Utafiti: Asilimia 10 hadi 25 ya bajeti ya familia hugharamia huduma za afya

Jamii Africa

Imebainika kuwa nusu ya watu wote wanaoishi duniani hawapati huduma bora  za afya jambo linalowatumbukiza kwenye umaskini kutokana na kutumia gharama kubwa za matibabu.

Licha ya juhudi mbalimbali za mashirika ya kimataifa kuboresha afya ya ulimwengu bado gharama za upatikanaji wa huduma za afya zimekuwa kikwazo kwa wananchi kuondokana na umaskini wa kipato na kifikra.

Kulingana na Ripoti ya Usimamizi wa Afya ya Ulimwengu (2017) iliyotolewa na Benki ya Dunia na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaeleza kuwa licha ya hatua iliyopigwa kuimarisha afya duniani, watu bilioni 3.5 karibu nusu ya watu wote hawapati huduma bora za afya.

Kutokana na hali hiyo kila mwaka watu milioni 100 huingia kwenye umaskini wa kiwango cha juu kwasababu ya gharama kubwa za matibabu ambazo hawawezi kuzimudu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa watu milioni 800 hutumia asilimia 10 hadi 25 ya bajeti ya familia kwenye huduma za afya, ambapo huathiri mwenendo wa mapato katika ngazi ya kaya.

Wananchi wengine hulazimika kukopa fedha ili kuokoa maisha yao. Wanawake na watoto ndio wanaoathirika na ukosefu wa huduma bora za afya katika maeneo mbalimbali duniani.

Sara Robert, mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam mwenye watoto 3, wawili wana umri chini ya miaka 5, ambao huugua mara kwa mara na kumlazimu kutumia fedha nyingi kuwatibu katika hospitali binafsi.

Sara ambaye anamiliki duka dogo la mahitaji ya nyumbani, anasema hawawezi kumudu gharama zote za matibabu kwasababu biashara yake haizalishi faida inayoweza kukidhi mahitaji yote ya familia.  

“Biashara ya duka haitoshelezi mahitaji yote ya nyumbani na wakati huo huo zinahitajika fedha kwa ajili ya matibabu, nalazimika kukopa ili watoto wangu wawe na afya bora na kuweza kuhudhuria shule”, anaeleza Sara Robert.

Kutokana na hali hiyo ya umaskini wa kipato ndani ya familia, WHO imeanzisha mfumo wa Usimamizi wa afya ya ulimwengu ili kumuwezesha kila mtu kupata huduma bora za afya bila kujali hali yake ya maisha.

Mpango huo ambao unaongozwa na dira ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ya 2015/2030 unakusudia kuondoa vikwazo vyote vya upatikanaji wa huduma za afya ikiwemo gharama kubwa za matibabu ikizingatiwa kuwa afya ni huduma muhimu kwa maisha ya mwanadamu yeyote.

Nchi wahisani ambazo zinatekeleza SDGs zinaelekezwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya kuboresha miundombinu, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa, vifaa tiba ili kuwapunguzia wagonjwa gharama kubwa za matibabu.

Tanzania ni miongoni nchi ambazo zinatekeleza SDGs na kwa sehemu kubwa imefanikiwa kuboresha afya ya mama na mtoto na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi wa mpango.

Hata hivyo, sekta ya afya nchini inakabiliwa na uhaba wa madaktari na upatikanaji wa dawa, hali ambayo huongeza gharama za matibabu kwa wananchi na kuzidi kuwaweka katika mfumo wa umaskini usioisha.

 Akizungumza kwenye ufunguzi wa hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila iliyopo mkoani Pwani, rais John Magufuli amesema Tanzania ina watumishi wa afya 89,842 kati ya 184,901 wanaohitajika na upungufu wa watumishi 95,059 wakiwemo madaktari na wauguzi.

Takwimu hizo za serikali zinathibitishwa na ripoti ya shirika la Twaweza (2017) kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii ambapo wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi wanakumbana na uhaba wa madaktari wakienda kutibiwa katika vituo vya afya.

 “Wananchi watatu kati ya kumi (29%) waliohojiwa wanasema hawakukuta madaktari, na idadi sawa na hiyo walikuta huduma zikiwa ghali sana au wahudumu wa kituo cha afya hawakuwajali au kuwaheshimu”. Inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Changamoto nyingine ni Wananchi wanaoenda kutibiwa katika vituo mbalimbali nchini wamekiri kukumbana na upungufu wa dawa na wakati mwingine dawa muhimu hazipatikani katika vituo hivyo.

Ripoti hiyo ya Twaweza iliyoangazia maoni ya wananchi inathibitisha kuwa asilimia 70 ambayo ni sawa na wananchi 7 kati ya 10 waliokwenda kutibiwa ndani ya miezi mitano iliyopita walikutana na upungufu wa dawa na vifaa tiba.

 Kutokana na gharama kubwa ambazo wananchi wanatumia kupata huduma za afya, nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania zinashauriwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya unaolenga kutoa huduma bora zenye gharama ndogo ili kukuza uchumi wa wananchi wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *