Chadema yaongoza Arumeru, yashinda Kirumba, matokeo rasmi bado

Jamii Africa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kupitia mgombea wake Joshua Nasari, kinaongoza katika vituo vingi katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, huku mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Siyoi Sumari, akimfuatia.

Joshua Nasari

Katika matokeo ambayo yanamiminika katika mtandao wa Jamiiforums.com, Chadema wanaiacha CCM kwa tofauti kubwa katika vituo vingi, huku chama hicho tawala kikiongoza katika baadhi ya vituo kwa tofauti ndogo.

Hali kama hiyo imejitokeza pia katika matokeo ya viti vya udiwani katika kata zilizofanya uchaguzi huo leo Jumapili Aprili mosi, 2012.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, Kata ya Kirumba CHADEMA wamepata kura 2938 na CCM 2131. “Tunapenda kutangaza rasmi kwamba tumeshinda Udiwani kata hii na kuendelea kulishika Jiji la Mwanza,” anaeleza Zitto. Hata hivyo, lolote linaweza kutokea kutokana na kuendelea kumiminika kwa matokeo kutoka maeneo ya vijijini.

Tutaendelea kuwaletea taarifa kadiri zinavyotufikia.

 

Kampeni za uchaguzi huo hizo zilianza Machi 9, mwaka huu zilijaa kila aina ya vituko, vibweka na matukio ya kuvutia kutoka kwa wagombea, viongozi, wapambe na wafuasi wa vyama husika.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Sumari, aliyefariki dunia Januari 18, mwaka huu.

Licha ya kuwapo kwa vyama hivyo vinane, mchuano mkali unatarajiwa kuwa baina ya Sioi Sumari (CCM) na Joshua Nassari (CHADEMA), ambapo vigogo wa vyama hivyo viwili walishiriki kikamilifu kuwanadi wagombea hao.

Vyama vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi huo ni TLP, CCM, CHADEMA, Chama cha wakulima (AFP), NRA, SAU, DP na UPDP.

 

7 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *