Foleni vituo vya afya kikwazo kwa wananchi kupata huduma bora

Jamii Africa
Nurse and patient talking in hospital

Huduma bora za afya ni haki ya msingi ya kila mtu lakini changamoto katika sekta ya afya nchini huwa kikwazo kwa wananchi kuzipata huduma hizo kwa wakati.

Uhaba wa madaktari na wahudumu wa afya ni sababu mojawapo inayowafanya wananchi kusubiri kwa muda mrefu katika vituo vya afya kabla ya kupata matibabu.

Aidha, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa Tanzania bado ina uwiano usioridhisha wa daktari kwa wagonjwa ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa katika nafsi ya mwisho duniani kwa kuwa na uwiano wa daktari mmoja kwa wagonjwa 50,000.

Fikra Pevu inaelezwa kuwa kwa sasa uwiano kati ya daktari na wagonjwa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 25,000, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaitaka Tanzania kuwa na daktari mmoja kwa wagonjwa 8,000.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sasa Tanzania ina upungufu wa madaktari unaofikia asilimia 49.

Akizungumza hivi karibuni na vyombo vya habari, Mganga Mkuu wa serikali, Prof. Muhammad Kambi amesema kuwa kwa tathmini iliyofanywa na serikali, wanahitajika madaktari takribani 3,510 na mahitaji makubwa yapo katika hospitali za Wilaya ambapo wanahitajika madaktari (832), hospitali za rufani za mikoa (460), vituo vya afya (816), hospitali ya Bugando (152) na hospitali ya Taifa Muhimbili madktari (235).

Mpaka kufikia Julai mwaka huu, kulikuwa na wanafunzi 2,843 waliohitimu mafunzo ya udaktari na hawajaajiriwa na serikali ili kuziba pengo lililopo la uhaba wa madaktari nchini.

Serikali imekuwa ikieleza kuwa uhaba wa madaktari katika vituo vya afya hautokani na uchache wa madaktari bali uwezo wa kuwaajiri wahitimu wote kwa wakati mmoja.

Ripoti ya shirika la Twaweza ya mwaka 2017 kuhusu huduma za afya na ustawi wa jamii inathibitisha kuwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi wanakumbana na uhaba wa madaktari wakienda kutibiwa katika vituo vya afya.

“Wananchi watatu kati ya kumi (29%) waliohojiwa wanasema hawakukuta madaktari, na idadi sawa na hiyo walikuta huduma zikiwa ghali sana au wahudumu wa kituo cha afya hawakuwajali au kuwaheshimu”. Inaeleza ripoti hiyo.

Changamoto nyingine inayojitokeza ni muamko mkubwa wa wananchi kwenda kutibiwa katika vituo vya afya vya serikali lakini wakifika kwenye vituo hivyo hukutana na foleni na kulazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kutibiwa.

Kulingana na ripoti ya Twaweza inaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita wananchi sita kati ya kumi (61%) walienda kwanza kutibiwa katika vituo vya serikali.

Na idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita ambapo chini ya wananchi 5 kati ya kumi walienda kutibiwa katika vituo vya serikali.

Uhaba wa madaktari na wananchi wengi kwenda kutibiwa katika vituo vya serikali umezidisha tatizo la wananchi kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupata matibabu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa tatizo kubwa lililojitokeza sana ni muda wa kusubiri kupata huduma kwenye vituo vya afya. Ripoti inasema, “Wananchi sita kati ya kumi (63%) walioenda kupata matibabu wanasema muda wa kusubiri ni mrefu sana”.

Kwa muktadha huo zaidi ya nusu ya wananchi wanaotibiwa katika vituo vya afya hawapati huduma kwa wakati jambo linalowaletea usumbufu na kusababisha migongano kati yao na wahudumu wa afya.

“Wananchi watatu kati ya wanne (76%) wanaoenda kupata matibabu katika vituo vya afya husubiri chini ya saa moja kabla ya kuhudumiwa. Mwananchi mmoja kati ya watano (20%) hulazimika kusubiri zaidi ya saa moja”. Ripoti hiyo inabainisha.

Kutokana na ongezeko la vituo vya afya vya serikali, idadi ya wananchi wanaotibiwa katika vituo vinavyomilikiwa na watu binafsi, makanisa au mashirika yasiyo ya kiserikali imepungua kwa 4% ikilinganishwa na 2016 ambapo ilikuwa 20%. Mgonjwa mmoja kati ya wagonjwa kumi (10%) katika vituo binafsi vya afya husubiri zaidi ya saa moja, ukilinganisha na wagonjwa wawili kati ya kumi (22%) katika vituo vya afya vya serikali.

Hali hiyo husababisha wagonjwa wengine kufariki wakiwa kwenye foleni na wengine kurudi nyumbani kwasababu tu wameshindwa kusubiri kwa muda mrefu.

Mtafiti kutoka shirika la Twaweza, Nellin Njovu, anasema sekta ya afya bado inakabiliwa na changamoto nyingi na suala la wagonjwa kusubiri kwa muda mrefu bado linawatesa wengi. Anashauri changamoto ya muda wa kusubiri iangaliwe ili kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma bora.

“Tuna upungufu wa madktari tayari, na watu kwenda katika vituo vya afya na wengi kuhudumiwa ndani ya saa moja ni jambo la kusheherekea japokuwa wagonjwa ni wengi na mtu ameweza kuhudumiwa ndani ya saa moja”,

“Lakini hiyo isiwafanye watu waone ni sawa, inabidi muda upungue zaidi kwasababu watu wengine wanaumwa sana na wanahitaji huduma kwa haraka zaidi”. Anasema Bi. Nellin Njovu.

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameitaka serikali kuwajibika kwa wananchi wake na kuitaka kutengeneza mfumo thabiti wa kusimamia utoaji wa huduma bora za afya.

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ya 2030 hasa lengo la 3 linasisitiza kuweka mifumo imara ya utoaji huduma za afya ili kuhakikisha watu wote wanakuwa na afya bora.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *