TRAUMA: kidonda cha kisaikolojia kinachohatarisha maisha ya watu wengi

Jamii Africa

Tunaishi katika dunia ambayo inakabiliwa na matatizo mbalimbali ambayo husababishwa na shughuli za binadamu na nguvu za asili kama mafuriko, vimbunga, matetemeko chini ya ardhi ambayo huwa nje ya uwezo wetu.

Matatizo hayo kwa nyakati tofauti yamesababisha madhara kwa wananchi ikiwemo ulemavu na wengine kupoteza maisha. Lakini matukio hayo huacha vidonda na makovu ya kisaikolojia kwa watu walioshuhudia na ikiwa wataendelea kuyaona matukio mabaya katika maisha yao kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata majeraha mengi ya kihisia.

Hali hiyo inatambulika kama kiwewe au kwa jina la kitaalamu ‘TRAUMA’.   Ili nieleweke vizuri nitatumia neno Trauma, twende pamoja katika makala hii ili tuchimbe kwa undani juu ya dhana hii ambayo imekuwa ikiwaletea watu wengi shida, lakini pia tutafahamu tiba yake.

TRAUMA ni nini?

Trauma au kiwewe ni  muitikio wa kihisia ambao hutokea kwa mtu baada ya kushuhudia tukio baya katika maisha yake. Matukio hayo ambayo yanatajwa kuwa ni trauma hutofautiana kutoka yale ya kawaida kama kupewa talaka, kuumwa, ajali,  kufiwa na ndugu wa karibu mpaka matukio ya kushtusha  ya vita, kubakwa, mateso, maumivu makali na mauaji ya  halaiki (kimbari).

Matukio hayo humletea mtu aliyeshuhudia hisia za hofu, mashaka, wasiwasi, kujitenga, kilio na mshtuko na mwingine kuogopa kuwaona watu fulani au kutembelea maeneo ambayo matukio hayo yametokea.

Vita huleta hofu na maangaiko

Chama Cha Tiba ya Magonjwa ya Akili cha Marekani (PTSD) kinaelezea Trauma kuwa ni hali ambayo humkuta mtu baada kupitia au kushuhudia tukio au matukio ambayo yalihusisha au kutishia kifo, majeraha makubwa ambayo yalimletea madhara mwenyewe au wenzake na wakati mwingine yanajenga hofu, kukosa msaada na vitisho.

Tatizo hili la kisaikolojia linafafanuliwa kwa kina na Mtaalamu wa Saikolojia wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Zainabu Rashidi ambaye anasema mtu akishuhudia tukio baya kama ajali na vita taarifa zake hutunzwa katika ubongo.  Picha za matukio hayo hujirudia kwa mtu na kutengeneza kidonda cha kisaikolojia ambacho kisipotibiwa kinaweza kusababisha matatizo ya akili hata kifo.

“Baadhi ya matukio tunatunza katika ubongo halafu yanakuja tena” anasema na kuongeza kuwa “ Trauma ni kidonda cha kisaikolojia ambacho ni matokeo ya kuumia kihisia”

Anasema dada mmoja miaka kadhaa iliyopita alibakwa na bosi wake ambaye wakati anambaka alikuwa amevaa suti nyeusi. Kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji kingono, dada huyo aliathirika kisaikolojia na  kila alipomuona mtu aliyevaa nguo nyeusi hukumbuka tukio alilofanyiwa na huingiwa na hofu ya kubakwa tena.

Anaeleza kuwa hisia hizo zinamfanya mtu kuwa na muitikio wa matendo fulani ikiwemo hofu na woga wa kutembelea eneo ambako tukio limetokea. Uoga huo humfanya mtu kushindwa kufanya jambo fulani, Mfano mtu mwingine anaweza kuogopa kupanda ngazi za ghorofa kwa hofu ya kuanguka, mwingine akiguswa tu na mdudu anaruka na kuingiwa na hofu.

Hali hiyo ya kisaikolojia hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa sababu sio watu wote wanashtushwa na matukio mabaya, wengine huona ni sawa tu lakini wengine huumizwa na kupata msongo wa mawazo. Tofauti hiyo ni matokeo ya malezi katika jamii zetu ambazo zina mitazamo na matukio tofauti ambayo hujenga taswira tofauti kwa watu wake.

“Tunatoka jamii tofauti zenye mitazamo tofauti, Mfano mama mwingine akipigwa na baba haumii kwasababu kwao wanawake kupigwa ni kawaida lakini mwingine itamuumiza sana” anaeleza Zainabu Rashidi.

Anasema kidonda hicho cha kihisia kikipona huacha kovu ambalo hudumu katika ubongo wa binadamu na likitokea tukio lingine baya huweza kuamsha hisia na kumkumbusha mtu matukio mabaya yaliyopita ambapo humjengea mtu mfadhaiko na msongo wa mawazo, “Trauma ina jenga kovu ambalo matukio mengine yakitokea mtu hukumbuka matukio yaliyopita na kumuumiza”.

Hata hivyo Trauma hutofautina katika muda wa kudumu ambapo kwa wengine hukaa muda mfupi na kutoweka lakini kwa watu wengine hukaa muda mrefu kabla hali hiyo haijatokea na kuleta madhara kama hatua stahiki hazitachukuliwa.

Mary Mtuka mkazi  wa Tabata  Dar es salaam, anasema wakati mwingine akiwa amelala kitandani usiku , hupata hali fulani ya mshtuko, ghafla huamka na kupiga kelele na kulia kwa sauti kwasababu matukio mabaya aliyoyaona wakati wa mchana humrudia wakati wa usiku na kumletea hofu.

“ Wakati mwingine nikiwa nimelala naamka na kuanza kupiga kelele na kulia kwa muda mrefu kisha nalala tena, lakini nikiamka asubuhi sikumbuki chochote” anasema Mary ambaye ameshuhudia matukio mengi ya kikatili katika jamii yake.

Dalili za Mtu mwenye Trauma

Ziko dalili mbalimbali ambazo huambatana na mtu aliyepata trauma kwasababu hali hii hujitokeza kwa namna mbalimbali ambazo humkuta mtu aliyeshuhudia matukio mabaya.

Mambo yafuatayo hudhihirisha kuwa mtu ana Trauma:

  • Kukosa Usingizi

Tatizo la kukosa isingizi (Insomnia) ni dalili mojawapo ya mtu mwenye trauma ambapo mtu hukosa usingizi kabisa na kulazimika kukaa kitandani akiyakumbuka matukio mabaya yaliyotokea.

  • Wasiwasi na hofu

Hofu ambayo hutengenezwa na mazingira yanayomzunguka mtu na kumfanya asitulie,  kukosa kujiamini na kuhofia usalama wake. Hofu hiyo humzuia mtu kufanya baadhi ya mambo, mfano kuogopa kupanda ngazi za ghorofa kwa kuhofia kuanguka na mwingine anaogopa kukaa pekee yake.

Hofu, mashaka na kujitenga humwandama mtu mwenye trauma

  • Umakini hupungua

Hali hii humfanya mtu kushindwa kutimiza majukumu yake kama inavyotakiwa na kukamilisha kazi kwa wakati kwasababu akili yake inakuwa haiko sawa. Mfano mtu anaweza kuanza kufanya kazi fulani lakini anajikuta anatumia muda mrefu kuimaliza.

  • Kukosa Usikivu

Hii hutokea zaidi wakati wa mazungumzo ambapo unaweza ukawa unaongea na mtu anaitikia lakini ukimuuliza mmeongea nini hakumbuki chochote. Mtu anakuwepo eneo husika lakini akili yake iko mbali ikiwaza juu ya tukio lilitokea na madhara yake.

  • Hasira na Ukali

Jambo dogo tu lisipoenda vizuri au muhusika akitofautiana na mwenzake hupata hasira na kufanya maamuzi magumu yaliyo nje ya uwezo wake. Hasira hizi huambatana na kutoa maneno makali bila sababu ya msingi.

Mtaalamu wa Saikolojia, Zainabu Rashidi anasema ukali hujidhihirisha kwa wanawake wenye umri wa miaka 45 na kuendelea  ambao wamefikia kikomo cha kuona siku zao (Menopause) ambapo hukumbwa na hasira na kuwa wakali kwa wenza na watoto wao.

Anasema  hali hiyo huwatokea wanawake hao kwasababu wengi wao wanakuwa tayari wamepitia vitendo vya ukatili wa kijinsia wakiwa katika umri wa miaka 20 na 30. Vitendo hivyo huacha kovu la kisaikolojia na wakipata maudhi hukasirika kwa haraka na hata kuwapiga watoto wao.

  • Kupata Mshtuko

Ubongo hutunza kumbukumbu zote katika akili zetu hivyo ni vigumu kusahau matukio tuliyoyaona wakati uliopita. Picha za matukio hayo hujirudia na hapo ndipo utamkuta mtu ametulia lakini ghafla hushtuka na kuingiwa na hofu.  Hali hii huja kama jinamizi ambalo humfuatilia mtu na kumfanya kuwa mwenye mashaka na kushtuka mara kwa mara.

  • Kujitenga

Kutokana na msongo wa mawazo, dalili ya kujitenga huonekana kwa mtu ambapo hutafuta mazingira ya kukaa pekee yake na hataki kuongea na watu wengine. Picha za matukio mabaya aliyoyaona humjengea hali ya kujitenga na kumfanya awaze kilichotokea.

 

Ungana nami katika makala ijayo ambayo itajikita kuelezea hali ya trauma duniani, kundi la watu walio katika hatari ya kupata trauma, madhara yake na tiba inayoambatana na tatizo la trauma.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *