Askofu Laizer awabeza wanaolia kukosa Uwaziri na U-DC

Jamii Africa

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer amewabeza mawaziri walioenguliwa na wanasiasa ambao wanalamikia uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete, akisema hawana hoja na wanajadili jambo lisilokuwapo.

Alikuwa akitoa nasaha zake katika mazishi ya mfanyabiashara Elitira Abraham Mengi, ambaye ni kaka wa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, yaliyofanyika Machame Mkuu, mkoani Kilimanjaro Ijumaa (jana) mchana.

“Maneno mengi ya nini? Taratibu zinatoa mamlaka kwa Rais kufanya mabadiliko ya ma-DC na Mawaziri, na hapaswi hata kutoa sababu, sasa unaposema amekosea ama umeonewa, unaleta maneno mahali ambapo hakuna maneno,” alisema Askofu Laizer.

askofu laizer bishop

Askofu Laizer msibani huko Machame Mkuu, Kilimanjaro

Naye Askofu Dk. Martin Shao, alisema wale ambao waliondolewa ama waliokosa nafasi katika uteuzi wa sasa aliwaomba wahusika washukuru Mungu na kwamba wajue Mungu ana mipango yake na sasa wamsaidie Rais na Watanzania.

Katika mazishi hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, aliwasisimua watu waliohudhuria mazishi hayo kwa kuelezea jinsi marehemu Elitira alivyomshauri kuachana na siasa kwa miaka 20, kabla ya kukubaliana naye hivi karibuni.

freeman mbowe na samwel sitta

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe akiwa na Mhe. Waziri Samwel Sitta

Mbowe ambaye ni mwanafamilia, alisema marehemu Elitira akiwa bado mwana CCM aliporidhia alimpa ng’ombe kama ishara ya kumtakia kheir na kumpa maneno ya hekima kwamba awe “msikilizaji zaidi na mzito kujibu” maneno ambayo amesema ndio dira yake.

Wengine waliohudhuria ni Mawaziri, Samuel Sitta, Bernad Membe, Harrison Mwakyembe na Naibu Waziri Lazaro Nyalandu. Pia alikuwapo DC Mteule, Novatus Makunga, ambaye amepangiwa wilaya ya Hai, ulipokuwa msiba.

umati wa waombolezaji huko machame

Sehemu ya waombolezaji katika msiba wa Marehemu Elitira Abraham Mengi

Familia ya mawaziri wakuu wastaafu John Malecela na Jaji Joseph Warioba, ziliwakilishwa na William J. Malecela na Kipi Warioba, ambao walitajwa kuwa karibu na familia hizo.

Walikuwapo maaskofu watano akiwamo Askofu Mstaafu Erasto Kweka, wachungaji, viongozi wa dini nyingine huku waliopata nafasi ya kuzungumza walirifurahishwa na mshikamano ulionyeshwa kwa watu wa itikadi na dini tofauti kuwa pamoja.

Sitta ambaye alitoa nasaha kwa niaba ya wenzake, alisema alikuwa karibu na marehemu Elitira pamoja na familia ya Mbowe alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro miaka ya nyuma.

Mbowe, Sitta, Membe na Mwakyembe ambao walionekana wakichangamkiana muda wote waliondoka pamoja kurejea Dar es Salaam Ijumaa usiku.

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *