Mihadarati: Freeman Mbowe, Simon Sirro kuibua mjadala wa kisheria

Jamii Africa

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Aikael Mbowe, amegoma tena kuitikia wito wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam uliotolewa kupitia vyombo vya habari na Kamanda Simon Sirro.

Hatua hiyo inawafanya sasa polisi kutumia mbinu za medani kumsaka kiongozi huo wa upinzani ambaye aliitwa kwa ajili ya mahojiano yanayohusu vita dhidi ya mihadarati.

Lakini wakati Polisi wakiahidi kutumia mbinu za kikachero kumsaka Mbowe, upande mwingine wanasheria wa mwanasiasa huyo wamefungua shauri Mahakama Kuu kuwashtaki Mkuu wa Mkoa Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Simon Sirro, na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda hiyo, Camillius Wambura, shauri ambalo linatarajiwa kuzua mvutano wa kisheria kesho Jumanne.

Jumamosi, Februari 18, 2017 Kamanda Simon Sirro kupitia vyombo vya habari alimtaka Mbowe kujisalimisha Polisi mara moja kwa ajili ya mahojiano hayo baada ya kutajwa kwenye orodha ya watu 65 wanaodaiwa kujihusisha na utumiaji na biashara ya mihadarati, ikiwa ni utekelezaji wa amri iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Polisi wanaeleza kwamba, waliamua kutumua vyombo vya habari kama ndiyo njia pekee baada ya juhudi za kumsaka katika makazi yake kushindikana huku simu yake ya mkononi ikiwa imezimwa.

Wakati akizungumza na wanahabari Jumamosi, Kamanda Sirro alisema Mbowe alikuwa amemahidi kwenda mwenyewe kituo kikuu cha Polisi Kati Februari 15, 2017, lakini hakwenda, na jeshi la hilo lilimtafuta usiku na mchana katika makazi yake bila mafanikio huku simu yake ya kiganjani ikiwa imezimwa.

Jana Jumapili, Februari 19, 2017, wanasheria wa Mbowe walitoa taarifa kwamba, mteja wao alisema polisi wanamuita kwa amri ya Mkuu wa Mkoa hata kama wanadai ni wao wanamuita.  

Kwa hiyo Mbowe alisema anayetaka kumkamata ni Mkuu wa Mkoa na anataka Mahakama itoe tamko kuhusu hilo na pia ifute mamlaka ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kukamata watu wakati nyakati za sasa kuna vyombo maalum.

Taarifa kutoka ndani ya Chadema zimethibitisha kuwa Sirro alichukua uamuzi huo baada ya kupelekewa wito wa Mahakama Kuu ya Dar es Salaam kumtaka yeye, na Mkuu wa Upelelezi, Camilius Wambura na Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kufika mahakamani siku ya Jumanne.

“Sirro alipopelekewa alisema apelekewe mkuu wa upelelezi, Mkuu wa upelelezi naye akasema apelekewe Makonda. Hii ni makosa kisheria, kukataa wito wa mahakama kuu.

“Na muhimu zaidi ni kwamba Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam ni mdaiwa wa kwanza, akifuatiwa na hao wengine. 

“Kukataa kupokea wito wa mahakama kunaleta maana kwamba pengine hawataki kuheshimu mchakato wa kimahakama sababu  busara ya kisheria ni kwamba kwa kuwa suala liko mahakamani; wao hawawezi kuendelea na kumuita Mbowe wakati Mbowe anahoji utaratibu wa yeye kuitwa/kukamtwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa tena baada ya kutajwa hadharani na kushushiwa hadhi yake kinyume na haki zake za kikatiba,” anasema Wakili Peter Kibatala.

“Sirro alipatwa na hasira baada ya kupokea wito wa mahakama, lakini sisi tunamshauri afuate taratibu za kisheria, wito wa polisi hautolewi kwa njia ya vyombo vya habari, Sirro afuate sheria kama hatamwona Mwenyekiti akienda bila shida, kwa sasa japo sipo Dar es Salaam ningekuwapo nisingemshauri Mbowe kwenda polisi,” anasema Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu.

Mbowe anahoji pia kama Mkuu wa Mkoa ana mamlaka ya kukamata watu kwa makosa yenye mamlaka maalum kuyachunguza na anapinga suala la polisi na Mkuu wa Mkoa kuendesha suala kwa mtindo wa trial by media na kangaroo court kinyume na katiba na sheria za jinai zinazoakisi katiba

“Sirro alipatwa na hasira baada ya kupokea wito wa mahakama, lakini sisi tunamshauri afuate taratibu za kisheria, wito wa polisi hautolewi kwa njia ya vyombo vya habari, Sirro afuate sheria kama hatamwona Mwenyekiti akienda bila shida, kwa sasa japo sipo Dar es salaam ningekuwapo nisingemshauri Mbowe kwenda polisi” anasema Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *