Janeth na kilio cha watoto yatima

Jamii Africa

MACHOZI ya mwanafunzi Janeth Julius (16) yanahitimisha mahojiano kwani sikuwa na ujasili wa kuuliza swali jipya. Yalibeba hisia za uchungu na ujumbe mzito uliowakilisha kilio cha watoto wa kundi lake.

Sikujua kuwa hakuwahi kupita kwenye mikono salama wala kuonja malezi ya wazazi. Pengine aliamini swali nililomuuliza lisingeleta ufumbuzi wa matatizo anayokabiliana nayo kwa sasa. Chozi la mtoto yatima.

Ni mwanafunzi wa kidato cha pili Sekondari ya Lake View iliyopo mjini Bukoba na amefika hapa alipo kwa juhudi za kaka yake ambaye ni mtoto mwenzake. Walipoteza wazazi wakiwa wadogo na huo ukawa mwanzo wa kuishi peke yao.

Ndani ya nyumba dhaifu ya udongo katika kijiji cha Buhanga wilayani Muleba,waliweza kuendesha maisha yao na baada ya Julian kaka yake kumaliza darasa la saba alielekea mjini Bukoba kwa shingo upande akimwacha nyuma mdogo wake.

Janeth pichani

Baada ya Janeth kumaliza darasa la saba hakuchaguliwa kuendelea na masomo, kaka yake alimleta mjini na kumtafutia shule binafsi ya sekondari huku akitegemea mapato ya uendeshaji wa pikipiki za abiria ili kulipa ada na mahitaji mengine.

Nilifahamiana na kijana huyu baada ya kunisafirisha kwa pikipiki mara kadhaa, sasa tumezoeana. Ananieleza jinsi alivyolemewa na malipo ya ada ya mdogo wake wakati huo akilazimika kukabiliana na ugumu wa maisha ya mjini.

Biashara anayoifanya sio endelevu wala sio mradi wake ingawa ndiyo tegemeo pekee la kuwawezesha kukidhi mahitaji yote. Hakuwahi kufikia ngazi hiyo ya elimu ingawa anatambua umuhimu wa elimu kwa mdogo wake.

Ndoto ya Janeth
Angependa kuwa Mwanasheria ingawa safari ya kufikia mafanikio hayo tayari imezingirwa na vitisho na wiki moja iliyopita alisimamishwa masomo kutokana na deni la ada ya shule wakati huo wenzake wakiwa katika maandalizi ya mtihani.

“Siku zote nafikiria kufukuzwa shule kwa ajili ya ada namtegemea kaka kwa ajili ya mahitaji yote ya shule napenda kusomea sheria,nitawatetea watoto wenye shida kama mimi”anasema Janeth

Yapo mamia ya wanafunzi wenye ndoto kama hii ingawa msingi wa ndoto ya Julieth umejengwa kupitia changamoto nyingi zaidi. Waliishi kwa upendo kama familia ya watoto wanaojilea, kwa umri wao mdogo walibeba majukumu yote.

Walijengewa matumaini ya muda kwa kutembelewa na wageni kupitia mashirika waliofika kushangaa watoto wanaojilea. Walipewa misaada ya muda isiyoweza kukidhi ndoto ya sasa.Baadhi walisaidia kukarabati nyumba yao ya udongo.

Wanawakumbuka wageni waliopitia shirika la World Vision Kanda ya Kagera,waliopelekwa katika familia hii kuthibitisha ukubwa wa tatizo la watoto yatima.Walipigwa picha na kupewa chakula bila kuwekewa mipango endelevu.

Wanawakumbuka wageni baadhi wakiwa raia wa nje. Pamoja na kazi kubwa ya mashirika ya aina hii bado hayawaandai watoto watakaofanya kazi ya utetezi katika ofisi zao kama ilivyo ndoto ya mwanafunzi huyu.

Utetezi wao ungesukumwa na mazingira halisi waliyopita kwa nadhalia na vitendo.Hii ndiyo sababu ya ndoto ya Janeth ambaye familia yao ilitumika kama shamba darasa na leo hawana chochote cha kujivunia.

Mwanafunzi huyu anasema kutokana na uwezo mdogo wa kaka yake hawezi kujiunga na masomo ya ziada’tuition’na baada ya kutoka shuleni hujishughulisha na kazi za nyumbani huku wenzake wakiendelea kujifunza.

Anasema anafikia hatua ya kukosa hata mahitaji madogo kama madaftali na vitabu na kuwa changamoto hizo hazijamfanya kufikia hatua ya kukata tamaa ya kufikia ndoto yake akikumbuka mahangaiko makubwa ya kaka yake.

Kwa kauli yake anaomba watu watakaomsaidia kufikia matarajio yake na kuwa hali ya kusimamishwa masomo kila mara kutokana na kukosa malipo vinachangia kutofanya vizuri zaidi darasani.

Kauli ya shule.
Pamoja na uongozi wa shule ya Lake View kusifu jitihada zake darasani na kuwa sio miongoni mwa wanafunzi wakorofi wanasema suala la malipo halina mjadala kwani shule inategemea malipo hayo kujiendesha.

Mratibu wa shughuli za shule hiyo Samwel Rutanjuka anasema wanafahamu wanafunzi wao wanatoka katika mazingira tofauti na kutaka serikali iwe na mipango maalumu ya kuwasaidia  watoto wa aina hiyo.

Mwanafunzi Janeth (kushoto) akiwa na wenzake wakifuatilia moja ya kipindi darasani katika shule ya sekondari Lake View.

Uzoefu wake wa kuwa mkuu wa sekondari mbalimbali nchini safari aliyohitimisha mwaka 2007 katika shule ya Kahororo ya mjini Bukoba unamfanya alione tatizo ndani ya serikali la kushindwa kuwatambua wanafunzi wenye mahitaji maalumu ya elimu.

“Hata katika shule za serikali matatizo ni yale yale,katika selection(uchaguzi wa wanafunzi)lazima serikali itambue kuwa kuna watoto wasio na uwezo na wana haki ya kusoma,wanataka walipe ada wakati hawana uwezo wa kuwatambua”anabainisha Rutanjuka

Alilaumu kauli za kisiasa ambazo huwachonganisha wazazi na wakuu wa shule kuwa majukwaani hutoa maelekezo ya kutokuwepo baadhi ya malipo tofauti na taratibu za serikali zinavyoleza juu ya ukusanyaji wa michango yakiwepo malipo ya ada.

Akizungumzia changamoto zinazomkabili mwanafunzi Janeth alionyesha kusikitishwa na mazingira magumu ya kusaka elimu yanayomkabili na kuwa hali ya kusimamishwa masomo mara kwa mara itakuwa inamwathiri kisaokolojia.

“Mwanafunzi huyu anaweza kuwa hazina kubwa kwa taifa,umasikini wake usiwe sababu ya kukatisha masomo serikali lazima ifikirie upya jinsi ya kuwasaidia watoto wa aina hii”anasema Mratibu huyo wa shule.

Baadhi ya viongozi na wanaharakati mbalimbali wamefika hapo walipo kutokana na michango ya kudunduliza na hata wengine kufanikiwa kunusa kuta za vyuo vikuu.

Habari hii imeandikwa na mwandishi wa FikraPevu Phinias Bashaya aliyeko mkoani Kagera

Saidia ndoto ya Janeth iwezekane. Namba ya shule 0282221542 na kaka yake 0754778915.

3 Comments
  • Tatizo hili ni kubwa sana kwa wanafunzi wengi wa kitanzania.

    Naamini kama Serikali yetu ikiweka mkakati makini, itaweza kubaini watoto wenye matatizo hayo na kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kusaidiwa. Zoezi hili linaweza kuratibiwa kuanzia ngazi ya Serikali za mitaa ambako ndiko watoto wa namna hii wanaishi na wanajulikana.

  • Jamii ishikamane kwa pamoja katika kuwsaidia watoto wa jinsi hii kama Janeth, kwani tukiungana pamoja matatizo kama haya yanakuwa mepesi.

  • Tatizo hili ni kubwa hasa hapa Tanzania ni jukumu la wote kuwasaidia watoto yatima. Serikali iwaangalie watoto yatima kwani ndiyo Tegemoeo la Taifa kwa baadae.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *