“NANI kauona mwaka! Nani kauona mwaka! Ni majaliwa yake Mungu eeeh, kuuona mwaka!…”
Haya ni mashairi ya wimbo wa ‘Nani Kauona Mwaka’ uliotungwa na Shaaban Dede ‘Kamchape’ na akauimba akiwa na bendi ya DDC Mlimani Park Orchestra mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Naam. Dede au ‘Super Motisha’ hatunaye tena. Mwanamuziki huyo mkongwe aliyejaaliwa kipaji cha utunzi na uimbaji, amefariki dunia leo Alhamisi saa 2:00 asubuhi, Julai 6, 2017 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Dede, ambaye anafahamika kwa utunzi wa tungo nyingi zilizosheheni ladha nzuri na maudhui bora kwa jamii, alikuwa amelazwa kwa wiki mbili kwenye Wadi ya Mwaisela Namba 5 kutokana na kusumbuliwa na tatizo la mishipa ya damu.
Kifo cha mwanamuziki huyo ambaye alikuwa akiitumikia Msongo Music Band kimewashtua mashabiki wengi wa muziki nchini Tanzania, hasa baada ya kuelezwa hivi karibuni kwamba hali yake ilikuwa ikiendelea vyema.
Hili ni pigo kwa tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, kwani Dede ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe waliosalia ambao walikuwa bado wanaendelea na muziki wa jukwaani.
Dede alizaliwa Kanyigo, Bukoba mwaka 1954 ambapo alianza kuupenda muziki tangu akiwa mdogo kwa vile wajomba zake walikuwa na bendi iliyofahamika kama Ryco Jazz.
Hata hivyo, bendi yake ya kwanza kujiunga nayo ilikuwa ikimilikiwa na Chama cha TANU na ilikuwa na maskani yake Biharamulo.
Mwaka 1974 alijiunga na Bendi ya Polisi Bukoba ambayo hakudumu nayo sana kwani mwaka 1975 alikwenda kujiunga na Tabora Jazz ‘Wana Segere Matata’ iliyokuwa ikiongozwa na Shem Ibrahim Kalenga.
Ni huko ndiko alikoanza kufahamika na kutokana na umahiri wake katika uimbaji, hatimaye bendi ya Dodoma International ikamnyakua mwaka 1976 ambako alidumu kwa miaka mitatu.
Mnamo mwaka 1979 alijiunga na bendi ya Juwata Jazz ‘Wana Msondo Ngoma’ (sasa Msondo Music Band ambayo alikuwa akiitumikia hadi mauti yalipomfika). Ikumbukwe kwamba, wakati anakwenda Juwata, bendi hiyo ilikuwa imeondokewa na wanamuziki wake kadhaa mahiri wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo na mpiga solo Abel Baltazar ambao walikwenda kuanzisha Mlimani Park Orchestra pale Mwenge Survey kabla bendi hiyo haijachukuliwa na STC na baadaye DDC.
Baada ya kutamba na wimbo wa Fatuma, alidumu na Juwata hadi mwaka 1982 alipohamia Mlimani Park Orchestra ‘Wana Sikinde Ngoma ya Ukae’, lakini akakaa kwa mwaka mmoja tu kabla ya Shirika la Bima la Taifa halijamchukua na kujinga na Bima Lee Orchestra ‘Wana Magnet Tingisha – Magnet Ndele’ pamoja na akina Max Bushoke. Huko aliibuka na wimbo wa Shangwe ya Harusi.
Baadaye alikaa kwa muda mfupi na bendi ya International Orchestra Safari Sound (OSS) “Wana Ndekule’ iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabishara Hugo Kisima, ambapo alikuwa na wamamuziki kama Maalim Gurumo, Hassan Rehani Bitchuka na mpiga solo Abel Baltazar. Pamoja na kushiriki nyimbo nyingi, lakini aliibuka na wimbo wa Nyumba ya Mgumba haina Matanga.
Mnamo mwaka 1987 Wakati Bitchuka aliporejea Sikinde, Dede alirudi tena Juwata ‘Msondo Ngoma’ ambako lakini alikaa kidogo tu na kurejea tena Sikinde baada ya kufanyiwa vitendo visivyo vya kiungwana na wanamuziki wenzake.
Ni hapo aliporejea Sikinde ndipo akatunga wimbo wa ‘Talaka Rejea’ akilalamikia kitendo hicho, ambapo anasema kwenye wimbo huo:
“Ulinitaliki kwa talaka rejeaaa….
Bila aibu ulininyang'anya nguo mbele za watuuu…
Huku ukitoa kashfa, nikajifunze kwa wazazi wangu…
Leo unaniambia nirejee kwako, ulivyonidhalilisha umesahau…
Mtu anapochukiaaa, moyo kuurudisha furahani ni vigumuuu…
Ukweli nasemaaaa, ni heri nipate tabu kuliko kurejea kwakoooo…”
Kwa hakika, tangu aliporejea Sikinde, Dede, akiwa na wanamuziki wengine mahiri kama Francis ‘Nasir’ Lubua, Hassan Kunyata, Hussein Jumbe Totoro ‘Mzee wa Dodo’ na wengineo waliweza kuiimarisha bendi hiyo na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya wapinzani wapo Msondo.
Ushindani huo ulifanya muziki wa dansi ukue na kuimarika kiasi kwamba kumbi za DDC na Amana zilikuwa hazikauki mashabiki kila bendi hizo zilipokuwa zikitumbuiza.
Mnamo mwaka 2011, Dede akaamua kujiunga tena na Msondo ikiwa ni mara yake ya tatu, na safari hii aliweza kufanya kazi nzuri akishirikiana na wanamuziki wengine wakongwe wakiwemo akina Said Mabera.
Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Dede mahali pema. AMEN!