Ellen John-Sirleaf: Mapambano dhidi ya Ebola yalivyomtoa kimasomaso hadi kupata tuzo ya Uongozi bora Afrika

Jamii Africa

Hatimaye tuzo ya uongozi bora ya Afrika imechukuliwa na  Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf kutokana na  utawala bora, mageuzi ya kisiasa na uchumi aliyoyafanya akiwa madarakani.

Tuzo hiyo imetolewa na taasisi ya Mo Ibrahim mwaka 2017 kwa Rais Sirleaf ambaye alikuwa Rais wa kwanza mwanamke Afrika ambaye aliondoka madarakani Januari mwaka huu, baada ya kushuhudia uchaguzi wa kidemokrasia tangu Liberia ilipopata uhuru mwaka 1944.

Rais Sirleaf (79) aliingia madarakani mwaka 2006, miaka miwili baada ya kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo zaidi ya watu 250,000 waliuawa na wengine kuachwa bila makazi.

Katika vipindi vyake viwili vya uongozi (2006-2017) Sirleaf alifanikiwma kuimarisha uchumi, kurejesha uthabiti wa kisiasa, heshima ya mwanake na utawala bora unaozingatia uwazi na uwajibikaji katika ofisi za umma.

Kutokana na vigezo hivyo, kamati ya  tuzo ya Mo Ibrahim katika taarifa yake imesema inatambua baadhi ya mapungufu ya Rais  huyo lakini kwa kiasi kikubwa ameonesha uongozi wa kipekee katika kukabiliana na changamoto zilizotokea katika awamu mbili za uongozi wake.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema kilichomtofautisha Sirleaf na marais wengine wa Afrika ni uwezo wake wa kutatua matatizo ya msingi ya raia wake ambapo amepata heshima kubwa Afrika na duniani kote.

Akishirikiana na jumuiya za kimataifa aliwekeza nguvu kubwa ya kutokomeza ugonjwa wa Ebola ambao uliikumba nchi ya Liberia mwaka 2014 na 2015 na ulisababisha vifo vya watu wengi kwa muda mfupi.  Ugonjwa huo huenezwa na kirusi cha ebola (Ebola virus).

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za Januari 2016 zinaonyesha kuwa watu 11,315 walikufa kwa ugonjwa wa Ebola likijumuisha nchi za Afrika Magharibi na Marekani. Vifo vingi viliripotiwa nchini Liberia (4,809), Sierra Leone (3,955), Guinea Bisau (2,356) na Nigeria (8). Idadi hiyo ilipatikana kwa kuthibitisha, kuhisi na kukadiria.

WHO imeeleza kuwa huchukua siku mbili mpaka tatu kwa mtu kugundulika kuwa na ebola ambapo dalili za awali ni uchovu, homa, maumivu ya tumbo, kichwa, misuli, koo ambapo mgonjwa hupata kichefuchefu na baadaye huanza kutapika, kuharisha na kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo masikioni na puani.

Mapenzi mema kwa raia wake yalimnyima usingizi Sirleaf akihangaika huku na kule kuhakikisha ugonjwa huo unakomeshwa haraka ili kuokoa uchumi na  afya ya jamii. Madaktari zaidi ya 50 walisambazwa katika maeneo mbalimbali nchini humo, huku elimu ya kujikinga ilisambazwa kwa watu wote kupitia vyombo vya habari.

                       Wataalamu wa afya wamebeba mwili wa mtu aliyefariki kwa Ebola nchini Liberia

Ilipofika Mei 9, 2015, WHO ilitangaza kutokomeza maambukizi yote ya ebola nchini Liberia  ambapo ilishuhudia idadi kubwa ya wagonjwa na vifo tangu ugonjwa huo ulipozuka 1976. Katika kilele cha maambukizi ambacho kilitokea Agosti na Septemba 2014, kila wiki kesi 300 hadi 400 za ugonjwa ziliripotiwa nchini humo.

Wananchi walijitolea kufanya kazi kwenye vituo, kuzika, wengine kubeba wagonjwa. Walifanya hivyo kwasababu ya kuwajibika kwa jamii yao na uzalendo kutokomeza Ebola na kurudisha matumaini kwa watu wote. Vifo vilipozidi, jumuiya za kimataifa ziliingilia kati kusaidiana na serikali na walifanikiwa kupunguza vifo hadi sifuri.

Kutokomezwa kwa ugonjwa huo kulimpa heshima na kuaminiwa na wananchi wake kwa vile alivyojitoa kuwapunguzia mzigo wa maisha na kuhakikisha Liberia inakuwa salama wakati wote dhidi ya tishio lolote la kibinadamu.

Tuzo ya Mo Ibrahim ilianza kutolewa mwaka 2007 na viongozi wa Afrika walifanikiwa kuipata ni marais wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chisano, Festus Mogae wa Botswana (2008), Pedro Verona Pires wa Cape Verde (2011) na Hifikipunye Pohamba wa Namibia (2014).

 

Ellen Johnson Sirleaf ni nani?

Ellen Johnson-Sirleaf alizaliwa 29 Oktoba 1938 nchini Liberia na alikuwa Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika baada ya kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2005. Johnson-Sirleaf ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini na katika mashirika ya kimataifa.

                              Rais mstaafu wa Liberia, Ellen Johnson-Sirleaf aliyeongoza nchi hiyo tangu mwaka 2006

Baada ya kumaliza masomo katika chuo kikuu cha Harvard, alifanya kazi katika serikali ya Rais William Tolbert mwaka wa 1970 akiwa ni Waziri wa Fedha. Johnson-Sirleaf alihukumiwa kifungo cha miaka kumi jela mwaka 1985 baada ya kushutumu utawala wa kijeshi nchini humo katika kampeni zake za kugombea ubunge. Alitumia kifungo hicho kwa muda mfupi kabla ya kuachiliwa na baadaye kukimbilia uhamishoni hadi aliporudi mwaka 1997 akiwa anafanyia kazi Benki ya Dunia na Citibank.

Johnson-Sirleaf alimuunga mkono Charles Taylor wakati wa mapinduzi yake dhidi ya Jenerali Samuel Doe lakini baadaye alikuja kuwa mpinzani wake mkubwa na hata kugombea urais dhidi yake mwaka 1997. Taylor alimwandama na hata kumpeleka mahakamani kwa madai ya kuhusika na hujuma za kihaini.

Hata hivyo, John-Sirleaf hakuchoka aliendelea kupigania ndoto yake na mwaka 2005 baada ya kipindi cha miaka 14 ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe aligombea nafasi ya urais akishindana na mpinzania wake George Weah ambaye ndiye Rais wa sasa wa Liberia.

Uchaguzi wa urais mwaka 2005 ulirudiwa baada wagombea urais kutopata kura za kutosha. Katika raundi ya kwanza Johnson-Sirleaf alikuwa wa pili, wa kwanza alikuwa ni mpinzani wake mkubwa George Weah. Katika raundi ya pili ya uchaguzi, Johnson-Sirleaf alitangazwa kuwa mshindi na kufanikiwa kuitawala Liberia kwa vipindi viwili mpaka alipoastaafu Januari 2018.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *