Arthritis: Maumivu ya viungo yaliyokosa tiba ya uhakika

Jamii Africa

Ipo dhana kuwa maumivu ya viungo vya mwili ni maradhi yanayowapata watu wenye umri mkubwa pekee. Lakini maumivu hayo yanaweza kumtokea mtu yoyote bila kujali umri.

Kitaalamu maradhi hayo hujulikana kama ‘Arthritis’ ambapo maungio kwenye magoti, mikono, kiuno hupatwa na maumivu, kukakamaa na kuvimba kwa ngozi ya sehemu husika na wakati mwingine kuwaka moto.

Maumivu hayo hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine kulingana na athari aliyopata. ‘Arthritis’ inajitokeza kwa namna mbalimbali kulingana na maumivu yalipojitokeza ikiwemo kukakamaa kwa magoti (osteoarthritis), kuwaka moto (bursitis), kuvunjika na kulegea kwa mifupa (osteoporosis) na kuvimba (rheumatoid arthritis.).

Tukianza na osteoarthritis inatokea wakati mfupa laini (cartilage) unaofunika na kulinda sehemu ya maungio kukauka. Kukauka kwa cartilage kunasababishwa na kupungua kwa majimaji yanayozuia msuguano wa mifupa. Wakati mwingine huchochewa na umri mkubwa au majeraha na matokeo yake mifupa inasigana na kuleta maumivu.

                                                                      

Osteoarthritis  mara nyingi huwapata watu walio na umri zaidi ya miaka 50 au wakimbiaji wa mbio ndefu, hii ni kulingana na taasisi ya Osteoarthritis Research Society International.

Rheumatoid arthritis ni jamii ya maumivu ya viungo ambayo huusisha kuvimba na kubadilika rangi kwa viungo zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja. Mikono, kiuno na magoti ndio huathirika zaidi. Huwapata watu wenye umri kati ya miaka 40 na 60.

Licha ya  arthritis kuhusishwa na umri, kuna sababu zingine hatarishi ambazo zina mahusiano ya karibu na maradhi hayo ikiwemo jinsia. Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha nchini Marekani kinaeleza kuwa asilimia 52 ya watu wazima wanaopatwa na arthritis ni wanawake. Wanawake wako katika hatari zaidi ya kupatwa na maradhi hayo kuliko wanaume.

Sababu nyingine ni uzito kupita kiasi. Watu wenye uzito kupita kiasi wako hatarini kupata maumivu kwenye maungio hasa magotini. Waatalamu wa afya wanaeleza kuwa miguu huelemewa na uzito wa mwili wakati wa kutembea ambapo mifupa husigana na ngozi kuvimba.

Pia baadhi ya kazi zinaweza kuwa kichocheo kwa mtu kupata maumivu hasa ya magotini.  Kwa kazi ambazo mtu anatumia muda mwingi kuinama, kuchuchumaa na kusimama, hii zaidi huwapata wafanyakazi wote wa viwandani na bustani.

Hata hivyo, hakuna jambo la kufanya litakalo kulinda dhidi ya arthritis kwa asilimia 100, japokuwa zipo hatua unazoweza kutumia kila siku kupunguza hatari ya kupata maumivu kwenye maungio.  Jiepushe na uzito uliopitiliza, kuvuta sigara na kula mlo kamili unaozingatia afya ya mwili.

Kama unapenda kufanya mazoezi, chagua vifaa vitakavyokukinga na majeraha. Hakikisha unatembea kwa uangalifu na ikitokea umepata jeraha kwenye maungio pata muda wa kumpuzika ili kurejea katika hali ya kawaida.

Isipokuwa daktari amekuambia vinginevyo, ni vizuri kufanya mazoezi hata kama una arthritis. Mazoezi yatasaidia kupunguza maumivu, kuongeza nguvu na viungo kuimarika. Zingatia aina ya zoezi unayofanya ili kujiweka katika tahadhari ya kiafya.

Dalili nyingine ambayo inaweza kumpata mtu ni kuchoka kusiko kwa kawaida ambako kunaambatana na maumivu yasiyo ya kawaida na wakati mwingine kupoteza fahamu. Ikitokea hali hiyo ni vema kumuona daktari.

Ili ujigundue haraka kuwa una arthritis ni kujitokeza kwa uvimbe wa duara kwenye vidole vya miguu, mikono na kiwiko cha mkono.

Bahati mbaya, hakuna dawa ya uhakika ya kutibu arthritis, lakini daktari akikutibu anakupa dawa ya kutuliza maumivu na kuvimba ili kupunguza athari na kukurejesha katika hali ya kawaida.

Ikiwa dawa hazijamaliza tatizo, mgonjwa anaweza kufanyiwa upasuaji hasa kwenye kiuno, nyonga au kubadilisha kisigino cha mguu. Hata hivyo, upasuaji sio njia sahihi kwasababu wataalamu wanasema hupunguza utendaji wa viungo husika baada ya upasuaji.

Ukiachilia mbali dawa na upasuaji, kuna matibabu mengine ambayo yanatuliza dalili za arthritis. Kulingana na tafiti mbalimbali inawezekana kupunguza maumivu ya viungo kwa kutumia tiba ya asili ya jamii ya China ijulikanayo kama ‘acupuncture’. Tiba hii huusisha kuingizwa kwa sindano maalum kwenye eneo lililoathirika ambapo hupunguza maumivu, kuimarisha mzunguko wa viungo na ubora wa maisha ya mgonjwa. 

Pia baadhi ya virutubisho vyenye mchanganyiko wa madini ya ‘Chondroitin sulfate’ vinaweza kutumika kutibu arthritis. Lakini kabla hujatumia kirutubisho chochote ni muhimu kumuona daktari ili kubaini ni aina gani ya tiba inayokufaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *