Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi: Wahakikishiwe usalama ili wapate elimu bora

Jamii Africa

Daniel Samson

Ulemavu wa ngozi ni hali ambayo huweza kurithishwa toka kizazi kimoja hadi kingine, huweza kupotea na pia hali hiyo yaweza kubaki katika ukoo au familia fulani na kuwa na mlolongo wa kuzaliwa watu wenye ulemavu wa ngozi katika familia husika. 

Ulemavu wa ngozi (Albino) ni dhana inayoelezea hali ya kundi la watu na wanyama ambao wana upungufu au ukosefu wa rangi katika ngozi, macho na nywele.

Ulemavu wa ngozi hutokea kwa watu wote kila taifa, rangi, kabila na dini. Kwa nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini inakadiriwa kuwa mtu 1 kati ya watu 20,000 ana ulemavu wa ngozi, ambapo kwa Afrika kiwango kiko juu. Na kwa Tanzania ni mtu 1 kati ya watu 1,400.

Msingi wa mafanikio ya mtoto ni kupata elimu bora inayolenga kumkuza kifikra, kimtazamo na kumpatia uwezo wa kutengeneza fursa mbalimbali za maisha ikiwemo kumudu mazingira yanayomzunguka. Watoto wenye ulemavu wa ngozi kwa nyakati tofauti wameendelea kukumbana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwa wao kubata elimu bora.

Hali ya elimu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi

Licha ya jitihada za serikali kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kuwapa fursa watoto wengi kuelimika, idadi ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (Albino) katika shule za msingi na sekondari nchini inapungua kila mwaka na kutishia hatma ya kielimu ya wanafunzi hao.

Kulingana na Takwimu za Kituo Huru cha Serikali (Open Data Tanzania) za mwaka 2016 zinaonyesha kulikuwa na wanafunzi 1,916 wenye ulemavu wa ngozi katika shule za msingi za Tanzania Bara ambapo idadi hiyo imeshuka kutoka wanafunzi 3,722 mwaka 2013 ambayo ni sawa na asilimia 51.

Tangu  mwaka 2012 mpaka 2016 idadi ya wanafunzi wenye ulemavu imekuwa ikipungua na kuongezeka. Mathalani 2012 kulikuwa na wanafunzi  3,134 na mwaka uliofuata idadi ikaongezeka kabla ya kupungua sana 2016 ambapo usalama wa watu wenye ulemavu wa ngozi unatajwa kuimarika.

Baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo imekuwa na mauaji mengi ya watu wenye ulemavu wa ngozi imeonekana kuwa na wanafunzi wachache ambapo mkoa wa Geita ulikuwa na  wanafunzi 23 na Simiyu (37).

Licha ya mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora ambayo nayo imekuwa ikitajwa kuwa na vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi imeonekana kuwa na wanafunzi wengi ikilinganishwa na mikoa ambayo ilikuwa na matukio machache ikiwemo Njombe, Manyara na Lindi.

 

Idadi hiyo inawezekana ikapungua zaidi kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa na  kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kupata elimu kama watoto wengine.

Hali hiyo haitofautiani na idadi ya wanafunzi waliopo katika shule za sekondari ambapo wanafunzi wengi wakimaliza shule za msingi hawaendelei tena na elimu ya sekondari na hata chuo.

Takwimu za Kituo Huru cha Serikali zinaeleza Kwa mwaka 2016 pekee, kulikuwa na wanafunzi 525 wenye ulemavu wa ngozi katika shule za sekondari nchi nzima ambapo ni sawa na idadi ya wanafunzi wa shule moja ya sekondari.

Kwa muktadha huo robo ya wanafunzi hao wa shule ya msingi (1,961) ndio walipata fursa ya kuingia sekondari na waliobaki hawakuendelea na masomo ya sekondari na kubaki nyumbani.

Hali hiyo inafanana na miaka iliyotangulia, ambapo mwaka 2013 kulikuwa na wanafunzi 3,722 wa shule za msingi na 556 wa sekondari. Takwimu hizi zinathibitisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa wanafunzi kwenye shule za msingi na sekondari.

Uwiano wa wanafunzi wa kike na wa kiume wenye ulemavu wa ngozi katika shule za sekondari uko vizuri, ambapo mwaka 2016 kulikuwa na wasichana 227 na wavulana 298. Hii ni ishara kuwa usawa wa kijinsia katika elimu umefanikiwa lakini bado watoto wengi hawapati elimu bora.

Hata wanaopata fursa ya kwenda shuleni bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutengwa, kutothaminiwa na  ukosefu wa vifaa vya kujifunzia ambapo wengine huacha masomo.

Zipo hoja kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi nchini sio wengi na kudai kuwa hata idadi ya wanafunzi waliopo shuleni iko katika kiwango kinachostahili.

Lakini dhana hii inakosa nguvu kwasababu bado kumekuwa na mkanganyiko juu ya idadi halisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, ukiachilia ile iliyotolewa na Sensa ya watu na makazi 2012.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania kuna jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 13,676. Pia takwimu za Chama cha watu wenye Ulemavu wa Ngozi (TAS) zinaonyesha ongezeko la watu hao kuanzia mwaka 2013 na sasa inakadiriwa kufikia 18,833

Sababu za wanafunzi hao kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari

Kutokana na Tanzania kuwa kinara katika mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo mbalimbali nchini, wanafunzi wengi hawako salama ambapo hulazimika kukaa nyumbani au kwenda kwenye maeneo yaliyo salama zaidi ili kukwepa mauaji hayo.

Umbali kutoka shuleni na makazi yao huwa kikwazo kwao kutembea umbali mrefu kuzifuata shule ziliko. Dhana hiyo inathibitishwa na Mwanachama wa  shirika la HakiElimu, Profesa Suleman Sumra katika andiko lake alilolitoa kwenye Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambapo anasema;

“Kama ilivyokuwa siku za nyuma, wazazi wengi huwaona watoto hao bado wadogo na hivyo kuweka kipaumbele katika kuwaandikisha shule wenye umri mkubwa kwanza. Baadhi ya sehemu, mathalan, umbali wa ilipo shule kulinganisha na makazi ni mkubwa mno kuliko uwezo wa mtoto wa miaka saba kutembea”.

Ripoti ya HakiElimu (2008) juu ya Hali ya na Upatikanaji wa Elimu kwa watoto wenye Ulemavu Tanzania inaeleza kuwa ubaguzi na uelewa mdogo wa mambo yanayowahusu watoto wenye ulemavu imekuwa sababu pia ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kutokuwepo shuleni,

“ Uelewa mdogo na kutothamini mambo yanayowahusu watu wenye ulemavu miongoni mwa mwalimu, viongozi wa shule na jamii kwa ujumla. Mambo yote haya yana madhara pindi linapokuja suala la kutambua na kuthamini mahitaji ya watoto wenye ulemavu” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya HakiElimu na kufafanua zaidi,

“Pengine kikwazo zaidi cha elimu kwa watoto wenye ulemavu ambacho kinaweza kujumuisha vikwazo vyote ni kwamba hakuna juhudi za makusudi zilizochukuliwa kuondoa vikwazo hivi. Kushindwa kutoa fursa za kielimu kwa watoto wenye ulemavu ni kudidimiza malengo ya MMEM

Nini Kifanyike kuinua elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi

Akihojiwa na vyombo vya habari hivi karibuni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu  anayehusika na walemavu, Jenista Mhagama amesema kwa sasa serikali imezindua mikakati na kampeni kuhakikisha wenye ulemavu wa ngozi wanalindwa na juhudi zilizofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani zimeweza kupunguza mauaji ukifananisha na miaka iliyopita.

Shirika la Under The Same Sun (UTSS) ambalo linapigania haki za watu wenye ulemavu wa ngozi hapa nchini, chini ya Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji, Peter Ash, linaeleza kuwa kazi kubwa wanayofanya kuinua elimu ya watu wenye ulemavu ni kuwaweka katika shule zenye hosteli ambapo huko wanalindwa, wanajumuika na wanafunzi wengine na kupewa vifaa kulingana na mahitaji yao ili kufika hatua zote za elimu.

Ripoti hiyo ya Hakielimu (2008) inashauri kutoa elimu kwa jamii pamoja na kuongeza uhamasishaji juu ya umuhimu na katima ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu nchi nzima.

“Uhamasishaji huu uendane na uboreshaji wa mahitaji ya kiuchumi kwa watoto wenye ulemavu pamoja na wale wenye mahitaji maalumu”.

 

 

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *