Albino Mwanza kugomea sherehe za miaka 50

Jamii Africa

CHAMA cha watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Mkoani Mwanza (TAS), kimeapa kutoshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kwa madai kwamba Serikali imeshindwa kukomesha mauaji ya walemavu hao.

Kadhalika, Chama hicho kimelaani kaulimbiu ya Serikali ya ‘Tumethubutu, Tumeweza na Tunazidi kusonga mbele’, na kimehoji sababu ya Serikali kuweka kaulimbiu hiyo wakati albino wanazidi kuuawa na kukosa uhuru wao ndani ya nchi yao.

Mwenyekiti wa chama hicho, mkoani Mwanza, Alfred Kapole ambaye pia ni mlemavu wa ngozi, ametoa msimamo huo leo Jijini hapa, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na msimamo wao huo.

Akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati Kuu Tendaji ya chama hicho, Kapole alisema, hawaoni sababu ya kushiriki maadhimisho hayo ya miaka 50 ya Uhuru, kwani hadi sasa bado wanaishi kwa hofu kubwa ya kuuawa, na hiyo inatokana na Serikali kuonekana kushindwa kudhibiti mauaji hayo.

“Hili ni tamko letu rasmi kwa Serikali kuhusu miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Sisi watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa Mwanza, hatutashiriki kamwe sherehe hizo hapo Desemba 9, 2011.

“Naomba hata Rais Kikwete atambue hivyo kwamba tumesusia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa nchi hii. Sisi tunaishi kwa kuwindwa kutaka kuuawa, hatuna uhuru ndani ya nchi yetu halafu tushiriki uhuru upi?”, alisema Kapole huku akionekana kujawa jazba.

Kuhusu kaulimbiu ya Serikali, mwenyekiti huyo wa Chama cha albino mkoani Mwanza, alihoji kwa kusema: “Eti Serikali inasema, Tumedhubutu, Tumeweza na Tunazidi kusonga mbele. Hivi wanasonga mbele na nani wakati sisi tunazidi kuuawa?. Usemi huu hatuutaki kuusikia kabisa”.

Kapole alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha Serikali yake inadhibiti kabisa wimbi la mauaji ya albino, na kwamba walemavu hao ni vema wakawekewa mazingira mazuri kwa usalama wa maisha yao.

“Historia ya nchi inaonesha wazi kwamba, kati ya miaka ya 1970 hadi 1980 hakukuwa na mauaji ya albino. Lakini kuanzia miaka ya 2000 hadi leo hii, albino wamekuwa wakiishi kama enzi ya mkoloni, na wengine kuuawa kama wanyama wa porini”, alisema.

Alisema, Serikali bado haijawatendea haki albino, kwani hata wale albino waliochukuliwa na kuhifadhiwa katika makambi maalum ya Mitindo Wilayani Misungwi Mwanza, Bukoba Kagera na Shinyanga, wanaishi kama wakimbizi kwa kupewa misaada ya chakula na malazi huku wakisubiri siku yao ya kufa.

Kapole alimpongeza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kuchukua watoto watatu albino kwa ajili ya kuwasomesha, na aliwataka viongozi wengine wa Serikali nchini, wakiwemo wabunge kuiga mfano huo.

Naye Padri Pascal Durand wa Parokia ya Kasamwa, Jimbo Katoliki la Geita, alisema: “Serikali inapaswa kuwasaidia wananchi wake ambao wameonekana kusahaulika, wakiwemo vikongwe wanaouawa kutokana na imani za kishirikina, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia”.

 

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

1 Comment
  • TAS mmefanya jambo zuri na lambolea”serikali ya ki freemanson kamwe haiwezi wasaidia kwa nia na dhati bali unafki na upambe kwani viongozi wengi tu wanahusishwa na ushirikina mbali na kuwa wafuasi wa shetani”leo hii wasipo toa damu kula yao imekwisha yani viongozi vipofu wa vipofu wasio na hofu ya MUNGU japo c wote ilakaribu wote ndivyo walivyo”POLENI SANA NDUGU ZANGU TUTAZIDI WAOMBEA ILI MWENYEZI MUNGU YEHOVA azidi shughulika na wadhalimu juu yetu sote”serikali yaki shetwani dawa yake ni maombi”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *