Elimu bure ‘yawahenyesha’ walimu Tarime, wakwama kufundisha

Jamii Africa

SHULE za msingi wilayani Tarime, zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa walimu, kiasi cha wanafunzi kushindwa kufundishwa vipindi vyote.

Uhaba huo umejitokeza, huku kundi kubwa la wahitimu wa ualimu nchini, likiwa mtaani kusubiri ajira.

Kutokana na uhaba huo wa walimu, mwalimu mmoja anajikuta akifundisha vipindi vinane kwa siku, sawa vipindi 40 kwa wiki.

Pamoja na kufunidisha vipindi vyote hivyo, mwalimu mmoja amekuwa akifundisha darasa lenye wanafunzi kati ya 100 na 200, kinyume cha sera na taratibu za kawaida ambapo anapaswa kufundisha wanafunzi 45 darasani.

Wanafunzi wa darasa la tatu 164 Shule ya Msingi Nyabusara, Kijiji cha Murito, Kata ya Kemambo-Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara wakiwa wamerundikana darasani kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.​

Ukubwa huo wa kazi, unaelezwa unachangia kuzorota kwa ubora wa elimu wilayani humo, huku baadhi ya walimu wakikosa hamasa ya kuendelea kufundisha.

Chanzo cha upungufu

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Murito, Abdalah Ntire, akiwa kwenye ofisi yake ambayo haijakamilika ujenzi. Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2013 kwa nguvu za wananchi.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa  tatizo la upungufu wa walimu limechangiwa na serikali kusitisha ajira za ualimu tangu mwaka 2016, huku ikianzisha utaratibu wa elimu bure kwa kila mtoto nchini.

Uchache wa walimu na madarasa, kwa upande mwingine umekuwa ukichangia utoro kwa wanafunzi, kwenye kujishughulisha na masuala mengine nje ya maeneo la shule.

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kuwa licha yakuwa Serikali imetoa elimu bure kwa wanafunzi bado ni changamoto kwakuwa haikuboresha mazingira rafiki kwa wanafunzi  hususani madarasa, vitabu, nyumba za walimu na vitendea kazi.

Katika Shule ya Msingi Nyabusara Kata ya kemambo-Nyamongo, ni jambo la kawaida kuingia darasani na kukuta darasa moja likiwa na wanafunzi 164.

FikraPevu ilishuhudia msongamano huo wa wanafunzi wakikaa  chini karibu na ubao kwakuwa hakuna nafasi ya kuweka madawati licha yakuwa kuna madawati ya kutosha.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyabusara Kijiji cha Murito Sijali Ngangambe anasema shule yake ina wanafunzi 1,001  na walimu 9.

“Mwalimu mmoja anafundihsa vipindi 35-40 kwa wiki. Madarasa hayatoshi. Darasa la kwanza lina wanafunzi 131, la pili 263, la tatu 164 na la nne ni 140.  Wanatakiwa kukaa  40-45, tuna upungufu wa vitabu vya historia, uraia na jiografia. Matundu ya choo yako 10 tu wakati yanatakiwa kuwa 43. Hakuna kisima,’’ anasema.

Kama ilivyo katika Shule ya Msingi Nyabusara, uhaba wa walimu na msongamano wa wanafunzi pia unazikabili shule za Nyamongo (1,225), Kewanja (1,315) na Nyabigena (1,091), Nyangoto 1,319 na Matare 1,288.

Wajumbe wa kamati za shule

Wanafunzi wa shule ya msingi Kewanja wakiwa mstarini.

Mjumbe wa Kamati ya shule ya msingi Kenyangi, Stephano Mrimi amiambia FikraPevu kuwa kitendo cha wazazi kutokuhudhurii mikutano kimekuwa kikizorotesha maendeleo ya kitaaluma.

Mwenyekiti wa kijiji cha Murito  Zephania Mahati  anasema kuwa, kutokana na  kijiji hicho kuwa na vitongoji 11, kilipaswa kuongezewa shule, lakini siasa ndiyo imekwamisha maendeleo.

Naye mwanafunzi wa shule ya Matongo, Ghati  Chacha ameiambia FikraPevu kuwa  tatizo la upungufu wa walimu unasababisha wasisome vipindi vyote kulingana na ratiba iliyopangwa, hivyo kutoa fursa kwa wanafunzi kutoroka.

Kwa kutambua umuhimu wa elimu, kila kaya katika kijiji cha Nyabichune imechanga 20,000 kwa ajili ya ujenzi, ambapo tayari madarasa manne yamejengwa hadi usawa wa renta kwa ajili ya shule mpya ya Kwihore.

Uhaba wa vifaa, miundombinu

Nyumba za walimu shule ya msingi Nyabigena Kata ya Kemambo.

Mratibu wa Elimu Kata ya Matongo, Hermes Rugeyasira  anasema kata hiyo yenye shule sita za msingi ina ya wanafunzi 5,244  na walimu 74, wakati mahitaji yakiwa ni walimu 131.

Kata hiyo pia ina vyumba vya madarasa  61 kati ya madarasa 131 yanayotakiwa.

Aidha, inakabiliwa na uhaba wa vitabu vya mtaala mpya vya masomo yote isipokuwa kwa darasa la kwanza na la pili.

Afisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Emanuel  Johnson ameiambia FikraPevu kuwa halmashauri ina shule za msing 116, wanafunzi  81,529, walimu 1,275 na vyumba vya madarasa 677, huku mahitaji yakiwa vyumba 1,504, hali inayosababisha darasa moja kuwa na wanafunzi wengi.

‘’Tukishakamilisha uandikishaji wa wanafunzi darasa la kwanza Machi 28, ndipo tutajua mahitaji kamili ya walimu, maana uhitaji wa walimu tunaupata kutokana na idadi ya wanafunzi iliyopo. Kutokufundishwa vipindi vyote, kunamfanya mwanafunzi awe mtoro. Akisoma kwenye ratiba na akijua kipindi hicho mwalimu hayupo au hajaingia darasani, anatoroka,’’ ameieleza FikraPevu.

Anaongeza: “Mwongozo wa elimu umeleta mkanganyiko kwa wananchi wakiamini hawapaswi kuchangia. Halmashauri yenyewe inasaidia baada ya wananchi kujenga majengo,’’ anasema.

Johnson anasema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa walimu wanaodai madeni yao, jambo linalowaweka kwenye msongo wa mawazo na kutokuwa na hari nzuri katika ufundishaji.

 Johnson abainisha kuwa walimu wanaidai serikali fedha za likizo kiasi cha shilingi milioni 86.9, uhamishi milioni 85.1, usimamizi wa mitihani milioni 46.

Anasema  kuwa  kwa mwaka wa fedha 2015/2016 halmashauri  ilipokea fedha za uendeshaji (Capitation) milioni 256,784,000/- kati ya milioni 363,834,000.00 zilizohidhinishwa.

Fedha hizo zinazodaiwa kuwa hazitoshelezi mahitaji, zimekuwa zikitolewa kwa kuzingatia idadi ya wanafunzi wa mwaka wa fedha uliotangulia, huku wanafunzi wapya wakiandikishwa Januari ya kila mwaka.

Halmashauri yatoa fedha

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Apoo Tindwa, ameiambia FikraPevu kuwa halmashauri hiyo ilitoa Sh. milioni 450 kukarabati shule za msingi 61 zilizojengwa kwa nguvu za wananchi na kwamba halmashauri haina upungufu wa madawati.

Mkurugenzi anasema halmashauri ilitengeneza madawati 1,800, wakati yaliyokuwa yakihitajika ni madawati 1,500.

Mkaguzi wa shule  za msingi wilayani Tarime, Joseph Mowinga anasema kuwa shule inapaswa kukaguliwa kila mwaka lakini wanashindwa kutokana na fedha kidogo wanayoipokea kutoka Serikalini  na hivyo  shule kuka zaidi ya miaka mitano  bila kukaguliwa.

Mowinga anasema kuwa tatizo la ukosefu wa pesa ni changamoto ambapo upokea kati ya milioni 1 hadi 2 za uendeshaji mzima wa ukaguzi zikiwepo pesa za mafuta,uchapishaji,Posho za kujikimu kwa wakaguzi wanapokwenda  shule za mbali za mafuta ni changamoto.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *