Ujenzi wa Reli ya Kati kuondoa adha ya usafiri. Jiwe la msingi kuwekwa wiki hii

Jamii Africa

UJENZI wa kipande cha kwanza cha Reli ya Kati chenye urefu wa kilometa 300 unatarajiwa kuanza mwezi Aprili, mwaka huu huku uwekaji wa jiwe la msingi ukitarajiwa kufanyika wiki hii.

FikraPevu imeelezwa kwamba, kipande hicho ambacho ni cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kikihusisha kilometa 203 za njia kuu na kilometa 100 za michepuko (Spurs) ni sehemu ya kilometa 1,219 zinazotarajiwa kuanza kujengwa katika kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar-Tabora-Isaka-Mwanza.

Meneja Uhusiano wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Catherine Moshi, ameieleza FikraPevu kwamba, reli hiyo itajengwa kwa awamu kwa kuanzia na kipande hicho cha Dar es Salaam-Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa (wa tatu kutoka kulia waliokaa), akisaini Mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya Kisasa (Standard Gauge) na wawakilishi wa Makampuni yatakayojenga reli hiyo jijini Dar es Salaam Februari 3, 2017.

“Mambo yamekwishaiva na hivi ninavyozungumza na wewe maandalizi ya kuweka jiwe la msingi yanaendelea ambapo uzinduzi rasmi utafanyika wiki ijayo ili kuwapa fursa makandarasi waanze ujenzi mara moja,” alisema Moshi.

Februari 3, 2017 Serikali ilitiliana saini ya makubaliano ya ujenzi wa kipande cha reli katika mkataba wa ubia na kampuni za Yapi Merkezi ya Uturuki na Mota-Engil Africa ya Ureno kwa gharama ya Dola 1.1 milioni za Kimarekani.

Utiaji huo wa saini ulishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Mbarawa, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya Yapi Merkezi, Erdem Arioglu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mota-Engil Africa, Manuel Antonio Mota, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Sekta ya Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho, na Mkurugenzi Mkuu wa (RAHCO), Masanja Kadogosa.

FikraPevu imeelezwa kwamba, ujenzi huo utafanyika kwa miezi 30 ukihusisha ujenzi wa miundombinu ya umeme, stesheni sita za abiria na sita za kupishana treni na ujenzi wa wigo wa 102km kwa usalama wa watu na magari.

“Zoezi la kubomoa majengo yaliyo ndani ya hifadhi ya reli linaendelea kote katika reli hii kwa sasa, tunataka mkandarasi akianza ujenzi asikumbane tena na vikwazo ambavyo vinaweza kukwamisha utekelezaji wake,” amesema Moshi.

Treni ya kasi zaidi

Treni kama hii ndiyo itakayotumika kusafirisha abiria katika Reli ya Kati mara ujenzi wa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) utakapokamilika.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alisema wakati wa utiaji saini mkataba huo kwamba, ujenzi wa reli hiyo itayotumia umeme na kwenda kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa itakuwa ni ya kwanza kwa Afrika ikifuatiwa na nchi ya Morocco.

“Tunataka kuifanya nchi yetu iwe ndogo kwa kutumia miundombinu ya kisasa ndio maana Serikali imeamua kujenga reli hii itakayotumia umeme na kwenda spidi kubwa kuliko nyingine zote barani Afrika,” alisema Prof. Mbarawa.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa reli hiyo utaongeza chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na kubainisha kuwa safari ya Dar hadi Moro itatumia muda wa saa 1:16 wakati Dar hadi Dodoma itatumia muda wa saa 2:30 na safari ya Dar hadi Mwanza itatumia muda wa saa 7:30.

FikraPevu inatambua kwamba, usafiri wa treni utakuwa ni wa haraka baada ya ule wa anga kuliko wa mabasi ambayo kwa kawaida yanatumia saa 3:15 kutoka Dar hadi Morogoro, saa 7:30 kutoka Dar hadi Dodoma na saa 14:00 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Katika mkataba huo, kampuni za Yapi Merkezi na Mota-Engil Africa kila moja ina asilimia 50 baada ya kushinda zabuni.

Nchi za Maziwa Makuu kunufaika

Mtandao wa Reli ya Kati na Reli ya Kaskazini uliopo sasa

Mtandao mpya wa Reli ya Kati na Reli ya Kaskazini

Hata hivyo, Moshi ameieleza FikraPevu kuwa, ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar-Tabora-Isaka-Mwanza ni sehemu ya njia zote za Reli ya Kati inayohusisha jumla ya kilometa 2,561, ambapo kukamilika kwake kutarahisisha usafiri kwa nchi za Maziwa Makuu kama Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

“Njia hizi ni Tabora-Kigoma (411km); Kaliua-Mpanda (210km); Mpanda-Karema Port (111km), Uvinza-Kalelema Border (mpaka na Burundi – 203km); na Isaka-Keza/Rusumo-Ruvubu nchini Rwanda kilometa 407,” alisema.

Akaongeza: “Reli ya zamani (hii inayotumika sasa) ilikuwa inaishia Mpanda, lakini tumeamua kuiongeza hadi Bandari ya Karema ambako itasaidia kubeba mizigo ya nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na abiria.”

Aidha, mchepuko wa kutoka Uvinza hadi Kalelema kwenye mpaka na nchi ya Burundi nao utasaidia kutanua mtandao wa usafiri wa reli, kwani Warundi nao wataanza kujenga reli hiyo kutoka hapo mpakani hadi Gitega kupitia Musangati.

Kuhusu kipande cha Isaka-Keza, FikraPevu imeelezwa kwamba kutakuwa na makutano hapo Keza ambapo utakuwepo mchepuko wa kutoka Keza kupitia Kabanga (mpakani) hadi Gitega nchini Burundi, na kwamba kipande ambacho kitajengwa na Warundi ni kutoka Kabanga hadi Gitega.

“Tutajenga pia kipande cha Keza hadi Rusumo, mpakani na Rwanda, ambapo Wanyarwanda nao watajenga kipande cha kutoka hapo hadi Kigali,” alisema Moshi.

FikraPevu inafahamu kwamba, bajeti ya ujenzi wa reli hiyo kwa upande wa Tanzania itakuwa kiasi cha Shs. 16.7 trilioni (takriban Dola 7.5 bilioni za Marekani).

Zabuni nyingine kufunguliwa Mei

Ameongeza kuwa, ufunguaji wa zabuni kwa ajili ya ujenzi wa vipande vingine umesogezwa mbele hadi Mei mwaka huu ili kutoka nafasi kwa kampuni zaidi kuomba.

Vipande vilivyosalia katika awamu zinazofuata ni kutoka Morogoro-Makutopora, Dodoma (336km); Makutopora-Tabora (294km); Tabora-Isaka (133km); na Isaka hadi Mwanza (248km).

“Tukimaliza hapo tunageukiza vipande vya Tabora-Kigoma; Kaliua-Karema Port; Uvinza-Keza-Rusumo,” Bi. Moshi aliiambia FikraPevu.

Tunachokijua FikraPevu

Awali, ujenzi wa reli yote ya kati ulikuwa ufanywe na kampuni ya Kichina ya China Railway Construction Corporation Limited (CRCC), lakini mchakato huo ukatenguliwa na kuanza upya.

Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile na Naibu Meneja Mkuu (Mikopo Nafuu) wa Benki ya Exim ya China, Zhu Ying, wakitia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (Standard gauge), Jijini Dar es salaam. MoU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile akipeana mkono na Naibu Meneja Mkuu (Mikopo Nafuu) wa Benki ya Exim ya China, Zhu Ying, mara baada ya kutia saini Hati ya Makubaliano ya  Ushirikiano wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (Standard gauge), Jijini Dar es Salaam Julai 22, 2016. 

FikraPevu inafahamu kwamba, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli hiyo ulifanywa na kampuni ya Canarail kutoka Canada ukihusisha njia za Dar-Tabora, Isaka-Kigali, na Keza-Msongati.

Aidha, upembuzi wa njia ya Isaka-Mwanza ulifanywa na kampuni ya Cowi ya Denmark ambayo pia ilifanya kwa reli ya Tabora-Kigoma na Kaliua-Mpanda.

Kampuni ya Cowi pia ilifanya ubunifu wa msingi wa reli mpya kutoka Mpanda hadi Karema Port kwenye Ziwa Tanganyika, wakati ubunifu wa ujenzi wa reli kutoka Uvinza-Msongati nchini Burundi ulifanywa na kampuni ya HP Gauff ya Ujerumani.

Serikali pia ina mpango wa kuifufua njia ya reli ya kutoka Manyoni hadi Singida yenye urefu wa kilometa 115 pamoja na kipande cha kilometa 108 kutoka Kilosa hadi Kidatu kuunganisha na Reli ya Tazara katika jitihada zake za kuimarisha miundombinu ya reli nchini.

Aidha, FikraPevu inatambua kwamba, hivi sasa upembuzi yakinifu unaendelea katika baadhi ya vipande vya Reli ya Kaskazini (zamani ikifahamika kama Reli ya Usambara) kwa kuiboresha kuwa ya kisasa kutoka Ruvu-Mruazi (188km) na Tanga-Moshi-Arusha (438km).

Mpango huo ni pamoja na kujenga reli mpya kutoka Arusha-Musoma (600km) pamoja na tawi la kilometa 70 kwenda Shinyanga kuungana na Reli ya Kati, lakini pia kutakuwa na kipande cha kutoka Ziwa Manyara hadi Ziwa Magadi kwenye machimbo ya magadi katika eneo la Engaruka pamoja na fosfeti huko Minjingu.

Catherine Moshi, Meneja Uhusiano wa RAHCO, ameithibitishia FikraPevu kwamba nia ni kutaka kuunganisha mtandao huo ili kurahisisha usafiri kwa treni kila mahali katika kanda hiyo.

“Kama ukitoka Moshi au Arusha unataka kwenda Rwanda au Burundi unaweza kwenda moja kwa moja bila kupitia Reli ya Kati, itarahisisha usafiri wa abiria na mizigo,” alisema.

Tangu Shirika la Reli Tanzania (sasa Kampuni ya Reli – TRL) lilipobinafsishwa mwaka 2007, njia nyingi za Reli ya Kati zimeshindwa kutumika ipasavyo huku Reli ya Kaskazini ikiwa haitumiki kabisa.

Wakati wa uhai wake, mwaka 2003 mtandao wa reli wa TRC uliweza kusafirisha jumla ya abiria 683,861 na tani 1,442,713 za mizigo, lakini wakati linabinafsishwa kiwango hicho kilikuwa kimepungua hadi kufikia abiria 593,889 na tani 545,241 za mizigo.

Hali hiyo inaelezwa kuchangiwa na ufisadi na uzembe wa watendaji, huku wengi wakituhumiwa kuna njama za makusudi na wafanyabiashara wanaohusika na usafirishaji kupitia malori na mabasi, ili wafanyabiashara hao washike hatamu.

Licha ya uboreshaji wa magari kwa sasa ambayo yanakwenda kwa kasi zaidi tofauti na zamani, pamoja na miundombinu bora ya barabara, usafiri wa reli bado unapaswa kuwepo kwa sababu unaweza kuingiza mapato makubwa kwa serikali.

Mizigo mingi inayosafirishwa na malori, iwe ndani ama nje ya nchi, inaweza kusafirishwa kwa treni na kuondoa msongamano wa malori pamoja na makontena bandarini kama ilivyo sasa, kwani treni moja linaweza kubeba hata makontena 50 yenye urefu wa futi 40 kwa mara moja.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *