Gazeti la MAWIO laibwaga Serikali Mahakamani. Kurejea mtaani Alhamisi wiki ijayo

Jamii Africa

HATIMAYE gazeti la MAWIO lililofutwa na serikali ya Tanzania na kuacha kuchapishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, limerejea mtaani kwa uamuzi wa Mahakama Kuu.

Serikali ililifuta gazeti hilo na kulizuia kuchapishwa kwa njia yoyote ile Januari 15, mwaka jana- 2016.

Uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Jumanne ya wiki hii, umetupilia mbali amri ya serikali ya “kuliua na kulizika kabisa” gazeti hilo lililokuwa likitoka kila wiki – Siku ya Alhamisi.

Mahakaka Kuu ilisema kuwa amri ya serikali kuliua MAWIO haikuwa sahihi, hivyo “gazeti hilo lilionewa.”

Jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo, limesema gazeti la MAWIO halikupewa nafasi ya kujitetea kabla ya hatua ya serikali ya kulifuta kutoka orodha ya msajili wa magazeti nchini.

Msajili wa magazeti nchini ni Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO).

Jaji Ignas Kitusi ndiye alisoma uamuzi wa Mahakama kuu – kwa niaba ya jopo siku ya Jumanne, wiki iliyopita (Februari 28). Jaji mwingine aliyekuwa kwenye jopo hilo, ni Jaji Ama-Isario Munisi.

Serikali ililifuta gazeti la MAWIO tarehe 15 Januari 2016 baada ya kudaiwa kuandika ilichoita habari na makala za “kichochezi.”

Utawala wa Kampuni ya Victoria Media Services Limited, wachapishaji wa gazeti la MAWIO, uliamua kufungua kesi mahakamani. Hii ni kesi Na. 15 ya mwaka 2016.

Wakili wa MAWIO, Dk. Rugemeleza Nshalla, ameiambia FikraPevu kuwa hatua ya serikali iliegemea falsafa ya “…Nyonga kwanza na sikiliza baadaye.”

Dk. Nshalla amesema katika mazingira yoyote yale, sharti walalamikiwa wapate nafasi ya kujieleza na kusiklilizwa na mahakama kwanza kabla ya hukumu kutolewa.

FikraPevu lilimpata Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa gazeti la MAWIO, Simon Mkina ambaye amesema alishangazwa sana na hatua ya serikali kufuta alichoita “mdomo wa wananchi.”

“Kufuta chombo hiki au kingine kama hiki, ni kukiri kuwa serikali haipendi kusikia kutoka kwa wananchi…” amesema Mkina katika mahojiano na FikraPevu.

Mkina amesema MAWIO limekuwa gazeti linalozingatia maadili na kufuata weledi wa hali ya juu katika kuandika na kuchapisha habari na makala na kuongeza kuwa limekuwa gazeti pekee linalotoa uwanja mpana kwa wananchi kuandika mawazo yao ili kuchochea uwajibikaji wa viongozi wa serikali.

Mkina amesema kufuatia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, MAWIO litarejea mtaani Alhamisi ya wiki hii na kuahidi kuwapa wasomaji wake habari zilizofanyiwa kazi ya ziada.

“Kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, wakati gazeti halipo mtaani – likiwa limefutwa na serikali, pamoja na kupoteza ajira za watu na kuingia katika hasara kubwa, bado tulikuwa na kazi ya kujiuliza ni wapi tulikosea na je, lini tutapewa haki yetu? Bahati nzuri haki yetu imefika,” aliongeza Mkina akiongea na FikraPevu.

Uamuzi na hatua ya kulifuta MAWIO, lililokuwa likichapishwa kila Alhamisi, ulitangazwa na Nape Nnauye, Waziri wa habari, vijana, utamaduni, sanaa na michezo.

Tangazo lililotolewa katika gazeti la serikali, Na. 55 la Januari 15, 2016, lilisema serikali inachukua uamuzi wa kulifuta kwa mujibu wa mamlaka iliyonayo kupitia Sheria ya Magazeti ya 1976; sura ya 229 kifungu cha 25(1).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *