Siku moja baada ya serikali kutangaza makubaliano yaliyofikiwa na kampuni ya Barrick kulipa fidia ya bilioni 700, Kurugenzi ya fedha ya kampuni ya Acacia imesema haina fedha za kuilipa Tanzania .
Kampuni ya Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick kupitia Mkurugenzi Mkuu wa Fedha, Andrew Wray akihojiwa na jarida la Reuters amesema kampuni hiyo haina fedha za kuipatia Tanzania bilioni 700 (US$ Milioni 300) kama walivyokubaliana katika mazungumzo yaliyofanyika katika miezi mitatu iliyopita.
Kampuni ya Barrick ilikubali kutoa fedha hizo ikiwa ni njia ya kuendelea na mazungumzo ya kuilipa Tanzania kodi ya asilimia 70 ambapo Sheria mpya madini itatumika katika mchakato mzima wa kusimamia sekta ya madini nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ametoa maoni yake wakati akihojiwa na radio Dutch Velle ya nchini Ujerumani mapema leo amesema kuwa serikali ya Tanzania imefanya makosa kutoa taarifa mapema ya makubaliano hayo kabla Kampuni ya Acacia nchini Uingereza kuthibitisha malipo hayo.
Amesema hata kama walikubaliana kupata mgao wa 50/50 lakini kampuni za madini zina mbinu mbalimbali za kuongeza gharama za uzalishaji na kuifanya faida inayopatikana kuwa kidogo. Ni muhimu kwa viongozi kuwa makini kabla ya kufanya maamuzi na kuelewa mfumo wa utendaji wa sekta ya madini ili kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa makubaliano.
Mchangiaji wa jukwaa la Jamii Forums anayejulikana kwa jina la Return of Undertaker ameandika kuwa;
“Wengi wasichofahamu, makampuni haya hayapati faida kubwa kutoka kwenye mauzo ya dhahabu bali wanapata faida kubwa kwenye kuuza hisa. Uzalishaji unalenga kuwapa ujasili wadau ili hisa ziweze kupanda”
“ Mathalani kabla ya Brexit hisa za Acacia zilikuwa na thamani kama ya dola 2.5 hivi. Baada ya Brexit zilipanda mpaka kufikia dola 5. Walioamua kuuza hisa zao walipata faida ya 100%. Wewe kama unasubiria faida ya 50/50 unaweza kusubiri mpaka uchoke. Serikali itamiliki 16%, je tutakuwa tunauza hisa na kununua?”.
Mapema mwaka huu Rais John Magufuli aliunda tume kuchunguza thamani ya mchanga wa madini (makinikia) unaosafirishwa nje ambapo tume ilibaini kiasi kikubwa cha mchanga hakilipiwi kodi na wawekezaji hao hutumia njia hiyo kuikosesha serikali mapato.
Kutokana na ripoti hiyo Rais alizuia usafirishaji wa mchanga na kuitaka kampuni ya Dhahabu ya Barrick kulipa bilioni 492 kama fidia ya madeni ya nyuma. Ili kutatua changamoto hiyo serikali na kampuni hiyo zilianza mazungumzo ambapo yamedumu kwa siku 80 na serikali ikaja na taarifa kuwa Barrick wamekubali kulipa na wako tayari kufuata masharti mapya.