Hatimaye Simba yakwea pipa, yaitandika Mbao FC 2-1 fainali Kombe la Shirikisho

Daniel Mbega

BAADA ya rufaa yake kutupwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hatimaye Simba wamejifariji kwa kunyakua Kombe la Shikirisho la Azam kwa kuifunga Mbao FC mabao 2-1 kwenye mechi iliyochezwa dakika 120. Simba sasa itashiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika.

FikraPevu inafahamu kwamba, Simba ilikata rufaa FIFA kupinga hatua ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka ushindi wa pointi tatu dhidi ya Kagera Sugar ambayo walidai ilimchezesha Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano.

FikraPevu inaripoti kwamba, FIFA imesema kwa mujibu wa Kanuni za Nidhamu (FDC), Ibara ya 108 (1) na (2), haina mamlaka ya kutengua uamuzi uliofanywa na Shirikisho la Soka la nchi mwanachama.

FIFA imesema baada ya kupitia nyaraka zote zilizowasilishwa na Simba SC pamoja na TFF wameona kwamba uamuzi uliofanywa na kamati maalum ya TFF ulikuwa sahihi na utaendelea kubaki kama ulivyo.

Hatua hiyo iliifanya Simba igangamale katika mchezo wa leo Jumamosi, Mei 27, 2017 wa fainali dhidi ya Mbao FC kutoka Mwanza, ambao ulipigwa katika dimba la Jamhuri mjini Dodoma na hatimaye kupata tiketi ya kukwea pipa wakati itakaposhiriki mamshindano ya kimataifa mwakani baada ya kutakosa kwa miaka minne.

Simba imetwa taji hilo pamoja na kitita cha Shs. 50 milioni.

Kumbukumbu za FikraPevu zinaonyesha kwamba, mara ya mwisho kwa Simba kushiriki mashindano ya kimataifa ilikuwa mwaka 2013 wakati iliposhiriki Ligi ya Mabingwa na kutolewa katika raundi ya awali na Recreativo do Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0.

Kwanza ilikubali kipigo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Februari 17, 2013 na ziliporudiana mjini Luanda Machi 3, 2013 ikatandikwa 4-0.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa timu hiyo kupata ushindi kwani vijana wa Mbao FC, ambao waliwatoa Yanga kwenye nusu fainali, walionyesha ushindani mkubwa wakiwa na shauku ya kushiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja msimu huu.

Bao la Kichuya katika dakika ya 120 ndiyo iliyowapatia Simba tiketi ya mashindano ya kimataifa baada ya kuongoza na hatimaye kukosa penati katika dakika ya 105 iliyopigwa na Blagnon kufuatia mlinzi wa Mbao kuunawa mpira katika jitihada za kuzuia shuti la Juuko.

Dakika 90 zilishuhudia milango ya timu zote ikishindwa kufunguka, lakini katika dakika ya 5 ya muda wa nyongeza, yaani dakika ya 95, Blagnon aliweza kuiandikia Simba bao la kuongoza baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Abdi Banda.

Mbao FC hawakukata tamaa, wakaendelea kulisakama lango la Simba na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 109 kupitia kwa Ndaki Robert, ambaye mabeki wa Simba walidhani ameotea.

Mbao ilikuwa na usongo mkubwa wa kutwaa taji hilo na kushiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya kimataifa na kuandika historia mpya ya timu za Mwanza tangu Pamba FC ilipofanya hivyo zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mchuano mkali tangu mwanzo

Tangu mwanzo wa mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam, ilionekana kulikuwa na mchuano mkali na Mbao FC walionyesha kudhamiria kufanya vizuri zaidi.

FikraPevu inatambua kwamba, Mbao walifuzu hatua hiyo ya fainali kwa kuichapa Yanga bao 1-0 kwenye nusu fainali iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Simba wao walipata ushindi kama huo dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Simba SC

Mbao FC

Kabla ya hapo, Mbao walikuwa wameitoa Toto African pia ya Mwanza kwa mikwaju ya penalty katika Raundi ya 6 baada ya kutoka suluhu muda wa dakika 90, wakati Simba yenyewe iliifunga African Lyon 2-1.

Katika Robo Fainali, Mbao wakaitandika Kagera Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, na Simba ikapata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Madini FC ya Arusha kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Matokeo ya Ligi Kuu

Pengine Simba itajivunia matokeo mazuri dhidi ya Mbao FC kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kushinda mechi zote mbili – kwanza ikiifunga bao 1-0 Oktoba 20, 2016 na baadaye mabao 3-2 Aprili 10, 2017.

Hata hivyo, FikraPevu inatambua kwamba Mbao FC, ambayo huu ndio msimu wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu, imeonyesha kiwango kizuri licha ya matokeo ya mwishoni kuitia mashakani na kukaribia kushuka daraja.

Miongoni mwa matokeo ya ajabu ambayo Mbao ilionyesha kwenye msimu wa Ligi Kuu ni kuitandika Azam FC 2-1 Novemba 6, 2016, ikaifunga Ruvu Shooting 2-0 kabla ya kuichabanga Mtibwa Sugar mabao 5-0.

Haya yalikuwa matokeo ya kushangaza kwa mashabiki wengi wa soka ambao wanaamini hata katika mechi ya fainali dhidi ya Simba, timu hiyo inaweza kufanya maajabu makubwa na hata kunyakua taji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *