Ahadi ya Waziri Mkuu haijaleta matumaini Katavi, upatikanaji wa dawa bado changamoto kubwa

Jamii Africa

MATARAJIO ya upataikanaji wa uhakika wa dawa katika Hospitali ya Manispaa Mpanda mkoani Katavi ambayo walikuwa nayo wakazi wa mkoa huo yameendelea kuota mbawa licha ya ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, takriban miezi miwili iliyopita, FikraPevu inaripoti.

Hospitali hiyo, ambayo ndiyo hutumiwa kama Hospitali ya Mkoa wa Katavi, imekuwa na uhaba wa dawa muda mrefu licha ya kufunguliwa kwa duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) mjini Mpanda.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa pamoja na ahadi hiyo ya Waziri Mkuu na Mkurugenzi wa MSD tatizo la upungufu wa dawa bado liko vile vile na hakuna nafuu yoyote.

Said Juma, mkazi wa Mtaa wa Kawajense, alisema kwamba, walitarajiwa baada ya ufunguzi wa duka hilo dawa zingeweza kupatikana kwa uhakika na wakati wote, lakini hali bado ni mbaya kwenye hospitali hiyo ambapo wagonjwa mara nyingi huandikiwa vyeti na kutakiwa kwenda kutafuta dawa kwingineko.

“Wagonjwa wanalazimika kwenda kwenye maduka ya nje ya hospitali kutafuta dawa, kwani mara nyingi hata duka la MSD huwa halina dawa walizoandikiwa ambazo ni za msingi kabisa kustahili kupatikana hospitalini,” alisema.

FikraPevu imebaini kwamba, wakati wa usiku hali huwa mbaya zaidi kutokana na maduka ya dawa muhimu za binadamu kufungwa huku lile la MSD likiwa halina dawa husika.

Aidha, hata katika maduka ya dawa ya nje ya hospitali, mara nyingi dawa muhimu huwa hazipatikani, jambo linaloendelea kuwapa wakati mgumu wagonjwa mkoani humo.

“Wateja wetu wakubwa hapa ni wagonjwa ambao huwa wanahitaji kwenda kwenye maduka ya nje kutafuta dawa, lakini nyakati za usiku muda wa kufunga maduka hayo unapopita na wateja hupungua,” anasema Francis, mmoja wa wasafirishaji wa boda boda zinazoegeshwa hospitalini hapo.

Wakati akifungua duka hilo la dawa la MSD, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaeleza wakazi wa mkoa huo kwamba, changamoto iliyokuwa ikiwakabili sasa imepatiwa ufumbuzi wa kudumu na kwamba huduma zitapatikana kwa uhakika.

“Leo tumefungua duka hili, naamini ile changamoto ya ukosefu wa dawa kwenye hospitali hii itakuwa imepatiwa ufumbuzi na wananchi watapata huduma kwa uhakika,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema kufunguliwa kwa duka hilo kungetoa ufumbuzi wa tatizo sufu la upungufu wa dawa katika hospitali hiyo pamoja na vituo vya afya na zahanati mkoani Katavi, kwani wasingeweza tena kusubiri kwa muda mrefu kuletewa dawa kutoka Dar es Salaam.

“Serikali imeweka mkakati wa kufungua maduka ya dawa kupitia MSD katika kila mkoa hapa nchini ili kuondoa tatizo la vifaa tiba na dawa na kuwapunguzia wananchi gharama za ununuzi wa dawa,” alisema katika hotuba yake.

Naye Mkuruenzi Mkuu wa MSD, Laurent Bwanakunu, alisema lengo la kufungua maduka hayo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuhakikisha wanapata dawa zenye ubora kwa bei nafuu na kwa wakati.

FikraPevu inafahamu kwamba, Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa saba ambayo tayari MSD imekwishafungua mamduka ya dawa, mpango ambao unatakiwa kuendelea kwenye hospitali nyingine nchini.

Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwenye maduka hayo, hali ambayo inaleta ugumu wa Tanzania kufikia lengo namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Duniani (SDG) ifikapo mwaka 2030.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *