Fahamu saikolojia ya msichana aliyepata mimba katika umri mdogo

Jamii Africa

Elimu ni njia sahihi ya kumkomboa mwanadamu kifikra na kumuwezesha kumudu mazingira yanayomzunguka ili kufikia malengo aliyojiwekea. Kwa kutambua umuhimu wa elimu, serikali imeweka mfumo mzuri ambao haubagui  jinsia ya mtu katika kupata maarifa ya msingi kwa faida ya jamii.

Licha ya mfumo wa elimu kuwa mzuri lakini bado mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni ambazo wanafunzi wa kike huzipata wakiwa bado shule na hivyo kudidmiza harakati za kuongeza idadi ya wanawake wasomi katika ngazi za maamuzi.

Tatizo la mimba za utotoni bado ni changamoto ambayo inahitaji nguvu ya pamoja ikizingatiwa kuwa idadi ya wasichana waokatiza masomo inaongezeka kila mwaka. 

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu (UNESCO) zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wasichana wote wanaondikishwa katika shule za msingi nchini Tanzania hawamalizi masomo yao kwa sababu ya kupata mimba wakiwa shuleni, hivyo hulazimika kuacha masomo na kwenda kulea watoto wao.

“Baada ya kugundulika nina mimba nilifukuzwa nyumbani na hata mwanaume aliyenipa mimba alinikataa”, hayo ni maneno ya msichana Fatuma Maulid (17) mkazi wa Mtwara, ambaye alilazimishwa kufanya ngono na kupata mimba.

Anasema ndugu zake wote walimkataa akakimbilia Dar es Salaam kwa dada yake, ambapo amejifungua mtoto wa kiume Aprili mwaka huu. Lakini anaishi katika hali ngumu huku mtoto wake akisumbuliwa na magonjwa ya mara kwa mara.

Zipo sababu nyingine za  wasichana kukatiza masomo yao ikiwa ni pamoja; utoro, umbali mrefu kati ya shule na nyumbani, mazingira duni ya kujifunzia na kukosa elimu ya uzazi.  Changamoto hizi huwalazimisha wasichana kuingia kushiriki vitendo vya ngono katika umri mdogo na matokeo yake ni kupata mimba.

UNESCO inaeleza kuwa wasichana wasiopungua 5,000 kila mwaka katika shule za msingi huacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni.  Lakini katika mwaka, kati ya siku 186 na 187 wanafunzi wa kike hawafiki shuleni  kwa sababu ya matatizo ya hedhi.

 

 Athari za Kisaikolojia

 Mtaalamu na Mshauri wa Masuala ya Saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii Tanzania, Zainabu Rashidi amesema mimba za utotoni zinaathiri mwenendo na tabia za msichana ambapo asipopata matibabu ya kisaikolojia uwezekano wa kufanya ukatili akiwa mtu mzima ni mkubwa.

“Mimba ina madhara mengi zaidi, msichana anaweza kumkataa, kumkimbia mtoto. Lakini anapokuwa na Yule mtoto uchungu unazidi kwahiyo anaweza akaendeleza tabia ambazo sio nzuri dhidi ya Yule mtoto ikiwemo kumpiga”, anaeleza Mtaalamu wa Saikolojia.

Anasema ikiwa msichana aliyepata mimba akipata matibabu anaweza kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na maisha yake. Anaishauri jamii kutoficha ukatili wa kijinsia lakini wawasaidie waathrika kupata matibabu.

 Wanaharakati Wanena

 Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga akizungumza katika ufunguzi wa Siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia amesema jukumu la ulinzi na malezi bora kwa watoto ni la jamii nzima wakiwemo wazazi, marafiki, walezi, viongozi.

“Tushirikiane na serikali kuboresha na kusimamia utekelezaji wa sera na kubadilisha sheria kandamizi ili wahusika wa ukatili huu hasa kwa watoto kike wawajibishwe kwa mujibu wa sheria”, ameshauri Edda Sanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI),Janeth Mawinza anasema matukio ya wasichana kupewa mimba na kutekelezwa yamekuwa kikwazo kwa wasichana kufikia ndoto zao.

Ameitaka jamii kupaza sauti na kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wasichana ili wapate nafasi ya kusoma na kutimiza ndoto zao za kielimu.

 

Msimamo wa Serikali

 Serikali imezifanyia maboresho Sera na Sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba za utotoni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Elimu sura 353 ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya Msingi na Sekondari.

Katika kutokomeza ndoa na mimba za utotoni Serikali imeanza utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo aina zote za ukatili na kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo mwaka 2020.

 

 Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katika Lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s 2030) linasisitiza Usawa wa Kijinsia katika jamii na linakusudia kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika sekta binafsi na Umma ikiwemo usafirisha wa watoto, udhalilishaji kingono na aina zote za unyanyasaji ifikapo 2030.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *