WANAFUNZI wenye ulemavu wa ngozi wanaohitimu darasa la saba katika Shule ya Msingi Mugeza Mseto ya Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, wamegeuza sehemu hiyo makazi yao ya kudumu kwa kuhofia usalama wa maisha yao wakirejea nyumbani.
FikraPevu imeelezwa kuwa shule hiyo iliyoanza kupokea walemavu wa ngozi tangu mwaka 2008 kutoka Kagera na mikoa jirani imeanza kulemewa na mzigo huo kwa kuwa wanafunzi wanaoendelea kupiga kambi shuleni hapo ni lazima pia waendelee kuhudumiwa.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mugeza Mseto Jenetulda Leonidas (aliyeshika tama) akitafakari jambo shuleni hapo akiwa na wenzake na alitolewa Kijiji cha Kumugamba, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera ili kumnusuru na tishio la mauaji dhidi ya watu wenye albinism.
Shule hiyo iliyopo nje kidogo ya Mji wa Bukoba, ilianzishwa mwaka 1950 kama shule ya kati na mwaka 1966 ilianza kusajiri wanafunzi wasioona kabla ya kupoanza kupokea wanafunzi wenye ulemavu wa viungo kutoka maeneo mbalimbali nchini mwaka 1974.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Johannes Josephat, aliieleza FikraPevu kuwa, shule hiyo inafanya vizuri kitaaluma ambapo mwaka 2016 walihitimu wanafunzi 58 na waliofaulu walikuwa 39, miongoni mwao wakiwemo walemavu 20 wa aina tofauti.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili shule hiyo ni baadhi ya walemavu wa ngozi waliohitimu na kutochaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza katika shule mbalimbali nchini kuogopa kurejea kwao kwa hofu ya kupoteza maisha yao.
Mwalimu huyo alisema changamoto nyingine za shule hiyo ni kutokuwa na uzio hali inayohatarisha usalama wa wanafunzi 150 wa bweni, wakiwemo walemavu wa ngozi, huku watumishi wakiishi mbali na eneo la shule hivyo kushindwa kuwasaidia wanafunzi kwa wakati.
FikraPevu inafahamu kwamba, Oktoba 27, 2016 Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba iliwatia hatiani mtu na mkwe wake kwa mauaji ya mlemavu wa ngozi Magdalena Andrea yalitotokea mwaka 2008 katika Wilaya ya Biharamulo na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Watuhumiwa waliokutwa na hatia katika tukio la Septemba 21, 2008 ni Lameck Bazil mganga wa jadi kutoka Mkoa wa Mara na Pancras Minago ambaye upelelezi ulionyesha ni mkwe wa mtuhumiwa wa kwanza.
Jaji Firmini Matogolo alisema upande wa Jamhuri ulifanikiwa kuthibitisha hoja zake kwa kuwasilisha vielelelezo 11 na mashahidi 12 dhidi ya washtakiwa na kuwa utetezi wa washtakiwa kuwa hawakuwepo kwenye eneo la tukio hauwezi kukubalika kwani ushahidi ulionyesha walikusudia kufanya mauaji.