Nchini Tanzania msichana wa shule ya msingi na sekondari akipata mimba ndio inakuwa mwisho wa masomo yake. Anafukuzwa shule na haruhusiwi kuendelea na masomo hata baada ya kujifungua.
Awali serikali ya awamu ya nne chini ya rais mstaafu Jakaya Kikwete, ilianzisha programu ya kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike waliopata mimba ili kuhakikisha wanatimiza ndoto zao za kielimu.
Rais John Magufuli alipoingia madarakani alitoa agizo la kuwafukuza na kutokuwaruhusu wanafunzi wa kike waliopata mimba kurudi shuleni akidai kuwa hawezi kusomesha watu ambao wameamua kuwa wazazi kabla ya muda wao. Agizo la rais liliibua mjadala mpana wa kitaifa ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu kumekuwepo harakati za kumkomboa mwanamke dhidi ya mfumo kandamizi ili kujenga jamii inayoheshimu usawa wa kijinsia.
Pia serikali kupitia baadhi ya Wakuu wa Wilaya inawakamata wasichana waliopata mimba na kuwafikisha mahakamani ili wawataje wanaume waliowapa mimba. Wanaharakati wa haki za binadamu wanatofautiana na adhabu zinazotolewa na serikali kuwa sio njia sahihi ya kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike nchini.
Licha ya Tanzania kutoa adhabu kubwa kwa wanafunzi waliopata mimba, nchi jirani ya Kenya inaendesha na program ya kuwasaidia wasichana hao ambapo huendelea na masomo na baada ya kujifungua wamewekewa utaratibu wa kupata matunzo ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao.
Inaelezwa kuwa adhabu inayotolewa na serikali ya Tanzania haijasaidia kupunguza tatizo la mimba. Kulingana na takwimu za serikali idadi ya wasichana wanaopata mimba walio na umri kati ya miaka 15-19 imeendelea kuongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi 27% mwaka 2015. Nchini Kenya hakujashuhudiwa ongezeko hilo ambapo kiwango cha mimba za utotoni ni asilimia 18 kwa miaka 5 iliyopita.
Watetezi wa haki za binadamu wamelaani hatua ya Tanzania kuwakamata wasichana waliopata mimba ambapo wanadai kuwa wasichana wamekuwa waathirika wa udhalilishaji wa kingono kutoka kwa walimu na watu wengine katika jamii na wanatakiwa wasaidiwe na kulindwa ili kufikia ndoto zao.
Ripoti ya utafiti wa taasisi ya Third World Quarterly imebaini kuwa tatizo la mimba za utotoni nchini Tanzania haliwezi likamalizwa kwa tabia mbaya au adhabu kwasababu suala hilo lina uhusiano wa moja kwa moja na umaskini na mabadiliko ya kimwili ikiwemo hisia za kimapenzi.
Mtafiti Kate Pincock anaeleza kuwa wasichana wanashawishika kuanza kufanya ngono katika umri mdogo si kwasababu ya tamaa za kimwili bali vikwazo zilivyowekwa mbele yao ili kupata elimu bora ikiwemo umaskini, walimu wa kiume, mtazamo wa jamii.
Mtazamo wa jamii ni kuwa wasichana wamejijengea tabia mbaya ya kujirahisha kwa wanaume ili kutimiza tamaa za kimwili ambazo huchochewa na makundi rika na mabadiliko ya sayansi ya teknolojia na sayansi. Lakini dhana hii haina nguvu kwasababu tabia za binadamu hujengwa na jamii yenyewe.
Suala la kwenda shuleni nchini Tanzania na maeneo mengine ya dunia linachukuliwa kama njia sahihi ya kutengeneza mstakabali mzuri wa baadaye. Lakini changamoto za kupata mahitaji ya shule ikiwemo vitabu, fedha ya chakula zinawalazimisha wasichana kufanya ngono ili kupata fedha ya kujikimu; mazingira duni ya shule huchochea zaidi tatizo hilo linakuwa kubwa zaidi kutokana na mazingira magumu ya kusomea katika shule mbalimbali nchini.
Baadhi ya walimu wa kiume huwataka wasichana kimapenzi kwa nia ya kuwapa madaraja mazuri katika masomo; msichana akikataa hufelishwa. tabia hii ya walimu wa kiume ni kikwazo kingine cha kumaliza tatizo la mimba za utotoni nchini.
Mwaka 2016, walimu nane wa shule ya sekondari Mihama, kata ya Kitangili, Wilaya ya Ilemela walisimamishwa kazi, watano kati yao walishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi wa kike.
Nje ya shule, wanakutana na wanaume wengine ambao huwarubuni kwa fedha na vitu. Changamoto inayojitokeza ni kukosa elimu ya uzazi wa mpango kuwawezesha kuzuia mimba wakati wa kufanya mapenzi, lakini njia hii imekuwa ikipingwa kwasababu inachochea wasichana kuingia kwenye mahusiano mapema. Hata jamii haiongelei kwa uwazi masuala ya uzazi wa mapango kwa watoto wao.
Tanzania inapaswa kujithmini juu ya hatua iliyochukua ya kuwaadhibu wasichana wanaopata mimba wakiwa shuleni na kujikita kushughulikia mizizi ya tatizo kuliko matokeo. Kuelimika ni haki ya kila mtu pasipo kujali hali aliyonayo.