BAADHI ya kaya zinazofuga kuku na wanyama wadogo wadogo wilayani Muleba zimelalamika kutofikiliwa kupata chakula cha msaada kwa madai kuwa mifugo yao ni kipimo cha kaya zenye uwezo.
Wakihojiwa kwa nyakati tofauti na mtandao wa Fikrapevu wilayani humo, baadhi ya wananchi wa kata ya Mushabago wameeleza kuwa katika mikutano ya vijiji walielezwa kuwa kaya yenye mfugo wowote haitakiwi kupata chakula cha msaada.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, Theobard Willibard mkazi wa kijiji cha Kyanshenge alidai kigezo hicho kimeziacha familia nyingi zisizo na uwezo zisiwe katika orodha ya watakaopata msaada.
Alilalamikia mifugo kama kuku kutumika kama kigezo cha kunyimwa msaada na kuwa hata familia zenye wanyama kama mbuzi,wengi huwamili kwa mkopo wakitegemea kupata mbolea.
Mwananchi mwingine Dominick Kamugisha alidai kuwa ufugaji unaofanywa na wananchi wanaolilia msaada wa chakula ni ule wa mfugo mmoja mmoja ambao hauwezi kukidhi mahitaji makubwa ya janga la njaa linalowakabili kwa sasa.
Akihojiwa kuhusu utaratibu uliotumika katika eneo lake mwenyekiti wa kitongoji cha Nyarubare kijiji cha Kashozi kata ya Buganguzi Charles Mini alisema takribani kaya zote ziko taabani na kuwa walitoa kipaumbele kwa kaya zenye hali mbaya zaidi.
“Nakubaliana na malalamiko ya wananchi kaya zangu zote sabini ziko taabani kwa kukosa chakula, zimechaguliwa familia kumi na nane tu na wengi wasio na uwezo wamebaki”alibainisha na kuwa umiliki wa mifugo si miongoni mwa kigezo kilichotumika.
Awali wananchi wa kijiji hicho Rwihula Felician na Thobias Kalumuna walidai malalamiko yao ni kutaka kupata mgawo sawa na kuwa janga la ukame na magonjwa yaliyoshambulia mazao ikiwemo migomba hayakubagua familia yoyote.
Alipoulizwa kwa njia ya simu na Fikrapevu ili kujua kinachoendelea kuhusu taratibu za ugawaji wa chakula cha msaada,Mkuu wa wilaya hiyo Angelina Mabula alisema alikuwa safarini kuelekea kata ya Nyakabango na kutaka atafutwe baada ya nusu saa,
Alisema kwa ufupi kuwa chakula hicho tayari kimefika kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kata aliyokuwa anaelekea ingawa alipotafutwa tena, simu ilipokelewa na msaidizi wake aliyedai mkuu wa wilaya alikuwa anaendelea na kikao.
Picha: Moja ya mkungu wa ndizi ulioathiriwa na ugonjwa wa unyanjano katika kata ya Buganguzi ikiwa ni miongoni mwa magonjwa yanayotishia kutoweka kwa zao hilo wilayani Muleba.
Habari hii ni kwa mujibu wa mwandishi wa FikraPevu aliyeko mkoani Kagera