Haya ndiyo mateso ya siri wapatayo wanawake wanaotoa mimba

Daniel Mbega

KUHARIBIKA kwa kondo la nyuma, kuharibika kwa mfuko wa neva na mimba zinazofuata, kuwa tasa, kufariki kwa mama au mama kuamua kujiua baadaye, ni miongoni mwa mateso ya siri wapatayo baadhi ya wanawake wanaotoa mimba, FikraPevu inaripoti.

Hayo yamethibishwa na madaktari ambao wamesema matatizo hayo yamekuwa sugu miongoni mwa wanawake wanaothubutu kutoa mimba kwa sababu yoyote ile.

“Uzoefu unaonesha kuwa, wanawake wengine wanaponusurika kutoa mimba bila madhara makubwa, hujenga usugu na hiyo kuwa tabia yao; mwisho anazeeka bila mtoto,” anasema Dk. Saili Mbukwa, Kaimu Mkurugenzi wa Programu, Uzazi na Malezi bora Tanzania (UMATI) Makao Makuu.

Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Pro-life) Tanzania, Emil Hagamu, anasema utoaji mimba humsababishia mwanamke maumivu makali tumboni, kuwa hatarini kupata saratani ya kizazi, upungufu wa damu, kupata maambukizo ya vijidudu na uwezekano wa kupasuka tumbo la uzazi.

Kisaikolojia, anasema, “Mwanamke anahangaika na kukosa amani akijihisi mkosaji au mwuaji na aliyepotelewa kitu maishani; hulia na kujutia.”

“Wengine wanatawaliwa na mawazo ya kifo hata kufikiria kujiua, wanakuwa katili na wenye hasira, waliokata tamaa na wanaojisikia kupoteza hadhi na haki ya umama.”

Dk. Bahati Maxwell wa Kituo cha Afya – Buguruni, Anglikana Ilala, anasema utoaji mimba huwafanya wanawake wengine kujidhani wamepata mimba za kuhisi ambazo baadaye huonekana zimepotea kimiujiza kumbe hazikuwapo.

 

Uchunguzi

Imebainika kuwa, baadhi ya wanawake waliotoa mimba wanatamani, wanawapenda au kuwachukia watoto wa wengine.

“Nikiona vitoto navitamani sana ndiyo maana ninapenda kununua midoli,” anasema Sophia Ramadhan (siyo jina halisi), mwanafunzi wa chuo kimoja cha uandishi wa habari wilayani Ilala anayekiri kuwahi kutoa mimba aliyoipata kwa mwanamume mwingine kabla ya kufunga ndoa kanisani miaka minne iliyopita, jijini Dar es Salaam.

Imebainika kuwa, utoaji mimba huiongezea familia gharama mwanamke husika anapofariki au kupata matatizo yanayohitaji huduma za matibabu.

Wengine wanapofahamika kuwa walitoa mimba, hunyanyapaliwa, kukosa ndoa au ndoa zao kuwa hatarini hasa wanapopata utasa.

John James wa Pugu, Ilala anasema, “Barani Afrika, fahari ya mwanamke ni uzazi na fahari ya ndoa ni watoto; nani ataoa mwanamke anayejua kuwa hana uzao kwa sababu tu, alisha-flash watoto tumboni!”

 

Mkasa wa majonzi

Amina Joseph (44) (siyo jina lake halisi), mfanyabiashara wa mbogamboga sokoni Buguruni, anasimulia madhira yaliyomkumba kwa kutoa mimba miaka miwili iliyopita.

Anasema aligundua mumewe alikuwa na “mchepuko” wakati yeye akiwa mjamzito. Akaamua kumkomesha kwa kuitoa mimba. Kwa kujua Serikali hairuhusu kitendo hicho, alielekezwa duka moja la dawa hapo Buguruni.

Siku hiyo mumewe akiwa safarini alitakiwa kurudi jioni wakati usiku ukiingia akiwa na Shs. 60,000 walizokubaliana.

Wakiwa chumbani, mhudumu aliyemsaidia kuitoa mimba ya miezi mitano, alimpa sharti la kufanya naye mapenzi kwanza, kitendo anachosema ni kubakwa.

Anasema alishindwa kupiga kelele wala kukataa kwani alishampa pesa na umma ungemuuliza alifuata nini chumbani usiku ule. Hii ni kati ya hatari wanazokumbana nazo baadhi ya wanawake wanapokwenda kutoa mimba.

Amina anasema huu ni mwaka wa pili mzunguko wa hedhi haujulikani. “Nataka kuzaa, lakini sipati mimba. Ninashindwa kumwambia mume wangu ukweli tutafute ufumbuzi; anatumia fedha nyingi, lakini siwezi kumweleza kilichotokea,” anasema.

 

Kilio cha wanaharakati na wanasheria

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) Tike Mwambipile anasema, “Sheria za nchi zinazuia utoaji mimba na imani zetu haziruhusu, lakini tatizo lipo. Watu wanaogopa sheria; wanatolea mimba vichochoroni; wengine kwa kukosa pesa, wanatumia dawa za kienyeji. Wanahudumiwa katika mazingira hatari; kwanini tuendelee kukaa kimya!”

Mhadhiri Mwandamizi katika Shule ya Sheria Tanzania, Dk. Julius C. Mashamba, anasema, “Changamoto zilizopo sasa zinahitaji kuruhusu mjadala wa utoaji mimba salama inapolazimu ili kumlinda mtoto dhidi ya athari za jinai kama kubakwa.”

Anahoji, “Kwanini tunamfunga mbakaji, lakini hatumlindi mtoto aliyebakwa; tunamwachia mahangaiko? Maputo Protocol itasaidia kuboresha sheria za makosa ya jinai kwa kuweka mipaka ya ulinzi wa kisheria kwa waliolazimika kutoa mimba na sheria imlinde daktari anayepaswa kutoa huduma hiyo kihalali.”

 

Msimamo wa Serikali

Mratibu wa Mikoa na Kanda wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Kitaifa, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Martha Shakinyau anasema, Mwongozo wa Serikali unataka mwanamke ambaye mimba imeharibika ahudumiwe katika mazingira salama, penye mtaalam, dawa na vifaa safi, sahihi na vya kutosha kwa kuangalia usalama wake.

“Ikiwa ana matatizo mengine kama ugonjwa wa moyo, kisukari na kifafa cha mimba mambo hayo yadhibitiwe ili mama huyu awe salama… Sheria za Tanzania haziruhusu utoaji mimba…” anasema.

 

Nini kifanyike

TAWLA inasema, “Tanzania imesaini Mkataba wa Kimataifa wa Maputo (Maputo Protocol), iokoe watu wake kwa kuufanya mkataba huo kuwa sheria, hasa Ibara ya 14 (2) (c) juu ya afya ya ujinsia ili kulinda haki ya kizazi kwa wanawake.”

“Uwepo mjadala mpana kuhusu kuruhusu utoaji mimba kitabibu kwa mazingira yanayothibitishwa kisheria na kitaalam kwamba ni lazima ili kuokoa uhai.”

Mratibu wa kitaifa wa taasisi ya ULINGO, Dk. Avemaria Semakafu anasema jamii iungane kulinda maadili na kutoa elimu sahihi ya kiroho na kiafya kwa makundi maalum wakiwamo wanandoa na wanafunzi ili kuepuka mimba kabla ya wakati sahihi, hivyo kuepuka maambukizi ya VVU.

Ufanyike uchunguzi na ukaguzi wa ghafla katika maduka ya dawa na zahanati kubaini mazingira ya huduma zao.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *