Mpwapwa: Ushauri wa DC ulivyowakuna wananchi

Kulwa Magwa

BAADHI ya wakazi wa kata ya Lumuma, wilaya ya Mpwapwa, wameunga mkono na kupongeza ushauri waliopewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Kangoye, kuhusu soko la vitunguu.

Hivi karibuni, mkuu huyo wa wilaya akiwa ziarani katika vijiji vya Lufusi, Kitati na Mafwene aliwashauri wananchi kuacha kuuza vitunguu mapema, bali wawe na utamaduni wa kusubiri bei ya soko inapopanda ili iwaongezee kipato.

Kangoye alitoa ushauri huo kutokana na wakulima wengi kukimbilia kuuza vitunguu mapema kwa bei ya chini, ambapo baada ya muda huanza kuhangaika kuendesha maisha yao.

Christopher_Kangoye

MKUU wa wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye

Wakulima hao walisema, tangu walipovuna vitunguu vyao mwezi Agosti, mwaka jana, waliamua kuvitunza kwenye vichanja vya waziwakisubiri ongezeko la bei la Januari, Februari na Machi mwaka huu.

“Wakati mkuu wa wilaya akituhutubia, tulianza kufikiria itakuwa itakuwa haina maana kuingiliwa katika mambo yetu binafsi, lakini sasa nadhani nitafanya mambo makubwa maana bei ya imepanda na kufikia sh. 90,000 kwa gunia.

mpunga-mpwapwa

Hivi sasa kilimo cha mpunga kinaendelea kufanyika katika bonde la mto Lumuma

“Ningeuza wakati ule, ningeambulia sh. 35,000 ambazo zingeishia kwenye matumizi machache ya nyumbani, “ alisema Kamilius Ngolelwai, mkazi wa Mafwene.

Naye Damas Kazi, mkazi wa Lufusi, alisema vitunguu alivyotunza anakusudia kuviuza wakati wowote kwa bei isiyopungua 100,000 maana ana uhakika siku chache zijazo vitapanda.

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Lufusi, Jonas Mbogo, alisema watu walipohamasishwa na mkuu wa wilaya kujifunga mikanda kwa kutouza ovyo vitunguu vyao, walidhani serikali haikuwa na lengo zuri dhidi yao, lakini wengi hivi sasa wanapongeza ushauri huo.

Mbogo alisema waliouza mapema vitunguu vyao wamekuwa wakijilaumu baada ya kuwaona waliovumilia wanaendelea ‘kuvuna’ fedha nyingi.  

Banio

Banio mojawapo linalotumika kusafirisha maji kwa wakulima wa mto Lumuma, wilayani Mpwapwa

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Lumuma, Joklan Cheliga, alipongeza ushauri wa DC na kuwataka wapiga kura wake waendelee kuutumia katika misimu mingine ya kilimo ili wanufaike na jasho lao.

“Katika suala hili mkuu wa wilaya amenisaidia hata mimi, maana naweza kukaa na watu wangu tukapanga mipango ya maendeleo kwa kuwa tuna fedha zilizotokana na jasho letu, “alisema Cheliga.

Akizungumzia suala hilo, Kangoye, alisema ataendelea kuwahamasisha wananchi kutumia rasilimali na fursa walizo nazo kujiletea maaendeleo.

Alisema wakati mwingine umasikini ni wa kujitakia, ikizingatiwa kwamba kata ya Lumuma ina mto unaotumika kwa kilimo, lakini baadhi ya watu hawautumii ipasavyo kuwaletea maendeleo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *