Elimu Bure: Nkasi yaandikisha watoto 20,000, yahitaji vyumba vipya 1,192

Jamii Africa

Wanafunzi wa shule ya msingi Misunkumilo wilayani Nkasi wakisoma kwenye darasa lililoezekwa kwa turubai. (Picha kwa hisani ya HakiElimu).

 

WAKATI jumla ya watoto 20,000 wameandikishwa katika darasa la awali na la kwanza wilayani Nkasi, mkoani Rukwa Januari 2017, wilaya hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa 1,192, FikraPevu imebaini.

Uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, kwa sasa wilaya hiyo ina vyumba 650 tu kati ya mahitaji ya vyumba 1,842 vya shule za vijiji 99 pamoja na halmashauri ya Mji wa Nkasi.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Said Mtanda, amesema kwamba, kasi ya ongezeko la kuandikishwa kwa watoto imechochewa na uamuzi wa serikali wa mpango wa elimu bure ya msingi hadi kidato cha nne.

“Hadi sasa Wilaya ya Nkasi imeandikisha wanafunzi wa darasa la awali 9,000 kati ya maoteo ya watoto 11,000 na darasa la kwanza 11,000 kati ya maoteo 14,000,” alisema DC Mtanda katika taarifa yake.

Hata hivyo, amesema wamejipanga vyema kukabiliana na changamoto hiyo kubwa inayotokana na Elimu Bure na kwamba juhudi za maofisa tarafa, watendaji kata, vijiji, na wenyeviti itasaidia kupatikana kwa vyumba vipya kati ya 250-300 katika mwaka huu.

Hapa ni katika shule ya msingi ya Itete iliyopo wilaya ya Nkasi.

Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kwamba, katika bajeti ya mwaka 2017/2018 wataweka mpango wa ujenzi wa vyumba zaidi ya 50 ambapo kwa sasa wananchi wa vijiji 99 wamehamasishwa na tayari vijiji 90 vina akiba ya matofali ya kutosha na akasema fedha asilimia 20 zinazotokana na makusanyo ya halmashauri zimeelekezwa kujenga madarasa kwa kila kijiji.

“Tumeamua na tumeanza kutekeleza mpango wa wilaya wa kujenga vyumba vitatu vya madarasa kati ya sasa hadi Machi 31, 2017 ambayo ni tarehe ya mwisho ya kupokea watoto wa darasa la kwanza,” alisema.

Licha ya hali ya kilimo kusuasua kwa sasa, lakini amewapongeza wabunge wa wilaya hiyo – Desderius Mipata wa Nkasi Kaskazini na Ally Keisy Mabodi wa Nkasi Kusini – pamoja na wananchi kwa kuhamasika kwenye ujenzi wa madarasa mapya ambapo ziara na vikao vya uhamasishaji vimefanyika na kila kijiji kuhakikisha ujenzi wa vyumba vitatu unaanza mara moja.

“Nawashukuru wah wabunge wetu kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kutenga Shs. 30 milioni kwa ujumla kwa ajili ya kununua bati ili kusaidia juhudi za wananchi katika ujenzi wa madarasa,” alisema.

Fikra Pevu imebaini kwamba, kampuni moja ya ujenzi ya China inayojenga barabara ambayo imepiga kambi Paramawe na Kipande imeahidi kupeleka mchanga na kokoto katika Kata ya Paramawe, Nkole, Chala na Nkandasi ili kusaidia ujenzi huo.

Inaelezwa kwamba, Wachina hao tayari wamekwishapeleka mchanga na kokoto za kutosha kusaidia ujenzi wa shule ya sekondari ya Kasu, ambao unaendelea.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *