ASKARI wa kikosi cha zimamoto katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Masood Gadafi amezua tafrani ofisini kwake baada ya kukwidana na mteja wake na kisha akatafuna stakabadhi za serikali kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Habari zilizozagaa jijini hapa zinadai kwamba licha ya kuidhalilisha ofisi ya serikali , askari huyo mwenye cheo cha ‘meja’ bado hajachukuliwa hatua zozote za kinidhamu.
Inadaiwa kuwa tukio hilo lililokusanya umati wa watu wakiwemo wapita njia, lilitokea katika ofisi za zimamoto jijini hapa siku ya Septemba 15 mwaka huu, kati ya saa 6 na saa saba mchana.
Kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, inadaiwa kuwa chanzo cha tafrani hiyo ni ‘uchakachuaji’ unaofanywa na baadhi ya askari wa kikosi cha zimamoto Jijini hapa.
“ …tafrani hiyo ilitokea baada ya mteja mmoja aliyefamika kwa jina moja la Daniel kuomba kupatiwa stakabadhi kwa ajili ya malipo ya ‘sticker’ za magari yake malori yake mawili ambayo yanafanya biashara katika wilaya ya Magu” kilidai chanzo cha habari .
Inadaiwa mteja wa askari huyo alistukia uhalali wa stakabadhi alizokabidhiwa na ndipo alimkamata ili amfikishe katika vyombo vya sheria.
“ Pamoja na kuhoji uhalali wa zile stakabadhi, mteja wake alitaka kumkamata Masood mara baada ya kubaini kwamba stakabadhi hizo zilikuwa feki. ” inadaiwa.
Habari zinafafanua kuwa stakabadhi hizo zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya malipo ya stika za kughushi (gazeti hili limepata nakala zae) za malori yenye namba za usajili T915AVC na T394ABV.
Inadaiwa Masood kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyakazi wenzake a kikosi cha zimamoto Jijini hapa wamekuwa wakilalamikiwa kwamba wanatoa sticker pamoja na stakabadhi feki kwa wateja kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia zisizokuwa halali.
Kwa mujibu wa habari, askari huyo anatumia vitabu vilivyoibwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2010/2011 .
Habari zaidi zilizothibitishwa kwa njia ya simu na Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto nchini, Maiko Shija zinadai vitabu hivyo viliibwa katika ofisi ya zimamoto makao makuu, Jijini Dar es salaam na kwamba taarifa za upotevu huo zilitolewa kupitia vyombo vya habari.
“ Ni kweli hilo tukio lipo lakini ninaomba uongee na mkuu wangu wa idara” alithibitisha Masood huku akikabidhi simu yake ya mkononi kwa bosi wake wa idara. ya simu.
Hata hivyo, mkuu wake wa idara aliyejitambulishwa kwa jina la Musa Kaboni hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa bado linashughulikiwa kiofisi.
“ Ni kweli kwamba mimi ndiye bosi wake, na ndiye nilikuwa ninamkaimu Mkuu wa kituo cha Zimamoto hapa Jijijini Mwanza; lakini sina cha kukuambia zaidi ya kusema kuwa linashughulikiwa” alisema Kaboni ambaye ni mkuu wa idara ya utoaji wa stika zinaohusiana na moto katika magari, nyumba pamoja na boti Jijini hapa.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha Zimamoto jijini hapa, Julius Bulambu alikiri kupokea taarifa za kuwepo kwa tukio hilo.
“ Mimi sikuwepo wakati tukio hilo linatokea; aliyekuwa akikaimu ni afande Kaboni. Lakini baada ya kurejea nilipewa taarifa ambazo bado ninazifanyia kazi” alidai Bulambu.
Alifafanua kwamba tayari ameshachukua hatua, ikiwemo kumhoji Masood na kwamba bado anasubiri kupata maelezo ya kutoka kwa mlalamikaji( mteja aliyekwidana na Masood).
Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto Makao Makuu nchini, Maiko Shija, pia alikiri kupokea taarifa za kuwepo kwa tukio hilo.
“ Taarifa hizo ninazo lakini wasemaji wakuu wa suala hilo ni uongozi wa Zimamoto Jijini Mwanza ambao nimeambiwa walishuhudia wakati tukio hilo linatokea” alisema Shija kwa njia ya simu na kuongeza kuwa ofisi yake inaendelea kufanya ufuatiliaji.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Liberatus Barlow alisema suala hilo bado haljaripotiwa ofisini kwake.