Dar es Salaam kushika mkia matokeo kidato cha nne, tathmini inahitajika

Jamii Africa

MKOA wa Dar es Salaam kuwa na shule 6 kati ya 10 ambazo wanafunzi wake wamefanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2016, ni agenda iliyotawala vyombo vya Habari na jamii wakihoji nini kimeukumbuka mkoa huo.

Shule sita kati ya 10 zilizoshika mkia zimetokea mkoani Dar es Salaam ambazo ni Kitonga, Nyeburu, Mbopo, Mbondole, Somangila Day na Kidete. Shule nyingine katika orodha ya 10 mbovu ni Masaki iliyoko mkoani Pwani, Dahani iliyoko mkoani Kilimanjaro, Ruponda mkoani Lindi na Makiba mkoani Arusha.

Kwa bahati mbaya ni kwamba, shule zote 6 katika orodha ya 10 mbovu kutoka Dar es Salaam zinamilikiwa na serikali, ambapo Kitonga, Mbondole na Nyeburu ziko Wilaya ya Ilala, Kidete na Somangila (Temeke) na Mbopo (Kinondoni).

Nini kimeikumba Dar es Salaam kufanya vibaya katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne? Ni swali ambalo wadau wa elimu wanajiuliza kwa sababu mkoa huo unaaminika kuwa na miundombinu bora ya kijamii kwa ujumla kuliko maeneo mengine nchini.  

Katika matokeo ya mwaka 2015 Dar es Salaam ilikuwa na shule moja kati ya shule 10 zilizofanya vibaya. Shule hizo zilikuwa Saviak (Dar es Salaam), Pande (Lindi), Igawa (Morogoro), Korona (Arusha), Sofi (Morogoro), Kurui (Pwani), Patema (Tanga), Gubalk (Dodoma), Kichangani na Malinyi (Morogoro). Morogoro ilitia fola kwa kuwa na shule 3.

Lakini kutoka kuwa na shule moja mwaka 2015 hadi kufikia shule 6 ni matokeo mabaya ambayo kwa kumbukumbu za haraka hayajawahi kutokea mkoani Dar es Salaam.

FikraPevu inaamini ongezeko la shule tano safari hii ni kubwa na linaonyesha hatari iliyopo kwa mkoa huo ‘kumiliki’ orodha yote ya shule zenye matokeo mabovu ikiwa juhudi za makusudi hazitafanyika.

Nani anayeweza kutafsiri maendeleo ya elimu nchini ikiwa ubora wa elimu unashuka kila mwaka hata katika shule za mijini ukilinganisha na shule za vijijini ambazo zinakabiliwa na changamoto mbalimbali?

Licha ya kutokuwemo kwenye orodha ya ‘shule mbovu 10’ safari hii, matokeo ya Saviak hayana nafuu wala afadhali, kwani kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) 2016 ni wanafunzi sita tu ambao safari hii ‘wamefaulu’ kwa kupata daraja la 4 kati ya wanafunzi 23 waliofanya mtihani huku wanafunzi watano wakipata daraja 0 na 12 matokeo yao yalizuiliwa.

FikraPevu imebaini kwamba, shule 6 za Dar es Salaam ambazo zimeleta gumzo, anguko lake lilianzia miaka mitatu nyuma kwa sababu zimekuwa hazifanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne.

Mathalani shule ya Mbopo ambayo mwaka 2016 ilikuwa na wanafunzi 126 waliojiandikisha lakini waliofanya mitihani ni 123 na waliofaulu ni 21 pekee ambapo watatu wamepata daraja la III na 18 daraja la IV na waliofeli ni 102. Kitaifa ilikuwa shule ya 3,277 kati ya shule 3,280.

Matokeo hayo hayatofautiani na ya 2015 ambapo wanafunzi 115 walifanya mtihani, 40 waliofaulu kwa kupata daraja la nne pekee, huku 50 wakifeli na 25 wakifutiwa matokeo yao. Mwaka 2015 shule hiyo ilishika nafasi ya 3,287 kitaifa kati ya shule 3,452.

Shule ya Nyeburu, kama zilivyo nyingine za pembezoni, iko katika hali mbaya, mwaka 2016 ilishika nafasi ya 3,279 kati ya shule 3,280, ambapo wanafunzi 108 walifeli na 19 walifaulu kwa kupata daraja la IV. Na matokeo yake hayatofautiani na ya 2015 ambapo ilishika nafasi ya 3,329 kitaifa kati ya shule 3,452.

Shule hizo zinawakilisha shule nyingine ambazo hazijatajwa katika orodha ya shule zilizofanya vibaya na matokeo yake hayatofautiani na shule nyingine nchini ambazo ufaulu wake uko chini ambapo wanafunzi wengi wamepata daraja la IV na 0.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde amesema: “Watahiniwa wa shule wenye ufaulu mzuri wa daraja la kwanza hadi la tatu ni 96,018 sawa na asilimia 27.60, waliopata daraja la nne ni 143,744 (42.75%) na waliofeli kabisa ni 103,154 (25.55%).”

Hayo ni matokeo mabaya licha ya ufaulu kupanda kwa asilimia 2.56 kutoka asilimia 67.53 mwaka 2015 hadi 70.09% mwaka 2016.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, shule hizo sita ziko nje ya Jiji la Dar es Salaam ambapo huwalazimu wanafunzi na walimu kusafiri umbali mrefu kuhudhuria masomo.

Kwa matokeo hayo ya mwaka 2015 na 2016 kuna hatari shule hizo kuendelea kufanya vibaya katika masomo ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa na kutatua changamoto zilizopo.

Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa asasi ya kiraia ya HakiElimu, Godfrey Boniventura, akizungumza na chombo kimoja cha habari hapa nchini alisema: “Kama changamoto hizi hazitaboreshwa, ufaulu katika shule za pembezoni utakuwa ni ndoto.’’

Anashauri Serikali kutenga bajeti ya kutosha na kuhakikisha inasogeza huduma za jamii na kuboresha miundombinu katika maeneo karibu na shule zilizopo pembezoni ili kutoa ahueni kwa wanafunzi na walimu hao.

“Mwalimu huyu ambaye tangu anaanza shule ya msingi anasoma katika shule na vyuo binafsi huku akiwa anapata huduma muhimu kwa urahisi, anapangiwa kwenda kufundisha shule ambayo kupata dawa ya kupigia mswaki inampasa kutembea kilomita 20. Kwa hali hii, hakuna mwalimu anayeweza kuhimili haya,” anasema Boniventura.

Matokeo haya mabovu katika shule 6 yanaweza kuakisi hali halisi ya elimu katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ubora wake unashuka kila mwaka ukilinganisha na mikoa mingine ya Tanzania ambayo inafanya vizuri licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu ya shule, barabara, na usafiri.

Takwimu za NECTA (2016) zinaiweka Dar es Salaam katika nafasi ya 18 kati ya mikoa 31 katika ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne 2016 ambapo mwaka 2015 ilishika nafasi ya 15.

Ndani ya mwaka mmoja mkoa umeshuka kwa nafasi 3 na hali hii inaweza kuendelea miaka ijayo kama hatua stahiki hazijachukuliwa.

Pia wilaya tatu za Dar es Salaam zimepitwa na wilaya za pembezoni mwa nchi ambazo zimefanya vizuri na kuzipita kwa mbali wilaya hizo za jiji. Wilaya za Mkulanga, Kibaha, Ilemela, Njombe, Kahama, Wanging’ombe, Igunga, Kakonko, Iringa na Bukoba ziko kwenye 10 bora za ufaulu.

Kwa mujibu wa takwimu za NECTA (2016) Wilaya ya Temeke imeshika nafasi ya 137 kati ya wilaya 178 ambapo mwaka 2015 ilikuwa ya 105, ufaulu wake umeshuka kwa nafasi 35.

Wilaya ya Ilala imeshika nafasi ya 84 kati ya Wilaya 178 ambapo imeshuka kwa nafasi 47 ikilinganishwa na 2015 iliposhika nafasi ya 37.

Kwa upande wa Kinondoni imekuwa ya 63 ikilinganishwa na nafasi ya 29 iliyokuwepo mwaka 2015 na imetoa shule moja ya Mbopo kati ya 10 zilizofanya vibaya.

Wadau wa elimu Mkoa wa Dar es Salaam hawana budi kufanya tathmini ya kina na kutatua changamoto mbalimbali za elimu hasa kwa shule zilizo pembezoni ili kuongeza kiwango cha ufanisi katika masomo, ikiwemo kuajiri walimu wa kutosha na kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufundishia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Usimamizi wa Elimu wa Ofisi ya Rais-Tamisemi, Juma Kaponda, anasema Serikali inafanya tathmini na kuzifanyia kazi changamoto na kuinua kiwango cha elimu na mwaka huu inatarajia kuajiri walimu 10,169 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa shule za sekondari ambao wengi wataelekezwa katika shule za pembezoni.

“Hawa walimu safari hii hawatapelekwa kwenye halmashauri, bali watapangiwa moja kwa moja vituo vya kazi kutoka wizarani; lengo ni kupunguza uhaba katika shule zetu,” alisema Kaponda.

Anaongeza: “Halmashauri pia zinatakiwa kuhakikisha zinagawanya walimu kutoka maeneo ambayo yana ziada na kupeleka maeneo yenye upungufu.”

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *