Bunge laitaka Serikali imalize mgomo wa madaktari haraka

Jamii Africa

SAKATA la mgomo wa Madaktari nchini, limeanza kuchukuwa sura mpya, baada ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuvunja ukimya juu ya tatizo hilo nyeti, ambapo imeitaka Serikali kufanya mazungumzo haraka na madaktari, kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi madai yao.

Kamati hiyo imesema, imesikitishwa sana na hatua ya Serikali kuonekana kushindwa kuyapatia ufumbuzi wa haraka madai ya wataalamu hao, jambo ambalo limeanza kuleta athari kubwa kwa taifa kwa baadhi ya wananchi kupoteza maisha yao kutokana na kukosa huduma hospitalini.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya kudumu ya Bunge, Margreth Sitta, alitoa rai hiyo kwa Serikali jana Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya La Kairo, muda mfupi baada kumaliza ziara ya kamati hiyo Mkoani Shinyanga.

Sitta ambaye amewahi kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, aliwaambia wanahabari hao kwamba, Serikali inatakiwa kukaa pamoja na madaktari hao kufikia muafaka wa madai yao, ili wasiendelee na mgomo huo ambao tayari Watanzania wameshaanza kuathirika.

“Kamati yangu ya Bunge ya Huduma za Jamii inaishauri Serikali ikutane haraka na kuzungumza na madaktari wetu hawa, ili kusikiliza na kuyapatia ufumbuzi madai yao. Siku zote wapiganapo fahari wawili nyika ndiyo huumia.

“Hatutaki kuona migomo ya namna hii. Kama ni migomo ije pale ambapo Serikali haina uwezo na jambo husika, na siyo hii maana Serikali wakikubali kuyapa ufumbuzi madai yao tatizo wala mgomo hupo”, alisema mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakati akijibu swali la mwandishi wa habari hizi.

Hivi karibuni madaktari walitangaza na kuanzisha mgomo rasmi kwa kutoingia kazini, ikiwa ni lengo lao la kuishinikiza Serikali iyapatie ufumbuzi madai yao wanayodai ya msingi ya kuongezewa mishahara, kuboreshewa mazingira ya kazi pamoja na kupewa nyumba za kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha alisema, Kamati yake hiyo ya Bunge ipo tayari kukutana na kuzungumza na viongozi wa madaktari hao iwapo watakuwa tayari, ili kuweza kuangalia namna ya kumaliza kabisa mgogoro huo unaodaiwa kuungwa mkono na madaktari wengi kutoka baadhi ya hospitali za Rufaa na nyingine nchini.

“Kamati tupo tayari hata leo hii wakisema tukutane nao. Wakiomba kukutana na sisi tutafanya hivyo maana hii ni nchi yetu sote na hatutaki athari kama hizi.

“Tunaamini hata wao si kwamba wanataka walipwe hiyo mishahara, kuboreshewa mazingira ya kazi na vingine le oleo hii. Kikubwa ni makubaliano tu ndicho Serikali inapaswa itambue hivyo”, alisema Margeth Sitta huku akionekana kusikitishwa zaidi na hali ilivyo sasa ya mgomo.

Hata hivyo, alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi iwapo Kamati yake hiyo itakuwa tayari kwenda kulishawishi Bunge kukatwa posho za Wabunge za sh. 200,000 kila mmoja kwa kikao kimoja, Sitta alisema: “Hizo posho mbona mimi nazisikia tu magazetini?. Mimi sijapokea wala sijaona hiyo 200,000 kwenye akaunti yangu”.

Pia Sitta alipotakiwa kuzungumzia msimamo wa Kamati yake juu ya tamko la madaktari kuwataka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu  wake, Lucy Nkya pamoja na Katibu Mkuu wa Wizra hiyo, Blandina Nyoni kuondolewa Wizarani hapo, alisema kwa kifupi: “Suala hili tuwaachie Serikali yenyewe”.

Kwa upande mwingine, mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Sitta aliionya Serikali kuwa makini na mambo kama hayo, na kwamba siyo lazima watumishi waanzishe mgomo mkali ndiyo madai yao yasikilizwe, na kwamba Serikali haina budi kuanzisha utaratibu mpya wa kukutana na kuzungumza na watumishi wake, ili kutatua changamoto mbali mbali zinazojitokeza.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza

2 Comments
  • Limejitokeza jukwaa la kutafutia umaarufu. Kila mmoja ana mizani mkononi ya kuona uzito unaelekea wapi ili aunge mkono huko. Kila mmoja anaonyesha umahiri katika fani ya unafiki. Mwangwi wa kauli ya viongozi ndo unatuumiza masikio maana hakuna lililokuwa halitegemewi. Ubabe bila busara kama kawaida vimejiri. God will sort things out for the poor including a peacefull passage to oblivion

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *