CHADEMA, Busara itawale uteuzi wagombea ubunge Afrika Mashariki

Elias Mhegera

LEO  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kitafanya uamuzi wa kuwapata wagombea wake kwa nafasi zake mbili za wabunge wa Bunge la Afrika ya Mashariki (EALA).

Kamati Kuu inayokutana Zanzibar ndiyo itafanya uamuzi huo pamoja na kutathmini kwa kina maendeleo ya chama.

Sina haja ya kuyarejea yaliyopita katika zoezi hilo pale bungeni Dodoma, lakini pia ni vyema kufahamishana kwamba mliingia ‘mjengoni’ mkiwa mmegawanyika kama chama, hata kama yote hayakusemwa hadharani.

Sitaki kuwa mchochezi wa mgogoro ndani ya chama, lakini naamini kwamba wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wataheshimu uteuzi wa watu 17 uliofanywa katika kikao cha tarehe 23 Machi 2017.

Hezekia Wenje na Lawrence Masha

Iwapo wagombewa wa awali walipingwa, siyo vibaya kuwapatia nafasi hiyo wengine. Kwa kufanya hivyo, viongozi wa chama wataepuka minong’ono kwamba kuna upendeleo au ubaguzi ndani ya chama hicho ambacho ni tegemeo kubwa la wapenda mageuzi nchini Tanzania.

Pia nashauri kwamba ni vyema chama kikaangalia hazina ya wanachama wake, na kuitumia vyema huku mtazamo na mwelekeo mkubwa ukiwa ni kubakiza hazina ya vijana wenye nguvu na uelewa mkubwa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2020. Orodha mpya isije kuleta mivutano isiyo na tija.

Hili ni pendekezo la mdau wenu ambaye pia ameamua kutumia kalamu yake ili kuongeza hamasa katika siasa za ushindani nchini Tanzania.  

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *