Imeelezwa kwamba kukosekana kwa lishe bora kwa wajawazito na watoto katika wilaya ya Bunda, ni chanzo cha makundi hayo kupungukiwa damu.
Hayo yameelezwa na mratibu wa afya ya mama na mtoto wilayani humo, Daines Lyimo, anasema hali hii inatokana na kuadimika kwa samaki ambao walikuwa ndio chakula na tegemo kwa akinamama na watoto.
Daines anasema kwa sasa minofu ya samaki hupelekwa nje ya nchi na kuwaacha wakazi wa Bunda, wakiwemo wajawazito na watoto kuishia kula viazi na vyakula vingine, ambavyo haviwezi kumsaidia mama na mtoto kuwa na afya njema pamoja na kinga bora ya mwili.
Mratibu wa wilaya ya Bunda, Daines Lyimo akiwa na kaimu mkurugenzi wa Wilaya hiyo Charles Makame
Anasema kutokana na hali hiyo wajawazito wengi wanaojifungua wanakuwa na tatizo la upungufu wa damu na kulifanya tatizo sugu kwa wilaya ya Bunda.
“Tatizo la upungufu wa damu kwa wilaya ya Bunda ni kubwa kwani ni 60% ya wajawazito wenye upungufu wa damu.” Anaeleza.
Daines anasema kila wajawazito 10 wanaokuja kujifungua, basi wawili watakuwa na upungufu wa damu.