Imeelezwa kuwa kukosekana kwa mfumo mzuri wa uwajibikaji na uwazi katika taasisi za serikali kumesababisha matumizi mabaya ya rasilimali za umma kama ilivyoibuliwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza katika mjadala wa Asasi za kiraia jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Wajibu, Yona Killagane amesema ripoti ya CAG ya mwaka 2017 imeweka wazi maeneo mbalimbali ambayo serikali haijawajibika katika mapato na matumizi jambo ambalo haliashiria ustawi mzuri wa uchumi wa taifa.
Amesema uwajibikaji katika bajeti ya serikali umepungua kutokana na kutofanyiwa kazi mapendekezo ya CAG na kusababisha watendaji kurudia makosa yaleyale katika utengenezaji wa ripoti za mapato na matumizi.
“Utekelezaji wa mapendekezo ya CAG umeongezeka 2016/2017 kutoka asilimia 14 hadi asilimia 21 lakini ongezeko hilo ni dogo kuliko mapendekezo ambayo hayakufanyiwa kazi ambayo yanafikia asilimia 25,” amesema Killagane.
Ameeleza kuwa hata mapendekezo au ushauri unatolewa na Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) hayakufanyiwa kazi inavyotakiwa kwa mwaka 2017 na matokeo yake taasisi nyingi za serikali zimepata hati za mashaka na chafu kutokana na matumizi mabaya ya fedha,
“Utekelezaji wa mapendekezo ya POAC ni asilimia 6 na mapendekezo ya LAAC yako kwa 31%. Ili nchi ipige hatua kwenye sekta ya fedha tunahitaji kuwa na taasisi na kamati za bunge imara na zenye nguvu ya kuisimamia serikali,” amesema.
Amebainisha kuwa maeneo mengine ambako kuna uwajibikaji mdogo ni kwenye halmashauri za serikali za mitaa (LGAs) ikizingatiwa kuwa zilishindwa kukusanya mapato kulingana na maelekezo ya bajeti ya mwaka 2016/2017.
“Kwa mwaka 2016/2017, LGAs zilikusanya Tsh. 523.56 bilioni kutoka kwenye vyanzo vyake. Hii ni sawasawa na 83% ya bajeti iliyopitishwa ya sh. 628.05 bilioni. Hii inaonyesha kuwa uwezo wa LGAs kukusanya mapato ulishuka ukilinganisha na ukusanyaji wa 90% ya mwaka uliopita (2015/2016),” amesema Killagane.
Ameongeza kuwa kushuka kwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kumesababishwa na kuhamisha vyanzo vya mapato kutoka serikali za mitaa na kupelekwa serikali kuu, kufutwa kwa baadhi ya kodi ikiwemo ushuru wa mazao. Pia usimamizi mbaya wa ukusanyaji mapato mfano CAG amebaini kuwa sh. Bilioni 2.41 katika halmashauri 39 hazikuingizwa kwenye mfumo wa benki huku bilioni 3.54 zilizokusanywa na mawakala wa serikali hazikufika kwenye halmashauri 41.
Kutokana na hali hiyo, miradi mingi ya maendeleo haikutekelezwa kwa wakati. Ripoti ya CAG imeonyesha kuwa asilimia 28 tu bajeti ya miradi ya maendeleo ndio iliyotumika kwenye halmashauri.
“Miradi 60 yenye thamani ya milioni 782.47 katika halmashauri 13 ilikamilika lakini haijaanza kutumika. Kwahiyo, hali hiyo unaonyesha dhahiri kupungua kwa uwajibikaji katika usimamizi wa miradi. Pengo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo haliwezi kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Kallagane.
Ameshauri kuwa serikali inapaswa kupunguza matumizi na manunuzi yasiyo ya lazima ili kutoa nafasi kwa halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuwaondolea wananchi ugumu wa upatikanaji wa huduma za kijamii.
“Zaidi ya 70% ya matumizi ya serikali yako kwenye manunuzi. Kinyume na matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya 2011 na kanuni zake za 2013. Mikataba mibovu ya manunuzi inaongeza gharama za uendeshaji katika halmashauri,” amesisitiza Kallagane.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dkt. Richard Mbunda amesema serikali inapaswa kujitathmini na kurekebisha makosa ambayo yameainishwa kwenye ripoti ya CAG.
“Nadhani ni nafasi pekee ambapo serikali inaweza kujiangalia na kujifanyia tathmini ya kina kulingana na utekelezaji wa bajeti . Bajeti kwa mfano ya serikali za mitaa kwamba zilipata fedha zaidi ya bajeti ilivyoamriwa lakini vilevile zingine zikapata pungufu. Kwahiyo vitu kama hivyo vinaleta maswali.” Amesema Dkt. Mbunda.
Ameshauri serikali kuzingatia mgawanyo mzuri wa bajeti na kuzitengea bajeti kubwa halmashauri zinazokabiliwa na matatizo mengi ili kuondoa umasikini wa wananchi wanaoishi vijijini.
“Kwasababu bajeti ni namna pekee ya kugawanya rasilimali za nchi sasa inavyonekana kwamba kuna baadhi ya serikali za mitaa zinapata bajeti kubwa zaidi ya zingine, itaibua maswali kwa baadhi ya watu.” Ameshauri Dkt. Mbunda.
Naye CAG mstaafu, Ludovick Uttoh amesema ni muhimu sheria na taratibu za uandaaji na utekelezaji wa bajeti zizingatiwe ili kuondoa makosa kwenye matumizi ya rasilimali za nchi.
Ikumbukwe kuwa serikali chini ya rais John Magufuli ilijitoa katika Mpango wa Uendeshaji Serikali kwa Uwazi (OGP). Mpango ambao uliwezesha taasisi za serikali kuwajibika kwa wananchi.