Waziri Mathayo: Tutafunga uvuvi Ziwa Victoria kulinda samaki wetu

Jamii Africa

SERIKALI imetangaza azma ya kutaka kufunga shughuli zote za uvuvi katika Ziwa Victoria, iwapo mbinu na mikakati thabiti zinazochukuliwa na Serikali juu ya kulinda rasilimali hiyo zitashindwa kuzaa matunda.

Mbali na azma hiyo ya kufungwa uvuvi kwa Ziwa hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani na la kwanza kwa ukubwa Barani Afrika, Serikali imekiri wazi kwamba wavuvi ni wanjanja na ndiyo maana serikali imekuwa katika wakati mgumu kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa hilo.

Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. David Mathayo David

Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. David Mathayo David ameyasema hayo mchana wa leo Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, ambapo baadaye Waziri huyo alikutana na kuzungumza na wadau wa sekta hiyo katika ukumbi mdogo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mwanza.

Waziri Mathayo alisema, kushamiri kwa uvuvi wa samaki ukiwemo uvuvi haramu umeathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa samaki, na kwamba kwa sasa Serikali kupitia Wizara yake inafanya mazungumzo na nchi za Kenya na Uganda kwa ajili ya kuangalia namna ya kutumia zaidi sheria ili kudhibiti uvuvi haramu ndani ya Ziwa hilo, ambalo ni chanzo Mto Nile.

“Kwa sasa Serikali ya Tanzania inafanya mazungumzo na nchi tunazomiliki nazo Ziwa hili ambazo ni Uganda na Kenya. Mazungumzo yetu haya yanalenga kutaka kutumia sheria zaidi kudhibiti hali hii.

“Lakini tukishindwa tutafunga kabisa uvuvi ndani ya Ziwa hili. Hatuwezi kuendelea kuona rasilimali ya samaki zinapotea…hivyo tutahakikisha kazi hii tumeifanya kwa faida ya wote maana sisi Tanzania ndiyo tunaomiliki eneo kubwa la Ziwa Victoria”, alisema Waziri huyo wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Mathayo.

Akikazia zaidi katika hilo, Waziri Mathayo aliziagiza vyombo vya dola na mamlaka mbali mbali, ikiwemo Mamlaka ya Kukusanya Mapato nchini (TRA), kuhakikisha vinafuatilia na kuwakamata watu wote wanaoendesha uvuvi haramu katika Ziwa hilo na mengine hapa nchini.

“Naagiza TRA na vyombo vingine kuhakikisha vinafanyakazi zake vizuri ikiwa ni pamoja na kuwatia nguvuni wale wote watakaobainika kukiuka sheria na taratibu za uvuvi. Muda wa kubembelezana haupo, nataka kazi hii ifanyike kuanzia sasa hadi dahari”, aliagiza Waziri huyo.

Takwimu za kitaalamu zinaonesha kwamba, iwapo shughuli za uvuvi zitafungwa katika Ziwa Victoria zaidi ya watu milioni moja wanaofanya kazi ya uvuvi na familia zao, watu 2,800 wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kuchakata samaki Mkoani Mwanza wataathirika kwa kukosa ajira.

Hadi sasa takwimu zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni 35 wanaoishi kwa kutegemea uvuvi katika Ziwa Victoria kwa Ukanda wa nchi za Afrika Mashariki, wapo hatarini kukosa ajira iwapo Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na nchi ya Kenya na Uganda zitaridhia kufungwa kwa shughuli za uvuvi huo ndani ya Ziwa hilo.

Ziwa Victoria lipo futi 3,726 kutoka usawa wa Bahari, na lina eneo la maili za mraba zaidi ya 26,000, na kwamba maji ya Ziwa hilo yanamiminika kwenye mto Nile na kuelekea katika Bahari ya Mediteranea kwa umbali wa maili 4,000.

Kadhalika, Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani likitanguliwa na Ziwa Superior ambalo lipo Amerika ya Kaskazini, ni kiunganishi muhimu cha mpaka wa nchi tatu za Afrika Mashariki, ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda, na iwapo shughuli za uvuvi zitafungwa katika Ziwa hilo litaathiri Tanzania wengi sana na itakuwa historia ya dunia.

Imeandaliwa na Sitta Tuma, Mwanza

1 Comment
  • Mh. Waziri, una idara ya ufugaji samaki kama utaitumia vema hiyo idara itakusaidia sana kupunguza hilo tatizo. Nchi nyingi sana duniani kwa sasa wanategemea samaki wa kufugwa.

    Ni wakati muafaka wa wewe kusimamia ufugaji samaki upewe kipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha. Nimekuwa nikifuatilia bajeti zenu lakini kila mwaka mnatenga fedha ndogo kwa idara hiyo. Amkeni na itumieni hii idara na wataalam wake vizuri ndani ya miaka michache mtafurahi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *