Igunga: Chadema, CCM na CUF washinda kwa hoja au tuhuma?

Jamii Africa

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CDM) kinaonekana kuwa ni mzigo mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi huko Igunga kiasi kwamba madai mbalimbali yanayoelekezwa dhidi yake kuanza kuonekana ni ya vichekesho na kejeli. Tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa na kuhusishwa na CDM huko Igunga zimeanza kuvuka mipaka na kuanza kuonekana kama baadhi ya mbinu chafu za uchaguzi.

Hata hivyo CCM nayo inaonekana kuwa ni tishio kwa matamanio ya CDM ambapo chama hicho kikongwe         kikitumia nguvu zake zote kuhakikisha kuwa jimbo la Igunga haliangukii mikononi mwa upinzani. Hivyo, wana mikakati wake kama wale wa CDM wanashambulia kotekote katika kukionesha kuwa CDM ni chama cha vurugu  na udini. Vyama hivyo vimebanana katika kushindana nani kati yao anaweza kuja na tuhuma za kutisha zaidi.

Kumwagiwa tindikali

Tuhuma za kwanza kali ambazo CDM ilihusishwa nazo ni tukio la kijana mmoja ambaye anadaiwa kuwa ni mwana CCM kumwagiwa kile kinachodhaniwa kuwa ni tindikali ambayo ilimuunguza vibaya usoni na baadhi ya sehemu za mwili. Kijana huyo Musa Tesha (24) inadaiwa alimwagiwa tindikali hiyo akiwa katika juhudi za kubandika mabango ya mgombea wa CCM. Mara moja madai yakaanza kutolewa kuwa wahusika wa tukio hilo ni CDM.

Hata hivyo madai hayo yalipuuzwa na uongozi wa CDM huku kukiwepo tuhuma kuwa watu waliofanya vitendo hivyo hawahusiani hata kidogo na CDM na hadi hivi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kwa tukio hilo licha ya kwamba baadhi ya viongozi wa CCM walidai kuwa Tesha aliwataja kwa majina wahusika wa tukio hilo.

CDM kupeleka “maghaidi” Igunga

Gazeti la Chama cha Mapinduzi la Uhuru likiandika kwenye kurasa zake Septemba 14 lilikuja na madai mazito ambayo yamerudiwa tena na Katibu Mkuu wa Chama hicho kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimepeleka kundi la maghaidi huko Igunga ili kuharibu kura. “kuna kikundi cha kigaidi kimepelekwa Igunga na CHADEMA, kwa lengo la kuwatisha wanawake na wazee wasijitokeze kupiga kura.  Pamoja na kutumia kikundi cha kigaidi ambacho kina vijana 800, CHADEMA pia imeandaa mkakati wa kutengeneza shahada bandia za kupigia kura mkoani Arusha ili zitumiwe na kikundi hicho na vijana wengine wa kihuni. Kwa sasa kikundi hicho kinamwinda mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni za CCM mjini hapa, ili amwagiwe tindikali kama alivyofanyiwa kada wa CCM, Mussa Tesha (24).” Liliandika gazeti hilo.

Hata hivyo madai hayo ambayo ni mazito yanadhalilisha zaidi vyombo vya usalama nchini ambavyo vyote vinasimamiwa na serikali ya Chama cha Mapinduzi. Madai ya kuwa kuna watu wamepata mafunzo ya kighaidi uko Afghanistan au Libya na wakaweza kuingizwa nchini bila kukamatwa (japo wanajulikana) yanatishia zaidi usalama na yanaweza kutumiwa kuonesha jinsi serikali ilivyo dhaifu. Baadhi ya watu walioandika kwenye mitandao mbalimbali wameshangazwa na madai hayo kwani yanadhihirisha kuwa vyombo vyetu vya usalama (polisi, usalama wa taifa, jeshi n.k) ni legelege na dhaifu.

Mmoja wa wachangiaji kwenye mtandao wa JamiiForums ameandika kuwa “Haya ya kutishia watu kwa mgongo wa CHADEMA mara makomandoo,mara magaidi hayana tofauti kubwa na zile propaganda za mwaka jana za Shimbo!.Na inasadikika vile vitisho ni moja ya sababu ya watu wachache kujitokeza kupiga kura,kwa hiyo CHADEMA inabidi wajitahidi kuwapiga dozi ya kudumu(elimu),ili hawa jamaa wasiweze kuwayumbisha wana Igunga katika maamuzi yao,maana CCM wamekata tamaa,wako desparate kuja na upuuzi wowote katika kipindi kilichobaki-Akili zao ziko likizo”

Kubakwa kwa binti ya Kada wa CCM

Mara baada ya tukio la kumwagiwa tindikali tukio jingine likatokea Igunga ambalo nalo kwa sababu zisizoeleweka likahusishwa na CDM badala ya kuchukuliwa kama tukio la kihalifu. Gazeti la Mwananchi liliripoti kuwa “Kada wa CCM, Francisco Msalika amejeruhiwa kwa panga kichwani na binti yake kubakwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake Mtaa wa Benki ya zamani mjini Igunga na watu ambao walimtaka atoe pesa za kampeni. Akizungumza akiwa kitandani katika wodi ya majeruhi katika hospitali hiyo, kada huyo alisema tukio hilo lilitokea juzi kuamkia jana majira ya saa nane za usiku. Alisema alisikia kishindo ambacho kiliuvunja mlango wake wa chumbani na kisha watu hao kummulika kwa tochi kali usoni.”

Hata hivyo tukio hilo linaendelea kuchunguzwa na Jeshi la Polisi. Baadhi ya wanasiasa walianza kulitumia tukio hilo na kuanza kuwaita CDM “wabakaji” kwani binti ya kada huyo ilidaiwa kuwa amebakwa katika tukio la uvamizi huo.

Tukio la kuchomwa banda la kuku

Lakini tukio jingine ambalo limeacha vinywa vya watu wazi ni lile la kuungua kwa banda la kuku la Katibu wa CCM Kata ya Nyandekwa huko Igunga. Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii ambapo inadaiwa watu wasiojulikana walitia kibiriti banda hilo la kuku na taarifa hiyo kuripotiwa na gazeti la Mwananchi la Jumatano. Gazeti hilo liliandika kuwa “MATUKIO ya hujuma yanazidi kulitikisa Jimbo la Igunga safari hii watu wasiojulikana wamechoma moto nyumba ya Katibu wa CCM, Kata ya Nyandekwa usiku wa kuamkia juzi.Tukio hilo linahusishwa na wafuasi wa Chadema kutokana na ujumbe wa maandishi uliokutwa umechomekwa katika nyumba hiyo ukisomeka: “Chadema sisi ni wajanja”.Katibu huyo, Hamis Makala alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliyemtembelea jana kumpa pole kuwa, kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na wafuasi hao wa Chadema.”

Na kuongeza kuwa “Alidai kuwa sababu ya kuwindwa na wafuasi hao inatokana na kukasirishwa na kampeni anazozifanya katika kata hiyo zinazoifanya CCM ikubalike kwa wananchi na kukiacha Chadema kikikosa watu kinapokwenda kufanya mikutano ya hadhara. Nyumba iliyoteketezwa kwa moto ilikuwa ikitumiwa na katibu huyo kwa shughuli za jiko na kuhifadhia kuku.” Kada huyo wa CCM alielezea kuwa “Niliposhtuka na kutoka nje nilikuta moto mkubwa unawaka nikapiga yowe kuomba msaada. Lakini majirani walishindwa kuuzima kwa kuwa ulikuwa umesambaa… kuku 15 kati ya 21 waliokuwamo ndani wamekufa”

Baada ya moto kuzimika kwa mujibu wa gazeti hilo Katibu huyo alirudi kwenda kulala na kesho yake alipoamka ndio walikuta hiyo karatasi inayodai kuwa imesema “Chadema sisi wajanja”. Hata hivyo imeshindwa kuelekeweka karatasi hiyo iliwezaje kunusurika moto huo au upepo hadi kesho yake asubuhi ambapo ilikuwa ikingojea kuchukuliwa kama ushahidi.Lakini cha

kushangaza zaidi ni kuwa baadhi ya viongozi wa CCM akiwemo Katibu Mkuu Bw. Wilson Mukama walijitokeza tena kutoa pole na kuilaumu Chadema kwa tukio hilo. Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa bw. Mukama amelaani tukio hiyo kwa kusema kuwa  “Ni lazima lilaaniwe kwa sababu halitoi taswira na maana halisi ya kuwa na vyama vingi ambavyo vinapaswa kushindana kwa ubora na sera… hatushindani kwa vitisho, uhuni na hata kumwagiana tindikali”

Hata hivyo kwa mara nyingine tena CDM imelazimika kukana kuhusika na tukio hilo. Kiongozi wa Kampeni ya CDM huko Igunga Bw. Benson Kijaila amepuuzia matukio hayo akisema kuwa “Matukio haya wanayapanga wao wenyewe halafu wanasingizia vijana wetu… kama ni kuchoma hiyo nyumba wameichoma wenyewe ni mpango wao huo”

Chadema nayo yaituhumu CCM

Pamoja na kuwa CCM imekuwa ikituhumu CDM kwa kuleta vurugu huko Igunga au kujihusisha na matukio ya kihalifu CDM haijawa pembeni katika kurusha tuhuma mbalimbali dhidi ya CCM ikiwemo madai ya kuandaliwa kwa kundi la vijana katika kile ambacho kinadaiwa kuwa ni “kambi za kighaidi”. Madai hayo yametolewa na kurushwa na mtandao wa TV wa CHADEMA ambao unamwonyesha mmoja wa vijana ambao wanadaiwa kupatiwa mafunzo mbalimbali ya kuvuruga uchaguzi.  Pia CDM ilituhumu CCM kuwa iliingiza vijana zaidi ya 20 kutoka Tarime kwa ajili ya kuwatisha watu mbalimbali kupiga kura.

Ni wazi kuwa kwa kadiri kampeni ya uchaguzi Igunga inavyoendelea ndivyo tuhuma mbalimbali ambazo zina lengo la kusababisha hofu ya kisaikolojia kwa wapiga kura zitazidi kutolewa. Watu wengi wameanza kuhusisha kampeni hii ya hofu na vitisho na mbinu ambazo zilitumika wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana ambapo kauli mbalimbali za umwagikaji damu, na vurugu zilitumiwa kuwatisha watu kujitokeza kupiga kura.

Ni wazi kuwa matokeo ya uchaguzi ya Igunga yatategemea sana ni nani anaaminika katika hizi tuhuma mbalimbali na ni kwa kiasi gani uzito wa tuhuma hizi umeathiri fikra za wapiga kura. Kama watu wengi watahofia kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi kwa sababu ya “hofu” ni wazi kwamba wale watakaojitokeza watakuwa wale ambao wanajisikia salama, ni wanaume na vijana kuliko wanawake  wengi na wazee. Vyama vya siasa Igunga na hasa CCM na CDM vinakabiliwa na jaribio kubwa la kuweza kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Hata hivyo jukumu hilo inaonekana ni gumu sana kwani karibu vyombo vyote vya usalama vimekaa katika hali ya kusubiri matukio yatokee ili waanze uchunguzi na uwezo wao wa kuzuia matukio kabla hayajatokea unaonekana ni mdogo na hivyo vyombo hivyo  kwa namna moja kuonekana ni sehemu ya tatizo la usalama huko Igunga.

Ni wazi kwamba kama vyombo vya inteligensia na usimamizi wa sheria vitashindwa kuzuia matukio kabla ya kutokea basi matukio ya uhalifu kwa jina la “kampeni za uchaguzi” yataendelea kutokea na hivyo kuharibu kabisa maana ya dhana ya chaguzi “huru na ya haki”

 

Masaa machache yajayo yataamua nani atakayeshinda.

Mwandishi Wetu

4 Comments
  • Demokrasi ya Afrika kwa ujumla ni yakuletewa,na baada ya uhuru kuingia kwenye Demokrasi,ni shinikizo nchi za magharibi walituwetea,hii ndiyo maana fikra zetu ni kudhani ktk chaguzi za kisiasa utaona hofu na vitisho na umwagikaji damu,uhuni,shutuma za uwongo,visasi,chuki n.k.Ni marachache kwa nchi zinazo jiita zilizo leta demokrasia kama Marekani,Uingereza n.k kufanya mambo kama hayo kwani tayari fikra za watu zilijengwa vizuri ktk maana kamili ya demokrasia hivyo umasikini fikra&waakili ktk demokrasia ni mdogo mno.Sisi tumekurupukia tu demokrasia inahitaji kujipanga ki fikra.

    Hawa CCM wanatumia njia ya “utekaji wa fikra”na “propaganda feki”ku rubuni akili za watu Igunga.kwa hivyo na vyama vingine lazima navyo vipigane kwa fikra,ambapo unakuja kupata “vita vya kifikra ktk demokrasia” Huwezi pigana vita vya chini ardhini wakati adui anapigana vita vya angani.

    Natoa wito wana Igunga chama kinachofanya demokrasia ya kweli na kinacho tetea haki,ukweli,usawa na uwazi.

    Inawezekana fikra za watu kuiamini kidogo ccm kwa aajili ya kupata ulinzi kipindi hiki hadi siku ya kura kwani fikra za wengi nikuwa askari,jeshi ni vyombo vya ccm,lakini ukweli askari na jeshi wameichoka hiyo ccm na wengi c ccm toka na hali mbaya ya maisha inayo tokana na uongozi wa serikali chini ya chama hicho tawala.

  • Demokrasia nchi za Afrika ni yakuletewa na kushinikizwa na nchi za magharibi mbaya zaidi hatukuandaliwa kuitambua kiundani,ndiyo maana tunaendekeza siasa za chuki,uwongo,vurugu,majungu,visasi,kutokuwa na umoja n.k
    Demo=Demos=MAPEPO
    Cracy=Utawala
    Hivi democracy ni utawala wa mapepo.

  • igunga mbona balaa kila chama kinalaumu mwenzake .Hapo ndo siasa mchwra za bongo .Tuwe makini na siasa za igunga

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *