutowepo kwa mipango na mikakati ya kuboresha elimu ama kuwepo kwa utekelezaji hafifu wa mipango hiyo kutejwa pia kama sababu inayochangia kuwepo kwa matokeo mabaya.

Tatizo la upungufu wa walimu linafahamika kwenye ngazi mbalimbali za elimu zikiwemo idara, na hata watendaji wa kata. Kwanini serikali za wilaya ama mkoa zisipange utaratibu wa kuwapata walimu wa masomo ya sayansi kutoka miongoni  mwa vijana waliomaliza vyuo vikuu, kwa kutenga mafungu ya pesa kutoka kwenye bajeti zao?

Kusuasua kwa ufundishaji mashuleni pia ni changamoto nyingine. Kwanini idara za ukaguzi wa elimu wilaya na mkoa, zisiweke utaratibu wa kutembelea shule zote mara kwa mara katika kuangalia na mwenendo wa ufundishaji na ujifunzaji hali kadhalika kubaini changamoto wanazokabiliana na walimu katika ufundishaji na uendeshaji wa shule?

Wazazi kutotambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao pia kunachangia kupata ufaulu wa chini.

Kwanini serikali za wilaya na mikoa zisiweke utaratibu wa kutoa hamasa kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watoto na kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kupanga mikakati na mipango mbalimbali shuleni?

Serikali ni lazima itambue wazi kuwa suluhisho na mwarobaini wa tatizo kwa ufaulu mdogo linaanzia kwenye mfumo mzima wa elimu na kuishia kwenye jamii.

Serikali ipunguze mzigo kwa walimu waliopo kazini kwa kufungua ajira mpya kwa walimu watakaokwenda mashuleni kufundisha. Bado shule nyingi sana hazijajitosheleza kwenye idadi ya walimu. Wanahitajika kwa kiwango kikubwa kufanikisha elimu bure.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *