CAG aanika ufisadi serikali za mitaa. Vyama vya siasa vyaitia doa serikali kuu

Jamii Africa
Rais John Magufuli leo akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ameagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Pangani na Kigoma Ujiji ambazo zimetajwa kuwa na hati chafu, wasimamishwe kazi. - Aidha, Rais ameagiza fedha za mradi wa maendeleo katika Wilaya ya Bumbuli zirudishwe hazina endapo viongozi waliokabidhiwa watashindwa kufikia muafaka kutokana na kubishana kuhusu sehemu ya kujenga Makao Makuu ya Wilaya, licha ya Mkuu wa Mkoa kupendekeza ijengwe Hospitali na wazo lake kupingwa - Katika muhtasari wa ripoti yake, Prof. Mussa Assad amesema #DeniLaTaifa limeongezeka kutoka trilioni 41 mpaka trilioni 46 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuzipatia hati chafu Halmashauri za Wilaya za Kigoma Ujiji na Pangani, rais John Magufuli amewasimamisha kazi wakurugenzi wa Halmashauri hizo ili kupisha uchunguzi.

Wakurugenzi waliosimamishwa ni Boniface Nyambe (Kigoma Ujiji) na Daud Mlahagwa (Pangani) ambao halmashauri zao zimebainika kuwa na madudu katika hesabu zao za serikali za mitaa.

Uamuzi huo umefikiwa leo wakati rais Magufuli akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof.  Mussa Hassad ambaye amebaini mambo mbalimbali kwenye hesabu za manunuzi na matumizi ya mashirika ya umma, serikali za mitaa na serikali kuu ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho.

Rais Magufuli alisema wamepokea ripoti ya CAG na wanaifanyia kazi ikiwemo kutoa adhabu kwa wale wote waliohusika na udhadhilifu wa mali ya umma na kuwakosesha wananchi huduma muhimu za kijamii katika maeneo yao.

“Moja ya Halmashauri zenye hati chafu ni Kigoma Ujiji na huo ni mfano tu. Naagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote zenye hati chafu wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi”, alisema Rais na kuongeza kuwa,

“Tusipoanza kuchukua hatua hatutafika, inawezekana isiwe nzuri sana nafikiri tuanze tuwe tunachukua hatua”.

Hata hivyo rais hakutaja Halmashauri zote zenye hati chafu lakini amesema wakurugenzi katika wilaya hiyo wasimamishwe na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya rais, CAG Prof. Assad amesema baadhi ya halmashauri zilishindwa kukusanya mapato kama inavyotakiwa na nyingine hazikuwasilisha vitabu vya mahesabu. Ameibainisha kuwa serikali za mitaa 140 zilishindwa kukusanya mapato ya sh. 116 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 22 ya mapato yote yaliyotakiwa kukusanywa.

“Zaidi ya hapo tuliona mawakala kutowasilisha sh. 3.5 bilioni ya makusanyo lakini hawakuwasilisha ni usimamizi tu mbovu wa halmashauri kwani kama mawakala wamekusanya kwanini usikusanye mapato yako?”, alisema CAG.

Ameongeza  kuwa katika uchunguzi wao walibaini upotevu wa vitabu 379 vya mapato ya serikali ambapo haikujulikana ni kiasi gani cha fedha kimepotea kutokana na upotevu wa fedha hizo.

“Kitabu cha mapato kisipokuja kwetu hatuwezi kujua ni kiasi gani kimetumika katika vitabu hivyo, lakini tuliona katika halmashauri za Biharamulo, Karagwe na Mpwapwa kulikuwa na miradi mitatu ambayo thamani yake ilifikia sh. 1.6 bilioni iliyochelewesha kukamilishwa”, alifafanua CAG.

Hata hivyo amesema baadhi ya fedha ambazo zilitakiwa zitoke hazina na kupelekwa kwenye halmashauri hazikufika ambapo hali hiyo ilikuwa changamoto katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii kwenye serikali za mitaa.

“Serikali za Mitaa zinazofika 146 hazikupata kiasi cha Tshs bilioni 582 ambazo ni asilimia 15 ya bajeti yote ya Serikali za Mitaa.Kiasi kikipangwa kifike ili Serikali za Mitaa ziweze kufanya kazi zake”, alibainisha CAG.

Wakati huo huo, ripoti ya CAG inaeleza kuwa kuna mabadiliko ya ongezeko la hati safi ukilinganisha na miaka iliyopita ambapo mashirika ya umma yamepata asilimia 96, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) 90%. Lakini kwa serikali kuu ni 80% ambapo imeshuka kutokana na baadhi ya madudu yaliyotokana na vyama vya siasa.

                   Rais John Magufuli akipokea ripoti kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad

 

CAG aonya ongezeko deni la taifa.

Kwa upande mwingine, CAG Assad amesema deni la taifa linaongezeka kwa kasi na kuleta wasiwasi na serikali inapaswa kuchukua hatua ili kupunguza ukubwa wa deni hilo licha ya kuwa ni himilivu.

Amesema deni la taifa limefikia sh. 46 trilioni kutoka sh. 41 trilioni mwaka jana ambapo ni ongezeko la asilimia 12 ndani ya mwaka mmoja tu.

“Tulichosema hapa kwa kweli ukuaji wa deni tunasema ni himilivu lakini jinsi linavyoongezeka tunafikia maeneo ya wasiwasi. Asilimia 72 ya GDP (Pato la taifa) sio mbaya lakini ikifikia asilimia 76 nchi nyingine zimepata shida, inabidi tuangalie namna gani tunaweza ku-control ukuaji wa deni hilo”, aalisema CAG.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2018/19, deni la Serikali limefikia sh. 47.7 trilioni ikilinganishwa na dola za Marekani 19,957 milioni Juni, 2016 ambapo ni sawa na kusema deni hilo limeongezeka maradufu katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu kuingia madarakani kwa serikali ya rais John Magufuli.

Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni sh. 34.1 trilioni, ikiwa ni asilimia 71.5 ya deni lote ambapo deni la ndani lilikuwa sh. 13.6 trilioni sawa na asilimia 28.5 ya deni lote.

Akieleza sababu ya kuongezeka kwa deni la taifa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema,  “Ongezeko la deni kwa kipindi cha Juni 2016 hadi Desemba, 2017 lilitokana na mikopo mipya na mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji fedha (exchange rate fluctuations)”.

 Hata hivyo, serikali ilisema uwiano wa deni la ndani na nje kwa Pato la Taifa kwa mwaka 2017/18 ni asilimia 34.4 ikinganishwa na ukomo wa asilimia 56, hivyo deni bado lipo chini ya kiwango cha hatari na uwezo wa kulipa deni bado ni imara.

 

Mapendekezo ya Kamati za Bunge

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Dkt. Raphael Chegeni amesema  amelalamikia kitendo cha ofisi ya msajili wa hazina kuwa na watendaji wanaokaimu nafasi zao, na kupendekeza ipate watendaji wenye sifa na wenye uwezo wa kusimamia ofisi hiyo na kuhakikisha fedha zinapelekwa kwa wakati kwenye miradi ya maendeleo.

 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia ameitaka serikali kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na ubadhirifu wa mali ya umma. Pia mfuko wa mahakama uongezewe nguvu ili  kushughulikia kesi za watumishi waliohusika na ufisadi.

 Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ripoti ya CAG inatoa matumaini na imeonyesha mapungufu katika utendaji wa serikali na kwamba watafanyia kazi ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati za Bunge na CAG.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *