Bima ya afya kuwahakikishia wazee huduma bora za matibabu

Jamii Africa

Na Daniel Samson

Maendeleo mazuri ya afya ya mtu ni pamoja kuwa na uhakika wa kupata matibabu akiugua au kupata ajali. Bima ya afya ni njia mojawapo inayomuhakikishia mtu kupata huduma za afya wakati wowote na mahali popote pasipo kujali hali ya kipato chake.

Lakini idadi ya wananchi wanaomiliki bima ya afya ni wachache ikilinganishwa na wale wanaotumia gharama kubwa kupata matibabu katika hospitali.

Utafiti uliofanywa na shirika la Twaweza (2017) kuhusu sauti za wananchi katika sekta ya afya unathibitisha kuwa mwananchi 1 kati ya 4 ana bima ya afya ambayo ni sawa na asilimia 27 ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita (25-26%).

Idadi hiyo ya wananchi wenye bima inaonekana kuongezeka kila mwaka, lakini ongezeko hilo ni dogo ikilinganishwa kuongezeka kwa gharama za kupata huduma za afya.

Bima ya afya hutolewa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na mifuko mingine kama Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na stategis.

Kundi linaloathirika sana kwa kukosa bima ya afya ni wazee ambao hukabiliwa na magonjwa ya mara kwa mara na kulazimika kutumia gharama kubwa kupata matibabu.

Katika sera ya Afya na Sheria ya Utumishi wa Umma inamtaja mzee kuwa ni mtu yeyote aliyefikisha miaka 60 kwa sababu nguvu za kufanya kazi zinakuwa zimepungua.

Wazee wako katika makundi mbalimbali, ambapo lipo kundi la wazee wastaafu, wafugaji, wakulima,wavuvi na wasio na ajira. Makundi haya ya wazee hutofautiana katika mahitaji na changamoto wanazokabiliana nazo kila siku.

Mfano mzee aliyestaafu utumishi wa umma hupewa pensheni na bima ya afya ambayo humsaidia kupata matibabu,ambapo kupata huduma za afya kwa wazee wengine ambao hawakuwa katika sekta ya ajira ni changamoto kubwa.
Licha ya ukweli kwamba mzee anapozeeka nguvu ya uzalishaji mali inapungua, lakini bado anatakiwa kuheshimiwa, kulindwa na kupewa huduma zote za afya kama binadamu wengine.

Kwa kutambua hilo serikali ilipitisha sera ya matibabu bure kwa wazee na kuwawezesha kupata huduma za afya bila malipo katika vituo vya serikali.

Lakini hali ya matibabu bure katika maeneo mengi sio ya kuridhisha kwa sababu bado idadi kubwa ya wazee wanatozwa fedha na kupata usumbufu kutoka kwa wahudumu wa afya bila kujali hali zao.

Ripoti ya Twaweza (2017) juu ya Sauti za Wananchi inathabitisha kuwa “wananchi wanne kati ya kumi (37%) wanasema kuwa watu wenye miaka zaidi ya 60 hulazimika kulipia huduma hizo”.

Ili kuondokana na usumbufu wa kukosa matibabu, wazee walio na umri zaidi ya miaka 60 wamekuwa wakidai kupatiwa bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya.

“Sisi wazee ni binadamu kama binadamu wengine tuna haki ya kuheshimiwa na kupata huduma za afya” haya ni maneno ya mzee Elisha Mwamkinga kutoka shirika la The Good Samaritan Social Services Tanzania (GSSST) ambaye amekuwa akipigania haki za wazee.

Anasema wanapata usumbufu katika baadhi ya hospitali na kutakiwa kulipia matibabu na wahudumu huwanyanyasa. Kutokana na changamoto hizo anataka uandaliwe utaratibu wa kupata vocha maalumu zitakazogharimia huduma zote za afya.

“Wazee tunadharaulika, hatuthaminiwi na hatupati huduma bora za afya kwa sababu hatuna kipato. Tunaiomba serikali itupatie vocha maalum ili tupate huduma za afya kwa wakati” anasema mzee Mwamkinga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa shirika la HelpAge International, Smart Daniel anasema licha ya wazee kutopata huduma za afya bado wanakabiliwa na changamoto za usalama, kipato duni na mauaji ya kishirikina.

“Kuna watu wanatoa huduma za afya lakini hawaelewi changamoto za wazee, tumekuwa na tatizo katika jamii yetu kuhukumu wazee kuwa ni wachawi”.

Anaitaka jamii na serikali kuwajali wazee na kuwaandalia mazingira sahihi ya kisheria ya kupata huduma zote za kijamii ikiwemo kuwapatia bima ya afya ili wasipate usumbufu katika vituo vya afya.

“ Tusiangalie mambo mabaya tu ya wazee Tuwatengenezee mfumo mzuri wa kisheria na sera ambao utawahakikishia huduma za afya na kupata kipato cha kujikimu katika maisha yao” anasema Daniel.

Afisa Ustawi wa Jamii (Kitengo cha Wazee), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ester Kaminda anasema serikali inashirikiana kwa karibu na wadau hasa mashirika na Asasi za kiraia kuzipatia ufumbuzi changamoto za wazee ikiwemo kuhakikisha ustawi mzuri wa afya zao.

Inaelezwa kuwa ni asilimia 4 tu ya wazee wote ndio wanatumia bima ya afya nchini ambapo ni sawa na wananchi wasiozidi milioni moja nchini kote.

Kwa mujibu wa Sensa ya 2012 kulikuwa na wazee milioni 2,449,257 ambao ni sawa asilimia 5.7 ya watanzania wote. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka ambapo katika kipindi cha miaka kumi ijayo Tanzania inatarajiwa kuwa na wazee milioni 16.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *