Elimu kwa mtoto wa kike bado ni changamoto

Jamii Africa

ELIMU ni haki ya kila mtoto. Haibagui wala haigombi, inapotolewa kwa msichana ama mvulana.

Uelewa ukiwekwa kwa watoto, hautagoma “kuishi” kichwani kwa msichana au mvulana. Utadumu na kuwa msaada mkubwa kwa wale wanaoupokea bila kujali jinsi zao.

Hata hivyo, jamii nyingi, hasa za Afrika – Tanzania ikiwamo, pamoja na umuhimu wake, watoto wa kike(wasichana) wamekuwa wakibaguliwa na familia, jamii na hata nchi wanamoishi katika kupata elimu.

Mtoto wa kike, akiwa na uwezo sawa wa kupokea elimu, kama ilivyo kwa wa kiume, amekuwa akikosa fursa ya kuipata kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikitajwa kuwa mila na umasikini.

Katika Tanzania, mifano ya watoto kukosa elimu kwa sababu ya umasikini au kugubikwa na mila zinazoweza kutajwa kuwa ni potofu ni mingi, lakini mmojawapo ni wa Veronica Marko.

Veronica, akiwa binti wa miaka 17 (wakati huo, mwaka 2013) akizungumza na Redio ya Umoja wa Mataifa(Radio ya UM) kupitia Afya Radio ya Jijini Mwanza, analia kwa kukosa elimu, licha ya kuchaguliwa kuendelea na  elimu ya sekondari.

Kilio cha mtoto huyo wa kike, Veronica kinaeleza machungu wanayokumbana nayo wasichana wengi kwa kukosa elimu kwakuwa tu wanakutana na changamoto nyingi, ikiwamo umasikini na mila.

Mkurugenzi wa Shirika la Wote Sawa la jijini Mwanza, Angela Benedicto anaeleza madhila ya mtoto wa kike kukosa elimu, huku akilaumu baadhi ya mila na umaskini kuwa chanzo kikubwa.

“Jamii ikiachana na mila potofu, kwamba watoto wa kike kazi yao duniani ni kuwa walezi wa watoto na watumishi wa jikoni, Tanzania itasonga mbele Zaidi, kwani maendeleo yote makubwa hutegemea uimara wa mwanamke,” anasema Angela.

angel_benedicto_fp

Angela ambaye alikimbia kuolewa, baada ya kulazimishwa na baba yake, ili mzazi apate mahari, hivi sasa ni mtetezi mkubwa wa wasichana na anaiasa jamii kuthamini elimu kwa watoto wa kike, ikiwa inataka “maendeleo makubwa na endelevu.”

Akizungumza na FikraPevu, Waziri wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema Serikali ya Rais John Magufuli imeweka mkakati kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa sawa ya elimu kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

“Tanzania hatuna ubaguzi katika elimu, ndiyo maana tumeamua kuwa na elimu bure kwa watoto wote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, hatuangalii msichana wala mvulana, wote wanaipata,” anasema Waziri Ummy.

Waziri Ummy alinukuliwa Bungeni akisisitiza wote watakaobainika kuwapa mimba wanafunzi wakamatwe na kufikishwa mahakamani haraka sana. Ni kauli inayoshabihiana na kauli iliyowahi kutolewa na Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Seriklali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo

Mwanaharakati wa Elimu kwa Wasichana, Jacqueline Kulwah, ameiambia FikraPevu kwamba watoto wa kike wana uwezo mkubwa darasani, hivyo ni vyema wananchi wakahimizwa kuhakikisha wanawapa elimu ili iwe chachu ya kuwepo kwa maendeleo ya uhakika nchini.

Jacqueline anabainisha kuwa takwimu zinaonesha kuwa watoto wa kike, kwa miaka mitatu mfululizo wameibuka kuwa vinara wa matokeo ya kidato cha nne nchini kuanzia mwaka 2013 hadi 2015.

Katika matokeo ya kidato cha nne, aliyeongoza kwa ushindi mwaka 2013 alikuwa Robina Nicholaus kutoka shule ya Marian, Dar es Salaam. Mwaka uliofuatia – 2014, aliyeongoza alikuwa Nyakaho Marungu wa shule ya Baobab, huku aliyeongoza mwaka 2015, akiwa ni Butogwa Charles kutoka shule ya Canossa ya Dar es Salaam.

Ni kutokana na matokeo haya, inawezekana kabisa dunia ikathibitisha kwamba watoto wa kike wana uelewa mkubwa zaidi wa kupambanua mambo kielimu, kuliko wavulana.

Mapema mwaka huu, Kashmea Wahi, msichana mdogo wa umri wa miaka 11, alitajwa kuwa na uelewa mkubwa wa mambo kuliko watu wote duniani; walio hai na hata waliofariki dunia.

kashmea_wahi

Kashmea, Muingereza mwenye asili ya India naelezwa kuwa na utambuzi wa mambo mengi na akili yenye kufanya kazi kwa haraka (IQ), tena akiwa na umri mdogo. Anatajwa na Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza kuwa “msichana mdogo mwenye uwezo mkubwa wa akili na upembuzi wa haraka wa majibu ya maswali magumu.”

Hata hivyo, pamoja na kuthibitika mtoto wa kike kuwa na uwezo mkubwa kupambanua mazingira alimo, anakabiliwa na changamoto nyingi.

Kama wanavyobainisha Veronica na Angela, jamii imekuwa ikimuona mtoto wa kuwa ni kiumbe dhaifu, asiyeweza kujitegemea, kujipigania au hata kujilinda. Lakini kwa uthibitisho wa takwimu, msichana anaweza kukabili yanayomkwamisha ikiwa anapata elimu.

Ni kutokana na umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike kutikiswa na kutishwa kwa namna moja au nyingine, serikali, taasisi, mashirika na hata watu binafsi, wamekuwa wakijitahidi kunusuru “anguko la elimu” kwa wasichana.

Rais wa awamu ya pili Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, kwa kutambua changamoto zilizokuwa zikiwakabili watoto wa kike wa Kabila la Wamasai, alitoa ardhi na kuhimiza ujenzi wa shule ya kwanza ya wasichana iliyokuwa ikipokea watoto wa Kimasai.

Leo, shule hiyo ikiwa na miaka 21, imeweza “kuzalisha” walimu zaidi ya 250, wanasheria tisa, daktari mmoja na mhandisi mmoja na kuwa mwanga kwa wasichana wengi wa jamii hiyo iliyokuwa imekumbatia mila zinazokwamisha elimu kwa watoto wa kike.

Ni kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa wasichana, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetenga dola za Marekani 1,605,000 (zaidi ya Sh. bilioni 3) ili zitumike kusaidia watoto wa kike nchini kurejea shuleni.

Mkuu wa UNESCO nchini, Zulmira Rodriguez anasema Tanzania bado inaonekana kuwa na tatizo la watoto wa kike kuachishwa masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kupata mimba za utoto na ndoa za utotoni hivyo kupitia mradi huo wataweza kuwasaidia watoto hao kuendelea na masomo.

UNESCO imeahidi kuendelea na misaada yake ikiwa ni njia ya kusaidia elimu kwa watoto wa kike wa Tanzania.

Madhila kwa watoto wa kike, hasa kwa kunyimwa au kukatishwa haki ya elimu, hakujaiathiri Tanzania pekee, bali nchi nyingi masikini, hasa za Afrika.

Ripoti ya Shirika la Save the Children mwaka huu – 2016, inaonesha kuwa nchi tano; Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali, Somalia na Niger, zina mazingira mabaya kwa elimu kwa watoto wa kike.

Sababu zinazotajwa na  shirika hilo, ni zilezile zinazowakabili wasichana wadogo wa Tanzania kuwa ni mimba za utotoni, mila mbaya, umasikini na ndoa za kulazimishwa.

Jitihada za wadau ikiwemo serikali na mashirika mbalimbali; Chama cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP), wameendelea kupambana na tatizo la mimba za utotoni kwa kutoa elimu na kupinga vitendo vyote vinavyohatarisha ustawi wa mwanamke katika jamii.

Hata hivyo, tatizo la mimba za utotoni bado ni changamoto kubwa kwa sababu idadi ya wasichana wanaopata mimba na kuacha masomo kila mwaka inaongezeka nchini.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 2.7 ya wasichana 597,000 wanaondikishwa katika shule za msingi Tanzania, ambao ni – watoto wa kike 16,119, hawamalizi masomo yao kwa sababu ya kupata mimba wakiwa shuleni, hivyo hulazimika kuacha masomo na kwenda kulea watoto.

Zipo sababu nyingine za  wasichana kukatiza masomo yao ikiwa ni pamoja; utoro, umbali mrefu kati ya shule na nyumbani, mazingira duni ya kujifunzia na kukosa elimu ya uzazi ambapo wasichana wanashindwa kutambua mabadiliko ya miili yao wakati wa kuvunja ungo.

baadhi-ya-walimu-katika-shule-ya-msingi-kidugalo-wakisahihisha-madaftari-ya-wanafunzi-nje-baada-ya-shule-hiyo-iliyoanzishwa-mwaka-2007-kukosa-ofisi-ya-walimu

Baadhi ya walimu katika shule ya msingi Kidugalo wakisahihisha madaftari ya wanafunzi nje baada ya shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 kukosa ofisi ya walimu

Changamoto hizi huwalazimisha wasichana kuingia katika tabia hatarishi na kujiingiza katika vitendo vya ngono na kusababisha kupata mimba.

Pia inaelezwa na wataalamu wa afya ya uzazi kwamba, pamoja na changamoto zingine za elimu kwa watoto wa kike, pia wengine hushindwa kuhudhuria masomo yao kutokana na kuingia katika hedhi. Inakadiriwa kuwa kati ya siku 186 na 187 kwa mwaka, wanafunzi wa kike hawafiki shuleni  kwa sababu ya matatizo ya hedhi. Wasichana wengi huanza kuingia hedhi wakiwa na miaka tisa hadi 12.

Takwimu za mwaka jana(2015) kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania zinaonesha kuwa mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni ni Shinyanga ambayo ina asilimia 59 ya ndoa za utotoni.

Mikoa mingine ni Tabora 58, Mara 55, Dodoma 51, Lindi 48, Mbeya 45, Morogoro 42, Singida 42, Rukwa 40, Ruvuma 39, Mwanza 37, Kagera 36, Mtwara 35, Manyara 34, Pwani 33, Tanga 29, Arusha 27, Kilimanjaro 27, Kigoma 29, Dar es salaam 19 na Iringa asilimia nane.

Katika hali yoyote, takwimu hizi zinaashiria kuendelea kuwepo kwa tishio kwa uhai wa elimu kwa wasichana, hivyo kuhitaji njia murua za kutokomeza ujinga kwa watoto hao.

Ni vyema sasa, kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike, kila mwananchi akawa balozi wa kuhimiza familia kufanikisha na kuhimiza kila mtoto wa kike anapata elimu.

1 Comment
  • Hakika elimu hii inaweza kuwa taa itakayoangaza ktk maixha ya vijana wengi xana na jamii kwa ujumla wake!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *